March 27, 2015


Na Saleh Ally
AKISIMAMA mtu akasema Watanzania ni waoga kupindukia, utaona watu watakavyopandwa jazba kama vile wametukanwa tusi kubwa sana au kudhalilishwa.


Hao watakaopinga au kukasirishwa, wanajua ukweli kwamba Watanzania ni waoga hata kwenye mambo ya kawaida sana. Sisemi waingie kwenye fujo au vurugu ambalo ni jambo baya sana, nazungumzia angalau kwenye kupasa sauti na kutete hoja zao za msingi.

Acha mimi nionekane mkorofi linapofikia suala la kutetea nchi kwa kuwa wengi wetu tunajisahau na kuwatukuza Wazungu tukiamini wanajua kila jambo, kitu ambacho si sahihi hata kidogo.

Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij ametangaza kikosi kitakachocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Kocha huyo raia wa Uholanzi ameita kikosi chake kilekile bila ya kuangalia vigezo ambavyo wote tunavijua. Haihitaji kuwa kocha kutoka Ulaya ili kuelewa uteuzi wa kikosi.

Nooij amemuacha kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuwachukua Mwadini Ally, Aishi Manula pamoja na Deogratius Munish ‘Dida’ ambaye amekuwa benchi kwa zaidi ya mechi saba.

Amewachukua mabeki wawili wakongwe wa pembeni, Oscar Joshua (Yanga) na Erasto Nyoni (Azam FC), sawa! Lakini hakuangalia kuwa kuna mabeki makinda ambao wanafanya vizuri zaidi.

Mabeki wawili wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Kessy na David Luhende (Mtibwa Sugar) angalau wawili kati yao.
Kuna viungo wangapi wangecheza badala ya mkongwe Amri Kiemba ambaye anaweza kutangaza kustaafu hivi karibuni?

Kwa washambuliaji, kumchukua John Bocco wakati akijua kuna wengine wanaofanya vizuri kama Rashid Mandawa (Kagera Sugar) au Samuel Kamuntu (JKT)? Wakati anamchagua, Bocco alikuwa na mabao moja, sasa ana mawili! Kamuntu ana saba na Mandawa nane.

Lakini vipi Ibrahim Ajib, Abdi Banda, Jonas Mkude na Said Juma ‘Makapu’ ambao wameonyesha kuwa na uwezo kweli?

Asingeweza kuwaita wote hao niliowataja, lakini angalau nusu yao na kocha mwenye hesabu na kikosi chake basi huangalia kutumia vijana hasa katika kipindi ambacho hakina mashindano.

Kwa alichofanya Nooij anaonyesha wazi hana mipango ya muda mrefu na Stars. Ndiyo maana anachoangalia ni rekodi zake, hataki kufungwa na anahitaji wachezaji wakongwe wampe matokeo.

Anataka rekodi zake ziwe safi zaidi hata baada ya kuondoka Stars, apate timu kwingine. Haangalii Tanzania itaathiika vipi kwa kuwa wachezaji wake wanazidi kuzeeka na hakuna waliopata nafasi ya kuwaridhi.

Kiemba atakayestaafu baada ya miaka michache, si bora angeitwa Ajibu ambaye ataendelea kucheza kwa miaka mingine nane au zaidi? Nani anaweza kusema Mholanzi huyo hajui hilo.

Anaamua kuwaita hadi makipa wanaokaa benchi na kuacha wanaodaka. Najiuliza anapoonekana kwenye Uwanja wa Taifa au Chamazi Complex amekuwa akienda kufanya nini hasa kama anakuwa na kikosi chake kichwani.

Bado siamini Zanzibar hawana wachezaji mahiri au bora wanaoweza kupata nafasi katika kikosi cha Stars. Tuliona michuano ya Mapinduzi ilivyokuwa migumu na wachezaji kadhaa walizisumbua timu za Bara. Wako wapi waliofanya vema Mapinduzi?

Kipindi chote hiki kazi kubwa ya kocha huyo huwa ni nini hasa? Kuchukua tu mshahara TFF? Maana kikosi chake anacho kichwani, sasa nini hasa anachofanya na kuisaidia nchi yetu?

Najua kwa uoga wenu wengi, mtaona kocha kaonewa. Lakini lazima kuwekwe utaratibu wa kuwabana makocha wanaofanya mambo kwa kuripua huku wakichota fedha za Watanzania.

Lazima wapewe changamoto na wajue wanafanya kazi na watu wanaoelewa mambo. Hivyo si wafanye wanachotaka kwa kuwa wanajua wanatoka Ulaya. 

Tanzania ni zaidi ya Ulaya, tunakosa vichache, si wakija hapa, wazidi kutokosesha badala ya kutusaidia. Akiendelea hivyo, basi kamwe sitakaa kimya, Tanzania si sehemu ya piknik.




1 COMMENTS:

  1. Tatizo ni TFF, wakati wanamchukua waliangalia CV yake na kuielewa!! Kuna makocha ni wa matokeo kama ilivyo kwa Mou, Benetez nk lakini wapo makocha wa kuendeleza vipaji kama Arsene w., Ancellot nk. Lakinibpia kocha kabla ya kumpa mkataba unatakiwa umpe malengo yako na yeye akupe program ya ku-achieve hayo malengo ndo muingie mkataba!! Kama haukufanya hivyo unamu-assess vipi mwalim maana hakuna TOR

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic