September 23, 2016



Huku zikiwa bado siku chache miamba ya soka hapa nchini, timu za Simba na Yanga zikutane uwanjani katika Ligi Kuu Bara, Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali amewasifia wapinzani wake hao kuwa wapo vizuri.

Akizungumza na juu ya mchezo huo wa Oktoba Mosi, mwaka huu, Akilimali alisema msimu huu Simba ina kikosi kizuri, imejitahidi kusajili wachezaji wazuri tofauti na msimu uliopita na kudai wakiwa makini wanaweza kutoa ushindani kwa Yanga lakini bado anaamini Yanga itaibuka na ushindi katika mchezo huo wa wiki ijayo.

“Kuna mambo ambayo nimezushiwa hivi karibuni kuwa eti nilikutana na viongozi wa Simba kujadili mchezo wa Oktoba Mosi, hao waliosema hivyo wana lao jambo.

“Ukweli ni kwamba, sijafanya kikao na kiongozi yeyote wa Simba na siku hiyo inayosemwa mimi nilikuwa Bagamoyo nikiuguza maumivu ya jino ambalo lilikuwa likisumbua lakini tayari nimeshaling’oa na sasa nipo kwangu hapa Dar, waniache, wasitake kunipaka matope kwa sababu tu ya msimamo nilionao juu ya Yanga kukodishwa.

“Kuhusiana na mechi yetu na Simba itakuwa na ushindani mkubwa msimu huu kutokana na usajili mzuri ambao Simba wamejitahidi kufanya, nawatabiria kuwa safari hii watapiga hatua kidogo kutoka nafasi ambayo msimu uliopita waliishika lakini pia watatoa upinzani kidogo katika mchezo wetu kama viongozi wao watajipanga.

“Lakini suala la kupata ushindi katika mchezo huo hilo wasahau kabisa kwani tutawafunga, hapo awali baada ya Simba kutufunga mabao 5-0 niliwahi kusema kuwa tutalipa kisasi kwa kuwafunga mabao mawili kila tutakapokutana nao ambapo mpaka sasa tumeshawafunga manne, hivyo siku hiyo pia tutawafunga mawili na kuwaacha na deni la bao moja,” alisema Akilimali.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic