Na Saleh Ally
UNAMUONA Francis Cheka
akiwa ulingoni akipambana, anarusha makonde kadhaa kwa ajili ya kusaka ushindi.
Pamoja na kupingwa ngumi kadhaa, wakati mwingine hata kuangushwa lakini
anainuka na kuendelea.
Mwisho huibuka na
ushindi, awali ushindi wake ulikuwa ukishangiliwa na watu wengi sana, hasa wale
walioonekana ‘kuchoshwa’ na ushindi mfululizo wa familia ya akina Matumla ambao
walikuwa wakiongoza kutokana na kuwa na vipaji vingi vya mchezo huo katika
familia yao.
Huenda wengi waliamini Cheka
anaweza kuwa ‘nguvu ya soda’ hasa baada ya kuwashinda wababe wakati huo kama
Rashind Matumla na baadaye Maneno Oswald au Mtambo wa Gongo. Lakini akaendelea
hivyo kwa kutoa kipigo kikali kwa Hassan Matumla ambaye lilikuwa tegemeo la
mwisho la kummaliza bondia huyo wa Morogoro.
Wakati Cheka akizipiga na
Japhaet Kaseba, wengi waliamini ulikuwa ni mwisho wake. Lakini wapi,
alichokifanya ilikuwa ni zaidi ya ‘sterlling’ anayetaka kulipa kisasi zaidi ya
‘jambazi’.
Alimpiga alivyotaka na
kushinda hadi mmoja wa mashabiki anayejulikana alipopanda jukwaani na kuvuruga
pambano. Lile la marudiano, halikufanyika.
Kama ambavyo wengi
walichoshwa na ushindi wa akina Matumla, huenda sasa wamechoshwa na ule wa
Cheka. Tena inaonekana ‘raia’ wa Dar es Salaam ndiyo hawataki kumuona tena
Cheka akishinda.
Awali ilikuwa ni watu wa
Keko ambao walikuwa na upinzani mkubwa na wale wa Kinondoni ambao wao
walimuunga mkono Cheka. Lakini baada ya kumchapa Kaseba, akawa adui wa
Kinondoni.
Sehemu nyingine maarufu
kwa mchezo wa ngumi ni Manzese jijini Dar es Salaam. Usiku wa kuamkia jana,
Cheka amevunja kambi hiyo, amempiga Thomas Mashali kwa knockout (KO) katika
raundi ya 10 na kumaliza kabisa ndoto za mabondia wa kumshinda.
Wakati akipigana na Mashali,
ilionekana wazi Cheka sasa ni adui wa Dar es Salaam, hana ugomvi lakini ujuzi
wake unasababisha asiwe na mpinzani unamfanya aonekane adui.
Lakini ukweli Cheka ni
shujaa wa taifa, ndiye bondia wa kulipwa anayeliwakilisha vilivyo taifa letu,
waulize mabondia wote kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika waliopigana naye,
wana taarifa zake.
Amekuwa akifeli kwa
mabondia wa Ulaya, inawezekana maandalizi ya michezo ya kimataifa ikawa tatizo
kwake, lakini kocha wake, Abdallah Saleh ‘Komando’ ambaye ni mwanajeshi mstaafu
anajitahidi vilivyo kumsaidia kijana wake kuendelea kuwa imara.
Bado Cheka anahitaji
sapoti, si kutoka Morogoro pekee anakotokea, badala yake ni nchi nzima kwa kuwa
ndiye mwakilishi anayeing’arisha Tanzania katika mchezo huo baada ya kuzeeka na
kupoteza umaarufu kwa Rashid Matumla ambaye pia anastahili kupewa heshima
kubwa.
Kwa mabondia wanaochapwa
na Cheka kila kukicha, si sahihi kuvizia ‘uzee’ wake wapate nafasi ya kulipa
kisasa, lakini lazima wajifunze kwa kuwa Cheka si malaika na si sahihi kuamini
ushirikina unamsaidia kuwa bora.
Nani hufanya mazoezi kama
yeye, maandalizi yake ni zaidi ya pambano. Mabondia wengine hawafanyi hivyo na
wanalijua hilo, lakini wanataka kushinda kwa ndoto.
Kushinda bila ya
maandalizi ya kutosha hasa kujituma kwa kocha na bondia mwenyewe si rahisi.
lazima kuwe na uungwana wa kukubali anachokifanya Cheka na wanaotaka mafanikio
wanaweza kujifunza kwake.
Kumchukia kwa kuwa anatokea
Morogoro na wewe ni wa Dar es Salaam ni sawa na kuisaliti Tanzania. Washauri
mabondia unaowashabikia wajifunze kutoka kwake, alichofanya yeye si ndoto za
mchana, amejituma kufikia alipo pamoja na kwamba aliishi maisha ya shida ya
kuishi kwa kuokota na kuuza chupa mitaani.
Cheka ameleta mapinduzi
ambayo wengi mmekuwa wavivu kufungua kurasa za kitabu chake kusoma kilichomo.
Mnaona ‘kava’ lenye picha linatosha kuwaeleza kila kilichopo, kosa kubwa. Cheka
ni shujaa wa taifa letu.
0 COMMENTS:
Post a Comment