ZIMEBAKI siku 13 kwa sasa kabla ya kuifikia Juni 13 ambapo vumbi ya Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili inatarajiwa kuanza kuonekana kwa wapenzi wa soka na familia ya michezo kiujumla.
Ile burudani ambayo ilikuwa imekosekana inatarajiwa kurejea upya ambapo kwa sasa ni lala salama kwa mzunguko wa pili na hatimaye bingwa atajulikana atakuwa nani.
Bado ninaona kwamba timu nyingi hazipo tayari kwa sasa kutokana na kuyumba kwenye masuala ya kiuchumi jambo ambalo linawafanya wakate tamaa mapema.
Kuna mchezo ambao huenda mambo yasipotazamwa ligi itapoteza mvuto kwa kuwa hakutakuwa na ule ushindani wa kweli kisa suala la ukata ambalo linazitesa timu nyingi.
Ukitazama kwa sasa labda unaweza kusema angalau timu nne pekee zinaweza kumudu gharama bila kusuasua lakini sio kwa kiwango ambacho kinafikiriwa kuwa kama ilivyokuwa awali.
Zipo timu nyingine ambazo zipo nafasi ya chini hazina uhakika kabisa wa kumaliza ligi zikiwa zimeshajinasua hapo zilipo kutokana na ukata ambao unazikumba.
Ukiachana na timu nne ambazo hizi kidogo zina unafuu bado kuna umuhimu wa kutazama namna ya kuweka usawa kwa timu hizi ambazo zinahaha kwa sasa kutafuta wadhamani.
Nikukumbushe kwamba Machi 17 wakati ligi inasimamishwa kutokana na janga la Virusi vya Corona, Kocha wa Ndanda FC, Meja Mstaafu, Abdul Mingange aliweka wazi kuwa anaamini wachezaji wake wataporomoka kiwango watakaporudi kutokana na ukata ambao wanapitia.
Mbali na Ndanda, Biashara United ambao walikuwa wanakuja vizuri na mpaka ligi kusimama walikuwa nafasi ya 10 wameweka wazi kwa sasa kuwa hali ni tete kwa upande wa kiuchumi.
Mbao FC nao wameweka wazi kwamba mambo sio shwari na habari zinaeleza kuwa baadhi ya wachezaji wamegomea kuripoti kambini kutokana na madai ya mshahara.
Hali ilivyo kwa sasa ni muhimu kutazama namna bora ya kuweza kuziwezesha timu hizi hapa ikiwa ni pamoja na wadau wenyewe bila kusahau mamlaka husika ya michezo Tanzania, Shirikisho la Soka (TFF) kutazama namna ya kuokoa jahazi.
Pia hata kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza na la Pili kuna namna ambayo inatakiwa ifanyike kwa viongozi pamoja na TFF kuona mambo yatakavyokuwa kuzipa sapoti timu hizi.
Ipo wazi kuwa hali kwa sasa sio shwari kwa upande wa uchumi kutokana na janga la Corona ambalo limevuruga mambo mengi lakini haina maana kwamba ndio timu ziache kujipanga hapana ni lazima kila timu ijiweke sawa kumaliza msimu.
Kwa wachezaji kazi yao itakuwa ni moja kupambana ndani ya uwanja kuipa timu matokeo chanya ila mwisho wa siku ni lazima malengo ya timu yatazamwe.
Ukiachana na hilo watu wameanza kupuuzia kuhusu kuchukua tahadhari ya Virusi vya Corona, bado janga hili lipo lazima tahadhari iendelee kuchukuliwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment