August 9, 2019






Na Saleh Ally
WIKIENDI hii msimu mpya wa 2019/20, utaanza rasmi katika sehemu mbalimbali duniani. Tunaanza kuona mpira wa ushindani na kujifunza mengi wakati tukiburudika.


Wakati tunakwenda kuanza msimu, kabla ya kuanza kupata mapya tunaweza kujifunza mengine ili kuingia katika msimu mpya tukiwa na kile kinachotuwezesha kutafakari.


Moja ya hayo ni kuhusiana na namna ambavyo mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere anaonekana kuwa na njaa ya mafanikio kwa kiasi kikubwa.


Kiasili, Kagere ni mzaliwa wa Uganda lakini aliamua kubadilisha uraia na kuwa Mnyarwanda. Kwa sasa ndiye mshambuliaji hatari zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Nasema Kagera ni hatari zaidi kutokana na takwimu za ufungaji wa mabao. Ligi Kuu Bara kwa sasa ndiyo ligi ngumu zaidi kuliko nyingine za ukanda huu na pia ni ligi maarufu na inayolipa vizuri tofauti na zile za Uganda, Kenya na hata Rwanda na Burundi.


Kagere alikuwa Mfungaji Bora Ligi Kuu ya Kenya, msimu uliofuata ambao ni uliopita baada ya kujiunga na Simba, ameibuka mfungaji bora akifunga mabao 23, katika msimu mmoja na kuingia kwenye rekodi ya kuwa mmoja ya washambulizi waliofunga mabao mengi zaidi hadi mwisho wa msimu. Hii ni tokea kuanzishwa kwa ligi hiyo.


Mabao 23 si jambo dogo na kama haitoshi kuthibitisha yeye ni hatari, Kagere akafunga mabao mengine sita katika Ligi ya Mabingwa Afrika alianza hatua ya awali hadi robo fainali. Hakuna ubishi tena yeye ndiye “Mfalme wa Nyavu” kwa ukanda wetu.


Katika hali ya kawaida, ungeweza kufikiria kuona mabadiliko kidogo kwa Kagere kuanza kusumbua, mfano kuchelewa kambini, kuomba ruhusa na kuchelewa kurejea au vinginevyo.


Ungeweza kuanza kusikia, Kagere amezozana na uongozi au kususia kitu fulani kama ambavyo tumesikia sana kwa wachezaji wengine wa kigeni ambao wamekuwa nyota katika klabu zetu za Tanzania.

Achana na wageni, hata wenyeji wengi ambao baada ya kupata mafanikio kidogo tu, tumekuwa tukisikia rundo la vituko na wakati mwingine kugoma, ulevi, kuchelewa basi, kuchelewa mazoezini na kadhalika. Lakini Kagere ni “Kazi tu.”

Kagere anaonakena hajalewa sifa kwa kuwa si kwamba amekuwa supastaa baada ya kutua Simba. Lakini amekuwa akiendeleza kilea anachofanikiwa kukipata badala ya kulewa sifa na hii inaonyesha bila ya ubishi atafika mbali zaidi.

Tayari kumekuwa na dalili kwa timu kutoka Misri hasa zile kubwa kuanza kumzungumzia. Maana yake kuna nafasi baada ya msimu huu au katikati kuondoka zake na kusajiliwa kwingine kwa fedha nzuri na maslahi mazuri kwake.

Kagere huyohuyo, msimu unaanza tayari amepachika zaidi ya mabao matano ikiwemo hat trick ya kwanza katika Simba Day. Alifunga mabao matatu Simba ikiitwanga Power Dynamo kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, juzi.

Angalia huyu mtu alivyo na njaa ya mafanikio kila kukicha na siku chache zijazo tutaanza kuzungumza kwamba aliwahi kucheza Simba. Anachofanya si kitu kidogo, lazima nyuma yake kuna maumivu kwa maana ya kujituma, kutopumzika kwa maana ya kufanya mazoezi zaidi na zaidi.

Pamoja na hivyo, lazima ukubali kwamba kuna vitu anajinyima kwa ajili ya kuwe na mwendelezo sahihi ambao wachezaji wengi wazalendo wanakosa.


Si kwamba hatuna kabisa, wapo na mfano mzuri ni kama akina John Bocco. Lakini tunahitaji kuwa na wachezaji wengi wazalendo wenye njaa ya mafanikio na uwezo wa kujinyima na kujiendeleza zaidi na zaidi.


Mafanikio yaanzie nyumbani baada ya hapo, mkayapate ugenini lakini kumbukeni, bila njaa ya mafanikio, mtaendelea kuyasikia kwa wengine huku mkilalamika tu.







1 COMMENTS:

  1. Umemtaja Boko sawa ila Boko anakosa nguvu kulingana na kimo na umbo lake.Boko hayuko fiti ni mwepesi mno. Yule beki wa Kenya kule kwenye uwanja wa kasarani kenya alimzalilisha Boko na kumgeuza kichekesho. Watanzania vipaji vipo ila ni walaini mno na wabunge walipolisemea hilo wakaonekana wanatoa maneno ya kashfa kwa wachezaji wetu ila ukweli utabakia kuwa ukweli.Nimekuwa nikimfuatilia spika wa bunge muheshimiwa Ndugai mara nyingi huwa hamumunyi ukweli na ni kweli kabisa wachezaji wa kitanzania wengi kama si wote wanakosa nguvu. Yaani hawapo fiti physically. Kwa Simba naweza kutaja wazawa watatu kwa sasa ambao nahisi wamejitenengeneza na wapo vizuri kifiziko nao ni Mkude,Muzamiru Yasini na Erasto Nyoni na nawasihi waendelee katika hali hiyo au wazidishe zaidi kuwa fiti. John Boko angeweza kuwa zaidi ya kagere kama angezingatia mazoezi ya kuukamilisha mwili wake ila watanzania huwaga tunachukilia vitu kirahisi rahisi tu na ndio maana ni wa rahsisi sana kulinganisha na wageni .

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic