September 16, 2021


 KAZI bado ipo kwa kuwa wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Azam FC bado wana kibarua kingine cha kufanya mbele ya Horseed FC ya kutoka Somalia.


Licha ya kupata ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa awali uliochezwa Septemba 11, Uwanja wa Azam Complex, benchi la ufundi la timu hiyo limeweka wazi kuwa bado kazi haijaisha watapambana kupata ushindi kuelekea mchezo ujao unaoatarajiwa kuchezwa Septemba 18, Uwanja wa Uhuru.


Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati aliliambia Spoti Xtra kuwa:”Bado kazi haijaisha unajua kwanamna ushindani ulivyo huwezi kusema kwamba upo nyumbani ama upo ugenini. Hawa tulianza nao kwa kasi ila wakatupa tabu hivyo bado tuna kazi ya kufanya kwenye mchezo wetu wa marudio,” .


Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Spoti Xtra liliweka kambi hapo na kuweza kufanya mahojiano na mshambuliaji wa Azam FC ambaye ni ingizo jipya kwa msimu wa 2021/22 anaitwa Idris Mbombo.


Ni Julai 31, Idris Mbombo, alitambulishwa ndani ya Azam FC  kutoka El Gouna ya Misri na alisaini dili la mkataba wa miaka miwili hivyo yupo hapo mpaka mwaka 2023.


Mchezo wake wa kwanza wa kimataifa akiwa na jezi ya Azam FC aliweza kupachika bao moja walipocheza na Horseed FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya awali kwa pasi ya mshikaji wake Salum Abubakar, ‘Sure Boy’ na Azam FC ilishinda mabao 3-1.


 Mbombo alisema kuwa bado hajawa kwenye mawasiliano mazuri na wachezaji wenzake ndani ya uwanja ila kuna jambo linakwenda kutokea mashabiki wawe na subira.



“Bado maisha yanaanza kwenye kikosi hiki na nina amini kwa kadri tunavyozidi kushirikiana tutakuwa imara na nina amini kwamba nitafunga mabao mengi kila ninapopata nafasi.


“Hii haitakuwa kwangu mimi peke yangu bali na wachezaji wengine, unajua yupo mtu kama Pricne Dube, Kola, (Rodgers) ni furaha kuwa na washambuliaji wengi halafu tukafanya vizuri. Umepanga kufunga mabao mangapi?


“Suala la kufunga hilo mimi ninapenda kufanya hivyo hasa ukizingatia kwamba nafasi yangu ni mshambuliaji. Ninachojua ni kwamba nafasi ambazo nitapata nitatumia kufunga ama kutengeneza nafasi za mabao kwa wenzagu.


Kuhusu ushindani wa namba je?


“Hilo napenda liwepo kwani pale penye ushindani inafanya kila mmoja awe imara na akipata nafasi kazi ni kwa ajili ya timu sio mtu mmojammoja.


Mchezo wake wa kwanza unauzungumziaje?


“Ni mzuri na ulikuwa na ushindani unaona kwamba kila mchezaji anakitu anataka kufanya. Nimefunga nafurahi ni furaha yangu, timu kiujumla pamoja na mashabiki.


Hesabu kimataifa na kwenye ligi zipoje?


“Kazi inaanza kwani baada ya mchezo wa kwanza kuisha unakuja mwingine hivyo hapana tunaendelea kupambana ili kupata ushindi. Kwenye ligi pia kuna malengo ya kufanya vizuri hilo lipo wazi.


“Kwa mashabiki ninawaambia neno moja waje kwa wingi kila tunapokuwa tunacheza, waje bila kuhofia tunaamini tutafanya vizuri kwenye mechi zetu kuanzia zile za ligi pamoja na za kimataifa,” alisema.


Mbombo rekodi  


Mbombo alipachika bao dakika ya 72  kwa pasi ya Salum Abubakar, ‘Sure Boy’ akiwa ndani ya 18 likiwa ni bao lake la kwanza kwenye mechi za ushindani.


Aliweza kuingia ndani ya eneo la 18 la wapinzani wake mara 39 na ni mara mbili alikuwa na mpira huku mara 37 akiwa katika eneo hilo bila ya mpira.


Pia alipiga jumla ya pasi 16 na aliweza kukokota mpira mara mbili ndani ya dakika 87 ambazo alitumia na alionyeshwa kadi moja ya njano na mwamuzi wa mchezo huo Djaffari Nduwimana kutoka Burundi pia mshambuliaji huyo aliotea mara nne. Nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji mwenzake Rodgers Kola.


 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic