Na Saleh
Ally
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), linajua fedha nyingi linazotoa kwa wanachama wake
barani Afrika zimekuwa zikitumiwa sivyo.
Fifa hutoa
zaidi ya Sh bilioni 15 kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia vyama mbalimbali vya
soka ambavyo ni wanachama wake.
Lengo la
fedha hizo ni maendeleo ya mchezo wa soka na hasa kuanzia kwa vijana, lakini
Fifa inaona wazi kuwa hairidhishwi na matumizi ya fedha inazotoa, badala yake
inataka kasi zaidi ya maendeleo.
Lakini inaonekana
Fifa inashindwa kuwa wazi kwa kuwa kiasi fulani, vyama vya soka katika nchi
mbalimbali vinabaki kuwa ‘hitaji’ muhimu sana kwa Fifa, hivyo lazima
ivinyenyekee.
Uongozi wa
shirikisho hilo chini ya Rais Sepp Blatter unajua bado kuna tatizo kubwa la matumizi
ya fedha kutoka katika kila nchi ambayo inapata msaada wa shirikisho hilo.
Fifa
inavihitaji vyama hivyo hasa kwa ajili ya kuwa na uhakika wa kura wakati wa
uchaguzi mkuu. Ingawa fedha zinatolewa kwa kufuata utaratibu kamili, lakini
inaonekana hakuna nguvu kubwa ya udhibiti na kutaka kujua matumizi yanakwenda
vipi.
Ingawa
vyama hivyo vinabaki kuwa taasisi ya umma kama ilivyo hapa nyumbani kwa TFF,
bado viongozi wake wamekuwa wakifanya matumizi ya fedha hizo bila ya kujali
kuhojiwa na Fifa kwa kuwa inawahitaji, basi imewawekea uzio kwamba wana haki ya
kujitawala.
Utaona hapa
kila upande unakuwa unauhitaji mwingine na kwa kuwa wanaotoa fedha ndiyo wanawalinda
waliopewa, mara nyingi serikali nyingi za nchi za Afrika zimekuwa zikishindwa
kuingilia na kutaka kuhoji matumizi ili kujua kama kila kitu kinakwenda sahihi.
Mkuu wa Kitengo
cha Kupambana na Ubaguzi wa Rangi Ndani ya Fifa, Jeffrey Web, anasema kama
wanavyopambana na ubaguzi, wanafanya kila kitu kuona fedha wanazotoa zinaleta
mabadiliko katika soka Afrika.
“Inawezekana
ni mfumo wa Fifa wa maendeleo na utendaji kazi ndiyo ulivyo. Kwamba tunataka
watu wawe huru na kufanya mambo yao kwa nafasi,” anasema katika mahojiano na
Championi jijini Zurich.
“Tunachofanya
ni kufuata utaratibu na kamwe hakuna anayemhofia mwingine, ndiyo maana utaona
kuna wakati kuna vyama au mashirikisho katika nchi kadhaa, yamekuwa
yakifungiwa. Lakini hata sisi tunaona kuna tatizo kweli.
“Matumizi
ya fedha hayaendani na maendeleo yanayopatikana katika vyama hivyo, nafikiri
hapa si ufujaji pekee, lakini hata ile hali ya watu wanataka nini na wamelenga
kitu kipi.
“Mfano,
angalia wachezaji wengi wa Afrika wanakimbilia kuja kucheza katika timu za
Ulaya. Wanapokuwa huku (Ulaya) wanaweza kufanya vizuri zaidi kwa kuna kila kitu
kama vifaa ukiwemo uwanja, vinapatikana.
“Kufanya
kwao vizuri ni kwa kuwa wanafundishwa na makocha bora, vifaa vya uhakika lakini
wanacheza katika viwanja vizuri vyenye hadhi. Vitu vyote hivi kwa Afrika ni
tatizo kubwa, ndiyo maana tumesimamia katika vijana na viwanja.
“Tunajua
sababu ya Ulaya kuwa na ubora wa juu. Hivyo Afrika wanapaswa kujua viwanja na
vifaa bora ni vitu vya muhimu kuliko kuamini kila mwanasoka akitaka kufanikiwa
lazima aende Ulaya. Bado Afrika ina nguvu ya kujitengeneza na ikiwezekana siku
moja wachezaji kutoka Ulaya wakacheze katika bara hilo.
“Hii
inawezekana na huenda kama Afrika itafikia nusu ya Ulaya kwa maana ya maendeleo
ya vifaa na ubora wa vifaa na walimu. Basi soka litakua haraka zaidi kutokana
na ushindani utakaokuwepo,” anasema.
Maelezo mazuri
ya kiongozi huyo yanaonyesha kiasi gani namna Fifa inavyotambua uwezo wa Afrika
ambayo inaonekana iko chini zaidi licha ya kuwa na vipaji lukuki vinavyotikisa
sehemu mbalimbali duniani kote.
Maana yake
Fifa wanaamini kama Afrika ingejiboresha zaidi kwa upande wa vifaa na
kuwasomesha walimu wake, basi soka lake lingekuwa juu na kutoa upinzani mkubwa
kwa Bara la Ulaya na kwingineko.
Huenda
fedha ni tatizo, lakini Fifa inaona Afrika ina uwezo wa kuwa na viwanja vizuri
kwa kiwango cha kucheza na mazoezi na suala la uwanja mkubwa wa kuingia watu
wengi lifuatie baadaye.
Upungufu unaonekana,
ingawa Fifa wanakataa kama hawawahofii viongozi walio madarakani katika vyama
mbalimbali hata kama watafuja fedha ambazo wanapata kwa ajili ya maendeleo ya
soka.
Lakini hali
halisi inaonyesha ni hivyo kwa kuwa wanategemea katika suala la kura wakati wa
uchaguzi, hivyo nao wanaweza wakawa wanalenga maendeleo au mabadiliko Afrika
lakini wanachotaka zaidi ni kura zao na si maendeleo hasa.
Mradi wa
Goal wa Fifa ni moja ya ile iliyopambana kuhakikisha kunakuwa na viwanja bora,
huu ni kati ya miradi michache ya Fifa iliyopata mafanikio na inaonekana
imefikia hapo kwa kuwa fedha haipitii katika vyama vya viongozi na badala yake
ujenzi unasimamiwa na wao Fifa na kweli mafanikio yameonekana.
Kama Fifa
wangekuwa hawana hofu ya kukosa kura, huenda maendeleo yangekuwa juu zaidi hadi
sasa, lakini hofu ya kumuudhi mpigakura, inaiangamiza Afrika na kuwafaidisha
wachache sana.
SOURCE: METODO
0 COMMENTS:
Post a Comment