WAKATI kiungo mshambuliaji Bernard Morrison akimaliza adhabu yake ya kufungiwa michezo mitatu, kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes tayari ameamua kumuandaa kiungo huyo kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Polisi Tanzania.
Morrison aliikosa michezo mitatu ya Simba wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga sambamba na ya ligi kuu mbele ya Biashara United na Dodoma Jiji, kufuatia kuwa na adhabu ya kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Chanzo chetu kutoka Simba kimesema kuwa tayari kocha Gomes ameonekana wazi kumpatia majukumu Morrison kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Polisi Tanzania ambapo nyota wa zamani wa Yanga Kelvin Yondani na Said Makapu wanachezea kwa sasa baada ya kutoka Yanga.
“Kwa mazoezi ya siku hizi tatu imejionyesha wazi kabisa kuwa kocha Gomes anamuandaa Morrison kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Polisi, kwani hata siku tunaenda Mara alitaka kuachwa Dar es Salaam, ila kocha aliomba aende naye.”
Championi Jumamosi lilipomtafuta Morrison ili azungumzie juu ya kumalizika kwa adhabu yake, alisema: “Kinachotakiwa kufahamika kuwa mimi nipo na timu hadi sasa kuanzia tulipokuwa Mara, hivyo adhabu yangu ikimalizika tu, nitaendelea kupambania ushindi wa timu hivyo nipo tayari kwa mchezo uliopo mbele yangu.”
Gomes amesema kuwa anatambua umuhimu wa kila mchezaji kwenye timu yake hivyo hesabu zao ni kuona kila mchezaji anapata nafasi.
0 COMMENTS:
Post a Comment