February 6, 2016

MASHABIKI SIMBA
Na Saleh Ally
LIGI Kuu Bara inaendelea, kutokana na Simba kushinda mfululizo, sasa msisimko uko juu sana.

Mashabiki wa Simba, wamerejea baada ya kupata matumaini upya. Lakini gumzo jingine ni Yanga kufungwa mara moja na sare moja. Huku wengine wakiwa wanazungumza kuhusiana na viporo vya Azam FC ambao walikwenda kushiriki michuano nchini Zambia, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi, wakawaachia waende.

 Watanzania wanavutiwa na ligi, lakini timu zinazocheza hazifaidiki hata kidogo na hakuna anayeweza kukataa tena kwamba timu zote zinajiendesha kwa hasara ambalo ni jambo la kiuwendawazimu kabisa.

Ninaliita ni la kiuwendawazimu kwa kuwa kujiendesha bila faida, haiwezi kuwa biashara. Timu zote zinategemea fedha za mchango, msaada au ruzuku kutoka serikalini kwa timu za majeshi.

Timu ipi inajiendesha kwa fedha kutoka katika mfuko unaotokana na kipato pekee cha Ligi Kuu Bara? Jibu ni hakuna na hapo ndiyo unaweza kujiuliza, kama ni kwa maana ya biashara, ligi ya nini sasa?

Kwangu jibu rahisi naona ni timu kwenda kucheza kwa ajili ya kufurahisha mashabiki. Hakuna hata timu moja ya Ligi Kuu Bara inayofanya biashara sahihi, kwa kuwa timu zote zinajiendesha kwa hasara.

Timu zilikuwa zinategemea zaidi mapato yanayotokana na viingilio. Tena timu zilizokuwa zinaweza kutengeneza mapato ya juu ni Yanga na Simba kutokana na ukongwe wao katika historia ya soka hapa nchini.

Sasa mambo ni tofauti kabisa, baada ya mechi kuanza kuonekana kwenye runinga ya Azam TV, watu wengi hawaendi uwanjani na mapato ya hadi mechi 10, yanaweza kulingana na mapato ya mechi moja tu.

Yanga, inalipa mishahara hadi ya Sh milioni 114 kwa mwezi. Lakini inaingiza kipato cha Sh milioni 54 hadi 64 kwa mwaka. Hii ni biashara au kufurahishana?

MASHABIKI YANGA

TFF wanalifanyia kazi hili? Jibu hapana kwa kuwa muda mwingi wanaingia kwenye malumbano na mambo mengi lukuki yasiyokuwa na maana.

Yanga au Simba wanaliona hili? Jibu hapana kwa kuwa wanasubiri kulumbana na wengine wako pembeni kuzozana kwa ajili ya kocha, kwa ajili ya viongozi au kulialia bila sababu lakini wakiangalia maslahi yao.

Nataka kidogo tujifunze, wakati Bongo tukiwa tumekalia majungu na migogoro, Ligi Kuu England ambayo tunaifurahia, watu wanafanya kazi kweli na pamoja na burudani yao kuwa bora, wanatengeneza fedha kwelikweli.

Nitakueleza sababu tano za Ligi Kuu England kwa nini ni burudani na biashara kubwa kweli. Watu wanaburudika huku wakiwa kazini wanaingiza mamilioni ya fedha.
Tanzania ingeweza kuingiza, si kama za England lakini timu zingejiendesha kwa faida na si hasara milele.

MASHABIKI AZAM FC

 1. Fedha tupu
Msimu wa Ligi Kuu England 2014-15 mabingwa Chelsea waliibuka na kitita cha pauni milioni 99 (zaidi ya Sh bilioni 306) huku walioshika mkia QPR wakipata pauni milioni 64.8 (zaidi ya Sh bilioni 200). Pauni bilioni 1.6 (karibu Sh trilioni 5) ziligawanywa kwa klabu kama zawadi mbalimbali.
Hizi zilikuwa ni fedha zinazotokana na viingilio pamoja na malipo ya haki za runinga kutokana na kila timu mechi zake ngapi zilionyeshwa.

2. Faida mkiani
Hata timu zilizokuwa mkiani, ziliingiza mamilioni. QPR ilicheza mechi 38 za ligi, ikaibuka na pointi 30 tu lakini mwisho mfukoni ikawa na pauni milioni 64.86.
Hii maana yake, katika kila pointi waliyoshinda walipata pauni milioni 2.16 au kila dakika klabu iliibuka na pauni 18,972.

3. Nguvu ya fedha
Arsenal ilipata zawadi ya pauni milioni 3.4 (Sh bilioni 10.5) kwa kushinda Kombe la FA, pauni milioni 1.8 (Sh bilioni 5.56) zilipatikana kwenye fainali na zilizobaki katika raundi za awali. Lakini fedha hizo za ubingwa wa FA, zilikuwa ndogo hata kuliko zile walizopata Newcastle ambao walimaliza katika nafasi ya 15 kwenye ligi. Hii inaonyesha nguvu ya fedha ya ligi hiyo.

4. Heshima ya vigogo
Katika msimu wa 2014-15, Manchester United ilimaliza ligi katika nafasi ya saba. Lakini ndiyo iliyochukua fedha nyingi zaidi za haki za runinga kwa kuwa mechi zake nyingi zaidi zilionyeshwa.
Katika mechi zake za ligi, 27 zilionyeshwa live, hivyo kuifanya ikusanye fedha nyingi zaidi kuliko timu yoyote ya Premier League wakiwemo mabingwa Chelsea. Hii inaonyesha kweli ligi hiyo ni biashara kwanza na si ukubwa wa msimamo wa ligi. Hii ni akili “kubwa”.


5. Mashabiki mtaji
Msimu wa 2012/13 uliokuwa wa mwisho kwa Kocha Sir. Alex Ferguson, Man United waliambulia pauni milioni 60.8 (Sh bilioni 188) lakini fedha zinazidi kuongezeka kwa kasi katika ligi hiyo, kwani fedha hiyo sasa ni ndogo hata kwa ile waliyopata QPR ambao walikuwa wa mwisho msimu uliopita.


Fedha inapanda kwa kasi kubwa, lakini hii inaonyesha namna gani kuna wataalamu wanatengeneza mazingira bora ya biashara katika ligi hiyo tofauti na kwetu Bongo, wataalamu wanakuwa wapambe wa mabosi wa klabu na mashirikisho au wanabaki kuwa watu wa kupiga majungu kufurahisha nafsi zao kwa kuwa wamegubikwa na ushabiki au si wanaojiamini. Sijui hapa kwenu hata robo ya hiyo kwa watu tulionao, tutafikia lini?

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic