LIGI Kuu Tanzania Bara mzunguko wa kwanza hesabu zake ndo zinafungwa kwa sasa ambapo timu zinakamilisha ratiba zao za mwanzo ili kufunga jumla mzunguko huu kabla ya kuanza ngwe ya pili.
Tayari timu nyingi zimecheza mechi zaidi ya 10 jambo ambalo linamanisha kwamba hakutakuwa na viporo kwa timu zitakapoanza mzunguko wa pili.
Kushindwa kuwa na timu ambazo zinawakilisha nchi kwnye michuano ya kimataifa ni miongoni mwa sababu ambazo zimefanya kusiwe na viporo vingi msimu huu kwani mechi zote zinachezwa kwa wakati.
Pia hali hii ilisababishwa na watani wa jadi kutovuruga ratiba kwa kupewa zile wiki zao za kujiaanda na badala yake ratiba imekwenda kama ilivyopangwa mwanzo mwisho.
Ni wakati mwingine kuona namna gani timu zote zitajipanga kwa ajili ya mzunguko wa pili baada ya kuvuna kile ambacho walikuwa wanakihitaji mzunguko wa kwanza.
Ukweli ni kwamba ushindani umekuwa mkubwa kwa timu zote Bongo licha ya kwamba zipo timu ambazo mwendo wake ni wa kinyonga bado hazijashtuka kwa kupata matokeo ambayo ni ya kawaida.
Nipende kuzikumbusha timu zote zinazoshiriki ligi kwamba tamati ya ligi ipo njiani wasipojipanga itakuwa ni ajabu kutoamini watakapojiona kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Msimu huu timu nne zinashuka jumla huku zile mbili za mwisho zinacheza mchezo wa playoff kutafuta mshindi atakayepata nafasi ya kushiriki ligi.
Yule ambaye atashinda ndiye atacheza mechi za ligi kwani hapa timu mbili ni zile za ligi ambazo zipo nafasi ya 15 na 16 zitacheza na wale waliopo nafasi ya pili kwenye kundi A na B kutoka Ligi Daraja la Kwanza.
Kwa timu ambazo bado zinaona zina mapungufu na hazijafanya usajili basi zijiandae kuvuna kile ambacho wamepanda kwani ukweli hauwezi kuuficha.
Zile ambazo zimetumia dirisha dogo kufanya usajili kulingana na mapungufu yao basi zinastahili pongezi na kutumia vema makosa yao kwa sasa kutengeneza timu.
Dirisha dogo ambalo limefungwa ilikuwa ni maana halisi kwamba timu ziongeze pale yalipo mapungufu yao na kuyafanyia kazi kwa ajili ya mzunguko wa pili.
Ushindani unazidi kushika kasi kwa sasa kwenye ligi na kila timu ina hesabu zake za kupata matokeo mazuri hakuna timu ambayo inafikiria kupoteza hivyo ni muhimu kujipanga.
Wachezaji nao wana kazi ya kuanza kujipanga na kutoa burudani kwa mashabiki wao ambao wanahitaji kuona timu inafanya vizuri kwenye mechi zote.
Kushindwa kwao kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao zilizopita kutafutiwe tiba kwa sasa na kuanza kupambana kwa ajili ya kurejesha furaha ambayo ilianza kumeguka kwa mashabiki.
Hakuna shabiki ambaye anapenda kujitokeza uwanjani na kuona timu inafungwa tena kwa makosa ambayo yalipaswa yafanyiwe kazi wakati wa dirisha dogo la usajili.
Kazi kubwa inayotakiwa ni kwa benchi la ufundi kupambana kutafuta matokeo mazuri ambayo yatawafanya mashabiki wawe na furaha kwenda uwanjani na kurudi wakiwa wamepata burudani.
Wachezaji wapya ambao wamepata kujiunga na timu mpya kwa sasa ni wakati wao kujiongeza na kupambana kuonyesha kile walichonacho bila kuzembea wakiwa uwanjani.
0 COMMENTS:
Post a Comment