UNAMKUMBUKA yule jamaa mwenye umatemate wa kutosha ambaye aliipa Yanga heshima Kanda ya Ziwa? Wanamuita Yanga Makaga. Aliisimamia shoo ya mechi nne Kanda ya Ziwa za Yanga na wakabeba pointi 12 na wachezaji wakapata mkwanja wa maana. Tena wakapanda na mwewe na maisha yakawa kama Ulaya.
Sasa huyo jamaa amefanikiwa kuiondoa Yanga Dar na uongozi wa juu umeridhia kwamba ndiye mtu sahihi wa kuiongoza timu kwa mechi zao kupigwa CCM Kirumba. Ishu iko hivi. Viwanja vyote vya Dar es Salaam ambavyo ni Uhuru, Taifa na Azam Complex vitafungwa hivi karibuni kupisha marekebisho tayari kwa fainali za Afcon kwa vijana zinazoanza mwezi ujao.
Sasa Yanga wamekaa vikao vya ndani wakakubaliana kwamba Mwanza ndiyo sehemu nzuri kwao haswa kutokana na ushawishi wa Makaga ambaye muda mwingi hayuko nchini.
Kwa mujibu wa Katibu wa Matawi ya Yanga Kanda ya Mwanza, Mhando Madega ni kwamba; “Makaga amehusika sana kuihamishia Yanga Mwanza na amekubali kuendelea kuipambania mpaka mwisho itakapotua hapa. “Uongozi wa juu umeona kwamba ndiye mtu sahihi wa kuisaidia timu kwa sasa ndio maana hata
kwenye kamati mpya iliyoundwa amejumuishwa, anajitoa sana.
“Aliisaidia sana timu kifedha kwenye mechi nne za Kanda ya Ziwa msimu huu tangu ile ya Mwadui, Kagera, Mbao na Alliance wachezaji wameishi maisha mazuri, wamesafiri vizuri ndio maana sasa tunaamini kwamba timu ikija huku itafanya vizuri zaidi,” alisema Madega na kusisitiza kwamba wamejipanga kuhakikisha kila mechi ndani ya Kirumba hatoki mtu salama.
Amesisitiza kwamba wataongeza nguvu ndani na nje ya uwanja kwa kushirikiana na Makaga zaidi ya ilivyokuwa kwenye mechi nne zilizopita kwa vile sasa wameka- bidhiwa timu.
Makaga mbali na biashara zake nyingine za ndani na nje ya nchi, ni muwekezaji kwenye vivuko vya Ziwa Victoria. Tangu aanze kuingiza mkono wake Yanga imeshinda mechi zote nne za Kanda ya Ziwa na kupata pointi 12 ikiwemo ile ngumu dhidi ya Mbao ambayo walikuwa hawafungiki na Yanga.
MSIKIE ZAHERA
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amewang’ong’a wanaofikiria kwamba wakihama Uwanja wa Taifa na kwenda kuvitumia viwanja vingine watakuwa na wakati mgumu kwa kuwaambia wasubiri muda waone watakachofanya.
Zahera ambaye amewahi ndiye kocha pekee aliyewahi kuikopesha timu iliyomuajiri, ameliambia Spoti Xtra linaloongoza kwa mauzo kila Alhamisi na Jumapili kuwa, watakapohamia Kirumba hakutakuwa na shida yoyote ile kwani wamejiandalia mazingira ya kucheza kokote na kupata matokeo mazuri.
“Wanaona kwamba tukihama Taifa ndiyo tutapata matokeo mabaya? Basi wasubiri waone nini ambacho tutakifanya baada ya hapo,” alisema kocha huyo ambaye amebeti kwamba Simba haiwezi kubeba ubingwa wa Afrika msimu huu wala kucheza fainali.
“Hiyo ishu ya kubadili uwanja haiwezi kutuathiri kwa njia yoyote ile kwa sababu tangu mwanzo tulijiandaa kucheza na kupambana kokote pale, nadhani moto huu wa Dar ndiyo tutahamia nao katika viwanja hivyo,” alisema Zahera ambaye anaamini Meddie Kagere wa Simba ndiye mfungaji bora msimu huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment