May 24, 2021


 WAKATI wa kufanya vizuri kwa timu ya taifa la Soka la Ufukweni, maarufu kama Beach Soccer ni sasa kwa kuwa imekuwa katika maandalizi kwa muda mrefu na wachezaji wamepewa majukumu yao kwa wakati.

Kufika kwao salama mapema nchini Senegal ni mwanzo wa kuweza kuyafikia mafanikio kwa kuwa kila hatua inaonyesha kwamba mipango inakwenda kukamilika.

Tanzania imekuwa ikishindwa kutusua katika mashindano makubwa hasa katika soka la mpira wa miguu katika mashindano mengi sasa inatosha.

Wakati huu iwe ni wakati wa kuweza kupata mwanga kwa ajili ya Soka la Ufukweni na kutusua katika mashindano haya makubwa.

Imani kubwa kwa mashabiki ipo kwa vijana waliopo nchini Senegal kwa ajili ya Afcon ambayo inahusisha soka la ufukweni 2021.

Kuanzia kwa mbinu ambazo walizipata walipoweka kambi visiwani Zanzibar ni mwanzo wa kufikia mafanikio ambayo taifa linahitaji kwa ujumla.

Kila mchezaji ambaye amepata nafasi ya kuwa katika kikosi hiki ni lazima apambane kutimiza majukumu yake kwa wakati ili kupata ushindi.

Uzoefu wa kushiriki Afcon kwa timu ya taifa ya ufukweni ni muhimu kila mmoja kufanya kazi kwa umakini ili kupata ushindi.  

Boniphace Pawasa ambaye ni kocha mkuu na vijana wake ambao ni 14 tayari amekuwa akifanya nao kazi kwa ukaribu hivyo anajua vijana wake wapoje katika hali ya kupambana na namna gani wanaweza kupata ushindi.

Muda ni sasa hakuna muda mwingine ambao upo kwa wawakilishi hawa kimataifa kufanya vizuri na kupata ushindi katika mashindano hayo makubwa.

Itapendeza kila mchezaji akitimiza majukumu yake kwa wakati na kushirikiana katika kutafuta matokeo ndani ya uwanja.

Hakuna kitu kizuri kama kushinda tena ugenini na kwenye mashindano makubwa ambayo yanafuatiliwa na dunia kiujumla.

Awali ilikuwa haifuatiliwi sana ila kwa sasa ule muamko umekuwa mkubwa na kila Mtanzania anatambua kwamba kuna kitu kinaitwa soka la ufukweni.

Ipo wazi kwamba furaha ya mashabiki ni kuona timu inapata matokeo chanya kwa namna yoyote ile hiyo iwe sera kwenye kila mchezo ambao mtacheza.

Wale ambao wamekuwa wakitegea katika mazoezi hilo waliweke kando waongeze umakini katika mashindao hayo ambayo ni makubwa Afrika.

Yule ambaye amekata tamaa kutokana na kushindwa kufanya vizuri kwa timu hiyo kwenye mechi zake zilizopita kwa sasa iwekwe kando kwa sababu matokeo yaliyopita huwezi kuyabadili.


Kwa sasa wakati wa kuyabadili ni kwenye mashindano haya kwa kupambana na kupata matokeo mazuri ambayo yatawafurahisha Watanzania pamoja na wachezaji kiujumla.


Imani yetu ni kwamba mtafanya kazi kwa juhudi na kutimiza kile ambacho mmeambiwa na benchi la ufundi.


Hakuna ambaye anapenda kupata matokeo mabaya hivyo hilo liwekeni kichwani kwamba Tanzania inawaamini na mmepewa jukumu la kupeperusha bendera ya taifa.


Kila kitu kwenye soka kinawezekana ila ni lazima juhudi iwepo na nidhamu pia iwepo katika kutimiza majukumu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic