Na Saleh Ally
KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Simon Happygod
Msuva amefikisha mabao 11 huku Yanga ikiwa kileleni kwa pointi 40 baada ya
kucheza mechi 19.
Kasi ya Msuva imekuwa gumzo kwa kuwa
ameonyesha uwezo mkubwa katika mambo mengi. Ingawa kitaalamu unaweza kusema si
mzuri sana katika umaliziaji.
Kila anavyocheza, anavyoaminiwa ana nafasi
ya kubadilika na kufanya vizuri zaidi ya hapo maana ndiyo ana miaka 22 tu.
Miaka 22 ya Msuva tayari ameanza kuchukuana
na wachezaji mahiri kama Didier Kavumbagu, Emmanuel Okwi katika ufungaji. Hii
ni sehemu ya kuonyesha ubora sahihi alionao na unaweza kuongezeka kama
ataendeleza juhudi.
Hakuna anayeweza kusema Msuva amefikia hapo
kwa kuwa ana bahati. Kila mmoja anajua alianzia katika muziki, alicheza shoo
lakini mwisho mambo yamekwenda vizuri katika soka. Je, Msuva anataka kumalizia
soka lake Tanzania?
Jibu ni hapana, mara kadhaa ameweka wazi ndoto
zake za kutaka kucheza nje ya Tanzania. Anataka kwenda lini? Au kama haondoki
sasa anasubiri nini?
Mara kadhaa, wachezaji wengi wamekuwa
wakikosea wakikosea wakati wa kwenda kucheza nje ya Tanzania. Wanaendelea
kubaki, huku wakitamani sifa na ufalme wanaopewa kwa wakati husika uendelee.
Samatta&Ulimwengu:
Wako wengi walifeli na kutaka kuondoka
nchini kwenda Ulaya wakati umri ukiwa unaingia ‘jioni’, unawajua. Lakini wako
walioshituka na kuwahi na mfano unao.
Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu sasa
wanacheza TP MAzembe ya DR Congo, moja ya timu bora barani Afrika na
inayojulikana karibu duniani kote.
Samatta na Ulimwengu ni tegemeo la Mazembe
na imekuwa hivyo kutokana na vipaji na juhudi zao lakini ‘target’ sahihi,
wameondoka nyumbani mapema, umri ukiwa unawaruhusu.
Msuva anasubiri lini? Anasubiri kesho? Kama
ni kwenda nje ya Tanzania, hakika ana uwezo ambao utawashawishi.
Kama ni kwenda Ulaya, basi Msuva hapaswi
kuwa na hofu hata kidogo kwa kuwa tayari ameaminiwa na lundo la Wazungu tena
kutoka nchi tofauti.
Mzungu aliyeanza kuonyesha imani kubwa kwake
ni Kim Poulsen akiwa na timu za vijana. Wako hawakuamini Msuva angeweza, yeye
aliamini tofauti na hilo likawezekana.
Baada ya hapo ikawa ni nafasi pia kwa Mzungu
mwingine kutoka Uholanzi, Ernie Brandts kumuamini. Aliendelea kufanya hivyo
hata kama wengine hawakuona anafaa sana.
Kocha kutoka Brazil, Marcio Maximo yeye
hakumpa nafasi kubwa sana. Hata hivyo mara kadhaa alioenekana angalau kumuamini
kidogo na akaendelea kuonyesha anastahili kuaminiwa.
Ujio wa Hans van der Pluijm raia wa Uholanzi
ambaye alishamwamini Msuva awali, umezidi kuthibitisha kwamba kweli ana uwezo
ingawa anatakiwa kujifunza zaidi.
Wazungu kutoka Uholanzi na Denmark
wameonyesha wanamwamini Msuva. Vipi wa Hispania, Ureno au kwingineko watashindwa
kumwamini?
Utaona tofauti kubwa kipindi hiki namna
anavyokokota mpira, anavyokimbia nao hata kutoa pasi, kuna tofauti kubwa na
ulivyomuona miezi sita iliyopita.
Meneja:
Huu ndiyo wakati wa meneja au wakala wa
Msuva kufanya kazi ya kuhakikisha anapata timu nje ya Tanzania.
Akisubiri akafikisha miaka 28 au 29 ndiyo
aanze kutafuta atakuwa amechelewa. Msuva mwenyewe akiona ni raha sasa kupambwa
au kuonekana mfalme hapa nyumbani, pia atachelewa.
Hakuna Yanga wanaopaswa kulaumu kuondoka kwa
Msuva. Simba walikubali Samatta ameondoka, leo kuna nyota kibao wanaendelea
kuibuka, huo mfumo wa maisha ya soka.
Unazaliwa hapa, unakulia huku halafu
unafanikiwa kule. Vitu vinapishana na Msuva ana ndoto zake. Wampe nafasi
azifikie ndoto zake, pia aipe Yanga cha kujivunia na kujitangaza zaidi duniani.
Hakuna haja ya kusubiri kesho ambayo haiwezi kuwa kama anavyofanya leo.
0 COMMENTS:
Post a Comment