Na Saleh Ally
SIMBA ndiyo klabu inaonekana kutokuwa na
ntimanyingo na mara nyingi imekuwa inawaruhusu wachezaji wake kwenda kufanya
majaribio ya kucheza soka la kulipwa.
Ukiachana na hivyo, Simba ndiyo
inayoongoza kuuza wachezaji wengi nje ya Tanzania na wengi wamekuwa
wakifanikiwa.
Wako waliofeli kwa matatizo yao binafsi,
hata rekodi ya kuuza wachezaji wengi nje bado inashikiliwa na Simba. Ukiangalia
imewahi kuruhusu au kuuza wachezaji wake Norway, Sweden, DR Congo na kwingineko.
Simba haikuanza leo kuuza wachezaji nje
ya Tanzania, tokea enzi za miaka ya 1990, wachezaji wake wengi walicheza Afrika
Kusini na kwingineko. Mfano ni Yusuf Macho, pia Selemani Matola ambaye
alikipiga na SuperSport United.
Lakini miaka ya hivi karibuni, Haruna
Moshi ‘Boban’ aliuzwa katika timu ya Gefle IF inayoshiriki Ligi Daraja la
Kwanza nchini Sweden sawa na Henry Joseph ambaye alikwenda Kongsvinger IF ya
Norway. Ingawa uhamisho wake ulikuwa na utata na inaelezwa ‘alijinunua’ lakini
mwisho ni hivi, alitokea Simba.
Mbwana Samatta anaendelea kufanya vizuri
akiwa na TP Mazembe ya DR Congo, moja ya
timu kubwa nab ado anaonyesha uwezo wa juu. Achana na hivyo, Mganda Emmanuel
Okwi pia ametokea Simba na kujiunga na Etoile Du Sahel ya Tunisia ingawa biashara
yenyewe ni kichaa.
Inawezekana Simba haijapata faida kubwa
kwa wachezaji hao, lakini sasa inabidi ijipange na idumishe kitengo chake cha
wachezaji wanaotoka nje.
Simba inauza wachezaji kwa ajili ya
faida na si kuwauza ili isifiwe kuwa inauza wachezaji na baadaye viongozi
watumie kilichotokea kama sehemu ya kujifanyia kampeni katika mambo mengine.
Hizo ni hesabu mbovu kwa Simba.
Makosa mawili ya haraka ndani ya miezi
sita yanaonyesha kuna tatizo ndani yake, ukianza na lile la Okwi, pili ni
kushindwa kumuuza kiungo wake nyota, Amri Kiemba maarufu kama Baba Shabani.
Kiemba:
Hili limekuwa kosa la pili ndani ya muda
huo mfupi ikiwa ni baada ya kuvurunda kwa Okwi na hii inaifanya Simba iendelee
kubaki na sifa tu ya kuuza wachezaji wengi Ulaya na nje ya Tanzania lakini
faida ni kidogo sana.
Klabu ya Raja Casablanca ya Morocco ilionyesha
nia ya kumtaka Kiemba na Simba ikakubali lakini ikasisitiza inataka angala dola
300,000 (Sh milioni 486), ili imuachie akacheze soka Afrika ya Kaskazini.
Fedha ilizodai Simba kwa Kiemba
zilionekana kuwa ni nyingi mno kwake, lakini Simba ikasisitiza kuwa ni lazima
iwe hivyo na si zaidi na kama Raja watakuwa hawana, basi hakuna biashara.
Kulikuwa na hali ya haraka, wanaohusika
na kuuza wachezaji kwa Simba walishindwa kutofautisha kati ya Okwi na Kiemba.
Si kwa maana ya kiwango au nafasi wanazocheza, lakini kulijua soko kwa
kuangalia umri wa wachezaji hao.
Timu nyingi ambazo zimepiga hatua
kibiashara zinaangalia mambo mawili makubwa, kwanza msaada wa mchezaji
zinayemnunua na hiyo inaweza kuwa asilimia 30 hadi 35. Zilizobaki ni soko lake,
kwamba akiwa pale zinaweza kumuuza na kupata faida.
Waarabu wa Raja, kwa Kiemba wanajua watapata
faida moja tu na si ziada. Kiungo huyo kuitumikia timu yao angalau kwa misimu
miwili au mitatu na si suala la biashara zaidi, kwani umri wake wa miaka 30
unamfunga kuendelea mbele.
Viongozi wa Simba hawakuwa wepesi
kuangalia umri tena, badala yake fedha tu. Tena wao wangeweza kuona mambo
matatu muhimu na mawili kama faida kubwa kwao.
Kwanza walimsainisha Kiemba kwa Sh
milioni 35, halafu wangepata zaidi ya Sh milioni 200 kama wangemuuza hata kwa
dola 150,000. Faida ya pili ni kwamba wanamuondoa mchezaji ambaye kwa umri wake
hawezi kuendelea kuwa tegemeo kwa misimu miwili ijayo.
Faida ya tatu inakwenda kwa mchezaji na
ingeonyesha kiasi gani Simba nao wanajali, kwamba baada ya Kiemba kuitumikia
kwa kiwango cha juu hasa kwa misimu miwili iliyopita, wanampa nafasi ya
kumaliza soka lake katika sehemu yenye mazingira mazuri zaidi kama mshahara na
fedha nyingi za usajili, hiyo ni kama shukurani.
Hayo hayakufanyika, kwa kuwa walio
katika suala la kuuza wachezaji si wataalamu zaidi na huenda waliyafanya mambo
kwa kuangalia karibu. Lazima wakubali kujifunza na kujenga tabia ya kukubali
kwamba kuna mambo ya kimasoko na utaalamu ambao unaweza kuonyesha uuzaji wa
mchezaji uende namna gani.
Kufuata utaalamu ni bora, lakini kuepuka
ushabiki au kuangalia pekee faida za timu kwamba kiungo huyo ni tegemeo pia ni
tatizo. Fedha ambazo ingezipata Simba ingeweza kusaini kiungo mwingine kinda
ambaye angekuwa msaada kwao baada ya muda mrefu zaidi kutokana na umri wake.
Lakini ingeweza kuzitumia fedha hizo pia
kuwalipa vizuri wachezaji makinda ilionao kwa kuwapa mikataba minono ambayo
ingewasaidia kujituma zaidi na kuwa msaada kwa Simba.
Kutomuuza Kiemba ni kosa kubwa kwa
Simba, huenda baada ya miezi michache ijayo wanaweza kuanza kuelewa. Lakini
Kiemba mwenyewe amekuwa mwepesi hadi amethubutu kusema anajuta kusaini Simba
haraka.
Huenda lilikuwa ni kosa jingine kwake,
kwamba aliona bora azichukue fedha hizo ambazo Simba walizitoa zikalala katika
sehemu ya mapokezi ya hoteli wakitaka alipwe.
Lakini huenda Kiemba hakuwa na kosa
kubwa sana, badala yake viongozi nao walipaswa kupimwa faida ya walichokifanya.
Okwi:
Hili linaweza lisiishie kwa Kiemba kwa
kuwa siku zinasonga na mambo yanazidi kujitokeza, kama itatokea mara nyingine
lazima viongozi wawe wa Simba, Yanga, Azam FC, Mtibwa Sugar au timu nyingine
waangalie suala la umri, faida kwao na pia kwa mchezaji na si kujiangalia wao
au kuingiza siasa.
Ukiachana na hivyo, bado Simba inapaswa
kuangalia suala la faida na si sifa ya kuuza tu wachezaji nje ya Tanzania huku
ikiwa haina kitu.
Biashara ya Okwi ni kichaa, hilo halina
ubishi. Aliyeshiriki ni Mwenyekiti Rage pekee, hapa wanapaswa kushirikishwa
wataalamu ambao watafanya uamuzi sahihi katika wakati mwafaka.
Inavyoonekana Simba huenda isipate hata
senti katika suala la Okwi kwa kuwa tayari Mganda huyo ameanza kuitibua hiyo
timu na yenyewe inaitaka Simba iwasaidie kumuuza, kitu ambacho ni kichekesho.
0 COMMENTS:
Post a Comment