Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema kuwa watafanya mazoezi mfululizo bila kupumzika ili kukifanya kikosi hicho kurudi kwenye ubora wake kabla ya kuanza mbio za kumalizia michezo 10 ya Ligi Kuu Bara waliyobaki nayo.
Vivier raia wa Burundi, alisema ameridhishwa na namna ambavyo wachezaji wake wameanza mazoezi, hali inayoonyesha kuwa kila mchezaji alifuata vizuri program yake, ingawa bado kuna tatizo dogo la utimamu na nguvu kwenye miguu jambo ambalo linahitaji muda kidogo kuliweka sawa.
Tangu Jumatano ya wiki hii, Azam FC walianza mazoezi wakijiwinda na michezo iliyosalia ambapo mbali na Ligi Kuu Bara wanaposhika nafasi ya pili, pia wana kibarua cha kucheza na Simba katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA.
"Wengi wanaonekana kukosa nguvu za miguu kwa sababu wamekaa muda mrefu bila kucheza mpira, ila tumetenga siku 12 za kufanya kazi ngumu ambazo hizo zitawafanya wote wawe fiti na kufanya vizuri uwanjani.
"Tunafanya mazoezi maalumu kwa ajili ya kukaa na mpira mguuni na kuulinda usipotee kirahisi, hilo nimeona limeanza kufanikiwa, ingawa bado tunahitaji muda kidogo kwa ajili ya wachezaji kurudisha nguvu za miguu ambazo kidogo zinaonekana kupungua," alisema Vivier.
0 COMMENTS:
Post a Comment