BAADA ya kuomba kuvunja mkataba wake ndani ya kikosi cha Yanga, Wazir Junior amewashukuru mashabiki na viongozi wa timu yake hiyo ya zamani.
Allibuka ndani ya kikosi hicho akitokea Mbao FC ya Mwanza na alitarajiwa kutatua tatizo la ufungaji ndani ya Yanga ila ngoma ilikuwa nzito.
Ni mabao mawili pekee alifunga kati ya 52 ambayo yalifungwa na timu hiyo ambayo kwa sasa imeweka kambi nchini Morocco ila Junior alibaki Bongo.
Usiku wa kuamkia leo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika:"Nichukue fursa hii kuwashukuru sana wana Yanga kuanzia makocha, wachezaji, viongozi na mashabiki kwa kuniamini na kuwa mmoja wao.
"Haikuwa safari rahisi licha ya kuwa fupi mno.Nilifika Yanga SC nikiwa na malengo makubwa lakini haikwenda kama nilivyotarajia labda kwa sababu zangu binafsi au vinginevyo.
"Ni kawaida yetu sisi wanasoka kukutana na changamoto kama hizi.Nimechukua maumuzi mgumu sana kwangu lakini yote ni kwa maslahi mapana ya ufanisi wangu. Nimeona nihamishie jitihada zangu sehemu nyingine.
"Yamkini sikufikia malengo ya klabu na kutokuwapa mashabiki ile furaha waliyotarajia kutoka kwangu lakini niwatoe shaka kuwa haikuwa dhamira yangu kuwaangusha.
"Niwatakie kila la kheri kwenye safari yenu kuelekea msimu ujao. Tuendelee kuombeana labda ipo siku tutakuwa pamoja tena kama sio, basi nitaendelea kuuenzi upendo na imani mliyoijenga kwangu.
"Najivunia kuvaa nembo ya klabu kubwa hapa nchini. Asante. Mungu kwanza," Wazir.
0 COMMENTS:
Post a Comment