June 15, 2020

LIGI Kuu Bara imeendelea Jumamosi, Juni 13 na mechi mbili zilichezwa kwenye viwanja vya Mkwakwani mkoani Tanga na Kambarage kule Shinyanga.

Kule Kambarage, Mwadui walikuwa wenyeji wa Yanga, wakati Coastal wakiwa wenyeji wa Namungo kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Matokeo yamekuwa kama ambavyo wengi hawakutarajia kwani Yanga ilishinda bao 1-0 mbele ya Mwadui, Coastal Union ilipindua meza mbele ya Namungo na kufanya sare ya mabao 2-2.

Ikumbukwe kuwa burudani ya mechi ilisimamishwa kwa muda Machi 17 na imerejea baada ya Serikali kuridhia kwa kueleza kuwa hali ya maambukizi dhidi ya Corona imepungua.

Jana pia mambo yaliendelea Uwanja wa Taifa, Simba ilikubali sare ya kufungana bao 1-1 na Ruvu Shooting huku Azam FC ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Mbao FC.

 Matumaini yangu ni kwamba, tahadhari zote za kujikinga na Corona zinaendelea kuchukuliwa.

Tumeona wenzetu ambao nao ligi zao walisimamisha baada ya Corona kutawala, wameanza kucheza.

Ujerumani walikuwa wa kwanza, kisha wamefuata Hispania ambao nao Alhamisi ilishuhudiwa mechi ya kwanza kuchezwa baada ya kupita takribani miezi miwili na nusu.

Wakati ligi ikirudi, nafahamu kwamba wachezaji mlikuwa kwenye maandalizi ya kutosha kabla na baada ya kuingia kambini.

Kabla namaanisha wakati mlipopewa program maalum na makocha wenu na mkawa mnazifanya, na baada ya kuingia kambini mkaendelea na mazoezi. Hapo mkawa mnaunganishwa kitimu.

Baada ya kuingia kambini, maandalizi yamefanyika kwa zaidi ya wiki mbili ili kurudisha muunganiko kwenye timu na sasa kilichobaki ni kwenda kuyafanyia kazi uwanjani yale ambayo mmeelekezwa na walimu wenu.

Huu ndio muda sahihi kwenu kuvuna mlichokipanda kwani mashabiki na wanachama wa timu zenu watapata kujionea kama kweli mlikuwa mmejiandaa kupata faida au hasara.

Binafsi naamini kwamba kila timu itavuna ilichopanda, sitarajii kuona visingizio vya aina yoyote kwani nafasi ya kujiandaa mlikuwa nayo.

Wakati huu ambao msimu unaelekea ukingoni, mamlaka husika mnatakiwa kuhakikisha haki inatendeka na kunakuwa hakuna viashiria vyovyote vya upangaji wa matokeo, mchezo uchezwe kwa haki pasi na upendeleo wa aina yoyote.

Ukiangalia msimamo jinsi ulivyo kwa timu zilizo nafasi kumi za chini kila mmoja inaweza kubaki kwenye ligi au kushuka daraja kutokana na uwiano wa pointi baina yao.

Hivyo basi hapa ni pa kuangaliwa kwa jicho la tatu ili kuepuka sintofahamu ambazo zinaweza kujitokeza hapo baadaye na kujikuta tunaharibu taswira ya soka letu ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limejizolea umaarufu mkubwa kwenye ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Tunahitaji kuona soka la ushindani ndani ya uwanja, ikitokea inaonekana wazi timu fulani inapendelewa, ushindani hautakuwepo.

Waamuzi nanyi muwe makini mnapochezesha mechi, yale makosa ambayo mlikuwa mkiyafanya hapo awali yasijirudie tena, yanaleta ukakasi mkubwa.

Mwisho kabisa, ninawaomba wadau wa michezo na kila mmoja wenu kuendelea kuchukua tahadhari kipindi hiki ambacho Corona bado ipo.

Wakati ambao ligi inarudi, tusijisahau kwa kuona kwamba Corona haipo, Corona ipo na tunachotakiwa ni kuendelea kuchukua tadhari kubwa ili tuitokomeze kabisa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic