KILA mmoja wetu anaweza kuwa na mawazo yake
tofauti na unavyofikiria wewe au mimi. Hii ndiyo sahihi kwangu. Leo nataka
kukuuliza jambo ambalo limekuwa likinishangaza sana na ninakosa majibu.
Nakuuliza swali kuhusiana na Dk Damas Daniel
Ndumbaro. Kitaaluma huyu ni mwanasheria, tena ni daktari wa sheria, unaweza
kumuita gwiji.
Dk Ndumbaro ni mwalimuwa sheria katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam pia Chuo Kikuu Huria (Out). Daktari huyo wa sheria pia
amewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro.
Dk Ndumbaro amewahi kuwa wakala wa kuuza
wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ni kati ya
wadau ambao wameshiriki mambo kadhaa ambayo yanahusiana na mchezo huo.
Nakumbuka mwaka juzi nilikutana naye makao
makuu ya Fifa jijini Zurich, Uswiss wakati nikiwa nimepata mwalimu wa
kutembelea na kujifunza mambo kadhaa kuhusiana na shirikisho hilo.
Ghafla nilimuona Dk Ndumbaro akitoka katika
moja ya ghorofa za jengo hilo akiwa ameongozana na marefa kutoka nchini Sweden,
tukaanza kufanya mazungumzo. Kwangu niliona faraja kumuona Mtanzania mwenzangu
akiwa katika eneo hilo.
Binafsi nimekuwa na mtazamo tofauti
kuhusiana na Dk Ndumbaro, ninaamini ni kati ya Watanzania wanaotakiwa na
Watanzania kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa soka kwa kuwa ili tubadilike,
tunahitaji watu imara, wenye upeo wa kuleta maendeleo na si kutaka kufaidishwa
na mpira au kuchota tu fedha.
Bila ya kupindisha maneno, ninaamini Dk
Ndumbaro ana uwezo mkubwa wa kuchangia na wadau wengine kuusaidia mpira wetu
kupiga hatua kama tutaachana na ushabiki au akili za uoga.
Naanza na ninaendelea kushangazwa na kesi
kati ya Dk Ndumbaro na TFF namna ambavyo imekuwa ikiendelea. Hivi karibuni
alifungiwa miaka saba, eti kisa alizitetea klabu zisikatwe fedha zao!
Kwangu niliona ajabu sana, nilipiga kelele
sana kwa kuwa haikuwa haki. Klabu zilionyesha unafiki kwa kukaa kimya na
kumuacha, akahukumiwa kwa kuonewa kila mmoja aliona.
Akakata rufaa, tuliona alilazimika kutoa Sh
milioni moja ili rufaa yake isikilizwe. Kwangu niliona angekuwa hajafungiwa,
fedha hiyo ingeweza kusaidia mchezo wa soka katika kuendelea hata kama ni robo
hatua. Au ingeshindikana angenunua mboga akala na wanaye nyumbani. Lakini
aliitoa kwa kuwa ana mapenzi mchezo wa soka.
Kupokea rufaa ilikuwa lahisi, lakini TFF
kuthibitisha kama imepokea rufaa ikawa kizumbumkuti, ikajaribu kupiga chenga
hapa na pale, ili mradi tu.
Siku chache zilizopita kimefanyika kituko
kingine. Kamati ya rufaa ya TFF ilijaribu kusikiliza kesi ya Dk Ndumbaro bila
ya kumuita, kilikuwa ni kitu cha ajabu sana kuingia masikioni na kueleweka
kwenye ubongo wa yoyote hata kama angekuwa juha. Mwisho, ikashindikana.
Usisahau, hata wakati anahukumiwa na
kufungiwa miaka saba, alikuwa nje ya nchi akiwa amealikwa kufundisha katika
chuo kikuu kimoja cha Marekani.
Alidhulumiwa, hakupewa haki ya kujitetea. Sasa
alitaka kudhulumiwa hata haki yake ya kujitetea katika rufaa.
Leo nasikia TFF imemuongezea kesi, kwamba
aliandaa mechi wakati akiwa kiongozi wa Simba. Jambo liko wazi, kipindi hicho
alikuwa wakala na hakuwa kiongozi wa Simba maana alijiuzulu uenyekiti wa kamati
ya uchaguzi ya Simba kabla ya kuchaguliwa tena.
TFF ya Leodeger Tenga ilikuwa inajua ndiyo
maana ikamruhusu kuandaa, ikamkopa fedha zake. Ikalipa kiasi nab ado anaidai.
TFF ya Malinzi hiyo ni kesi, mimi najua TFF ni moja. Sasa hii inaona sawa, hii
si sawa! Ajabu kabisa!
Kwa nini TFF ya Malinzi inamuogopa Dk
Ndumbaro, au ndiyo ile hadithi kwamba anataka kuchukua nafasi ya Malinzi?
Sasa itafanya hivi hadi lini? Mimi
nilifikiri watu imara ndiyo wajumuishwe na kushirikishwa katika soka kusaidia
maendeleo? Sasa aliye na uwezo anaogopwa, mwisho wa hili ni nini? walio imara
au bora hawastahili kwenye soka, tunataka waoga na wasio na uwezo ili
uwaendeshe na maisha ya soka yaendelee kuwa ya kubahatisha.
Mimi nimechoshwa na
hadithi ya Dk Ndumbaro kuhofiwa utafikiri Simba mla watu wakati inajulikana
ubora wa kazi yake na anaweza kuwa msaada katika maendeleo ya soka nchini. TFF
mlitafakari hili.
Huyo ni daktari wa kitabuni sio vitendo ndio maana hata wambura alihofia huo udk wake!
ReplyDelete