KOCHA Mkuu wa Yanga Mserbia, Zlatko Krmpotic amewapiga ‘stop’ wachezaji wake kucheza soka la pasi ndefu na badala yake kucheza pasi fupifupi wakati wakiwa na mpira wakishambulia goli la wapinzani.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kwa Yanga kuwafunga Mbeya City bao 1-0.
Mfumo wa soka la pasi fupifupi na nyingi wanazitumia kuzicheza Klabu za Arsenal ya Uingereza na Barcelona ya nchini Hispania wakati timu ikiwa na mpira ikishambulia goli la wapinzani.
Akizungumza na Championi Jumatano, Krmpotic alisema kuwa amechukizwa na aina ya uchezaji wa vijana wake walivyocheza na Mbeya City wakicheza soka la mipira mirefu.
Krmpotic alisema kuwa wachezaji wake walishindwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake aliyowapa kabla ya mchezo huo, huku akiahidi kulifanyia kazi ili kuhakikisha wanacheza vile anavyotaka yeye katika michezo inayofuata ya ligi.
“Licha ya kupata ushindi katika mchezo huu dhidi ya Mbeya City, niseme kuwa sikufurahishwa na namna tulivyocheza, nawapongeza wachezaji wangu walipambana kwa muda wote kuweza kupata matokeo. Haikuwa rahisi kucheza na timu ambayo imeweka wachezaji kumi nyuma ya mpira.
“Kwa wastani sisi tulicheza mpira kwa zaidi ya asilimia 70, muda mwingi tulikuwa eneo la wapinzani wetu, ilihitaji uvumilivu na kutokata tamaa, ni ushindi tulioupigania”
“Bado tuna kazi ya kufanya kwenye timu yetu. Ukiangalia kipindi cha kwanza hatukucheza tulivyotaka, tunapaswa kuweka mpira chini lakini wakati mwingine naelewa wachezaji wangu walilazimika kutumia mipira mirefu,” alisema Krmpotic.
0 COMMENTS:
Post a Comment