June 9, 2019

KILA kitu kwa sasa kinaanza upya hasa kutokana na ushindani ambao tumeuona msimu uliopita, hivyo ni muda mwafaka kwa timu zote kukaa chini na kufanya tathimini ya kile walichokifanya.

Hakuna anayeweza kufikia mafanikio makubwa endapo atasahau kuangalia pale alipokwama na kuanza kusonga mbele kwa ajili ya kuyafuata mafanikio.

Klabu zote ambazo zimeshiriki ligi kuu, ligi daraja la kwanza pamoja na ligi ya wanawake muda huu uliopo ni muda wa kujipanga na kuanza kuweka malengo upya.

Wapo ambao msimu uliopita walikuwa na malengo makubwa mwisho wa siku yote waliyopanga hawakuweza kulifikia hata lengo moja sio mbaya kwa kuwa ulikuwa ni mwanzo.

Sasa kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kuyatazama upya malengo na kufanya tathimini ni wapi ambapo mlikosea na kwa nini mlikosea?.

Mkijiuliza maswali haya itakuwa ni hatua moja nzuri ya kuanza kusonga mbele kuyafuata malengo ambayo mmejiwekea kwani tayari mtakuwa mmepata picha ya kile ambacho kiliwakwamisha.

Ni muda mzuri sasa viongozi wote kukaa chini na kuanza kutafakari mapya na kusahau kwa yale mabaya yaliyopita ili kuanza upya kujenga timu zenu.

Tunajua kwamba zipo ambazo zilifikia malengo hizo zinastahili pongezi na jambo ambalo linatakiwa kufanyika ni kuanza kujipa changamoto mpya kwa ajili ya msimu ujao.

Wengi wanafikiria kwamba mafanikio hutokea siku moja jambo ambalo limewafelisha wengi ni lazima kuwe na subira pamoja na uvumilivu katika kuyafikia mafanikio.

Mwendo wa haya yote pia uwe ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujitathimini pia katika uboreshaji wa kazi zao isije kutokea mapungufu kama ambayo yamekuwa yakionekana.

Zama kwa sasa zimebadilika kila kitu kinatakiwa kifanywe kwa uwazi na usawa masuala ya kuchanganya data yanaishusha thamani ligi yetu.

Tumeona namna ilivyokuwa ukianzia mwanzo mpaka mwisho wa ligi mengi yaliyokuwa yanapangwa yalikuwa yanapanguliwa na wenye mamlaka hivyo hizi ni kasoro ambazo zinatakiwa zipatiwe dawa.

Mpangilio bora utaboresha ligi yetu ambayo kwa kiasi fulani haijapiga hatua bado ipo palepale hasa kwenye upande wa waamuzi na uendeshaji.

Kwa sasa itapendeza klabu zote zikaanza kujipanga kwa ajili ya msimu ujao hasa ukizingatia kwamba kuna mengi ambayo yapo hayajatekelezwa kwenye ligi yetu.

Kila mmoja anatambua kwamba kinachotengeneza timu bora ya Taifa ni ligi bora hivyo namna ligi inavyokwenda ndivyo timu yetu ya Taifa inavyokuwa.

Licha ya kuwa na wachezaji wengi ambao wanacheza nje bado haitoshi kusema kwamba tumepiga hatua kubwa mapungufu yaliyopo yakifanyiwa kazi italeta picha nzuri hapo baadaye.

Haiwezekani kutegemea kupata timu bora ya Taifa huku ligi yetu ikiwa haina ubora tutakuwa tunajifurahisha sisi wenyewe na itatugharimu wenyewe pia.

Ligi bora haijengwi kwa maneno bali vitendo vinapaswa vifanyike muda wote hasa kwa ajili ya kupunguza makosa na kutendea kazi changamoto zote zilizopita.

Mambo mengi ya kukumbushana kwa sasa ni pamoja na umakini na ubora wa miundombinu yetu ambayo tunaitumia hasa kwa muda huu wa ligi ikiwa imeisha.

Ligi yetu inahitaji maboresho makubwa hali itakayofanya wakati ujao tufanye makubwa kwenye mashindano ambayo tutashiriki kila mmoja atumie nafasi yake kutekeleza kile ambacho kinatakiwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic