Na Saleh Ally
YANGA wamefanikiwa kutoka
sare ya bao 1-1 dhidi ya wageni wao Etoile du Sahel katika mechi ya kwanza ya
Kombe la Shirikisho hatua ya 16 bora.
Timu zote mbili
zinapambana kuvuka hatua hiyo ya raundi ya pili ili kuingia hatua ya mtoano
ambayo anayevuka anaingia katika hatua ya makundi.
Yanga imefanikiwa kufika
hapo baada ya kuing’oa FC Platinum ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 6-3 huku
Etoile ikiwa imeitoa Benfica ya Angola kwa mabao 2-1.
Sare ya bao 1-1 katika
mechi ya kwanza inaiweka Yanga hatarini, kwamba inakuwa na mchezo mgumu katika
kuwania kupata nafasi hiyo. Kuna mambo mengi ya kujiuliza kabla ya kupiga
hesabu nyingine.
Lakini kabla ya kuanza
kupiga hesabu nyingine kwamba Yanga itafanya nini kule Sousse, Tunisia wiki
mbili zijazo. Kwanza ni lazima kukubali kwamba timu hiyo ya Tunisia ina kiwango
bora zaidi ya Yanga na kuitoa lazima kazi ya ziada ifanyike.
Yanga ilikuwa inacheza
nyumbani, lakini ilizidiwa na mipango yake ilikataa. Ilionekana kama vile Yanga
ndiyo ilikuwa ugenini na Waarabu hao walikuwa wakicheza nyumbani.
Huenda mchezo huo ndiyo
ulikuwa mbaya zaidi kwa Yanga katika mechi zake zote za kimataifa msimu huu kwa
kuwa haikucheza vizuri na ukijumlisha na ubora zaidi wa Etoile, Yanga
ikaonekana haina kitu.
Mashabiki waliokuwa
katika majukwaa ya Uwanja wa Taifa jijini Dar waliingia uwanjani wakiwa
wanajiamini na matumaini yao makubwa. Lakini walitoka uwanjani hao wakiwa
tofauti kwa muonekano wa nyuso zao na nusu yao wakiwa wamekata tamaa kabisa
kwamba, Yanga sasa basi.
Etoile ni timu ya daraja
la juu, Yanga si daraja la Etoile lakini ni timu inayopambana kuhakikisha
inamuangusha Goliath, jambo ambalo linawezekana tofauti na wengi
walivyofikiria.
Upepo:
Si mara ya kwanza timu za
Tanzania kuwahi kuing’oa katika mashindano timu kutoka katika nchi za Waarabu
kama Algeria, Misri na kwingineko. Ugumu umeongezeka kwa Yanga kwa kuwa
imebadili upepo kutoka Kusini kwenda Kaskazini.
Katika bara la Afrika
tunajua timu zenye mafanikio makubwa katika michuano ya Caf ni zile kutoka
Afrika Kaskazini, Magharibi na kidogo Afrika ya Kati lakini si Mashariki wala
Kusini.
Mechi mbili za mwanzo
katika Kombe la Shirikisho, Yanga ilikutana na timu kutoka Kusini mwa Afrika
ambazo ni BDF ya Botswana na FC Platinum ya Zimbabwe. Etoile imekuwa timu ya
kwanza kutoka Kaskazini na tofauti imeonekana, kwamba Yanga inakutana na watu
wanaojua mpira.
Inawezekana:
Kuamini Yanga
imeishatolewa kutokana na kiwango walichokionyesha ni jambo bay asana kwa
binadamu anayeishi karne hii. Mtu wa namna hiyo, muoga wa hivyo hastahili
kuishi.
Nini maana ya kupambana?
Ndiyo maana suala la kwanza lilikuwa ni kukubali kwamba jamaa wanajua mpira
kuliko Yanga kutokana na uzoefu wa michuano hiyo. Umakini wa mpangilio wa klabu
yao, utajiri wao na mpangilio bora kabisa wa uendeshaji wa klabu.
Utajiuliza hivi, kweli
walionyesha ni bora kuliko Yanga. Lakini walifunga mabao mangapi katika mechi
hiyo? Jibu ni bao moja tu ambalo kama ni jibu la matokeo, halitawatofautisha na
Yanga kiubora!
Unaweza kusema walikuwa
wanataka sare, sawa. Nafasi nyingi walizopata na kupoteza vipi kwa ubora wao
walishindwa kuzitumia? Hiyo ndiyo sehemu ya maajabu ya soka, mwisho matokeo ni
1-1.
Yanga inashindwa kupata
2-2 ikiwa uganini Tunisia? Haiwezi kupambana ikashindwa? Yote yanawezekana kwa
kuwa Kocha Hans van der Pluijm sasa atakuwa akiwafundisha wachezaji wake kwa
taswira sahihi na si picha za video kama walivyofanya awali.
Wanajua ubora wa Etoile
ni kiasi gani? Yanga wanajua ni wapi walikosea na huenda ikawa lahisi zaidi
kujua nini cha kufanya.
Huenda kuwa na wachezaji
wengi majeruhi iliwaathiri katika mechi ya juzi. Kwa kuwa Hassan Dilunga
aliwafanya Yanga kucheza pungufu ya mtu mmoja kwa kipindi chote cha kwanza.
Alishindwa kukaba wala kuchezesha timu.
Pluijm akawa muoga
kufanya mabadiliko kwa kuwa tayari ilionekana Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye
ni stopper wake alikuwa anachechemea na mwisho akalazimika kumtoa.
Wachezaji karibu wote wa
Yanga walionekana kuwa waoga licha ya kuwa wako nyumbani. Walikimbia hata
kuuchukua mpira na ilionekana ni kama mechi fulani walioyokuwa wakikwepa
lawama.
Etoile kuona YAnga ni
waoga licha ya kuwa wako nyumbani. Wao ndiyo wakaanza kucheza mpira na
kuwatawala wanavyotaka. Huenda presha hiyo pia angalau kwa asilimia 20 itahamia
kwa Etoile wakiwa nyumbani na Yanga wakiitumia vizuri baada ya kujipanga
vizuri, inawezekana.
Kikubwa kwa Yanga ni
mambo matatu, kwanza kukubali jamaa wanajua, pili wajipange na kuangalia
wlaipokosea, hii ni kwa makocha na wachezaji wote na tatu, waamini hakuna
kinachoshindikana na mifano iko mingi.
0 COMMENTS:
Post a Comment