Na Saleh Ally
Kuna msemo mgeni siku ya
kwanza mpe maziwa, siku ya pili mpe samli lakini siku tatu mpe jembe akalime.
Hicho ndicho watakachokutana nacho wageni wa ligi Kuu Tanzania Bara.
Inaanza kesho huku mambo
yanayosubiriwa kwa hamu kubwa ni namna ambavyo wageni hao ‘wageni’ na wageni
‘wapya’ watakavyoweza kufanya kazi yao kwa kiwango ambacho kinaaminika kuwa ni
kikubwa zaidi ukilinganisha na wachezaji wa hapa nyumbani.
Ingawa kuna wachezaji
zaidi ya 15 kutoka nje ya Tanzania, lakini 15 ndiyo watakuwa wakisubiriwa kwa
hamu kuonyesha sababu hasa ya timu za Tanzania Bara kuendelea kusajili
wachezaji wa kigeni.
Yanga ina wachezaji wanne
kama ilivyo kwa Simba, Azam FC watano na Coastal Union watatu na kila mmoja
kati yao anajua ushindani mkubwa uliopo katika ligi hiyo hasa wale wanaotokea
katika vikosi vya Azam FC.
Watatu kutoka Coastal,
wawili kati yao Crispian Odula
aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Bandari Mombasa na Yayo Lutimba
kutoka URA ya Uganda watakuwa na kazi ya kuonyesha wanastahili kuwa Tanzania.
Nahodha wao, Jerry Santo
ni Mkenya mwenye uzoefu mkubwa na ligi hiyo ingawa hiyo haimzuii kuendelea
kupambana.
Simba:
Kwa Simba, kipa Abel
Dhaira atakuwa anacheza msimu wa pili lakini bado atakuwa na kazi kubwa ya
kuonyesha kuwa anastahili kuwa namba moja katika kikosi hicho cha Abdallah
Kibadeni.
Kazi hiyo pia inamkuta
beki Kaze Patrick ‘Demunga’ ambaye ametokea Vital’O ya Burundi. Yeye na kipa
huyo lazima wahakikishe Simba inapunguza kuruhusu mabao.
Msimu uliopita, Simba
ilishika nafasi ya tatu, ngome yake ikiwa imeruhusu mabao 25 na kushika nafasi
ya tatu kwa ubora kama ilivyokuwa katika msimamo.
Yanga ilikuwa na ngome
ngumu zaidi kwa kuruhusu mabao 14 tu, Azam FC na Kagera Sugar zikashika nafasi
ya pili zikiwa ‘zimeachia’20 kila moja.
Demunga ni nahodha wa
timu ya taifa ya Burundi, lakini atacheza na Joseph Owino, mmoja wa mabeki bora
waliowahi kuichezea Simba kabla.
Tegemeo hapa ni mabeki
hao kubadili mwelekeo hasa kwa kuwa msimu uliopita, Simba ilihaha kutokana na
kutokuwa na mabeki wawili wa kati wa uhakika.
Mgeni mwingine ni Amis
Tambwe, alikuwa nahodha wa Vital’O ambaye hivi karibuni aliingoza timu hiyo
kubeba Kombe la Kagame nchini Sudan.
Pamoja na kombe, akaibuka
kuwa mfungaji bora na mchezaji bora wa michuano hiyo. Maana yake Simba watakuwa
wanasubiri mazuri kutoka kwake na msaada mkubwa.
Sasa wana Betram Mombeki,
kama ataongezeka Tambwe maana yake watakachokuwa wanasubiri Msimbazi ni
kutikiswa mfululizo kwa nyavu za timu pinzani.
Msimu uliopita Simba
ilifunga mabao 38 na kushika nafasi ya tatu kwa upachikaji mabao huku ikiachwa
mbali na mabingwa Yanga waliokuwa na mabao 47, huku Azam FC ikiwa na mabao 46.
Kama ina mfungaji na
mchezaji bora wa michuano ya Kagame, basi Simba inategemea ‘kuchenji’ gia na
kupachika mabao mengi zaidi.
Coastal:
Odula na Lutimba kwa
upande wa Coastal Union pia watatakiwa kuonyesha uwezo zaidi. Kikubwa
walichonacho pamoja na kufanya vizuri katika ligi za nchi zao, Kenya na Uganda,
wana umri chini ya miaka 25.
Kwa umri huo maana yake
ni vijana na wanaweza kupambana na ushindani wa aina zote kwa maana ya kasi na
nguvu.
Azam FC:
Wageni wao pia hawana
kamba mguuni, maana walikuwepo msimu uliopita na sasa wanajua kipi cha kufanya.
Wote ni viungo na
washambuliaji, raha zaidi mfungaji bora msimu uliopita, Tchetche, kutoka Ivory
Coast, ndiye alikuwa mfungaji bora.
Lakini ndugu yake, Balou,
ameonyesha ana uwezo kwa misimu miwili sasa, lakini anaweza kuongeza. Bryan
Umonyi (Uganda) na Wakenya wawili Jockins Atudo na Humfrey Mieno wana msimu
mmoja, lakini pia ni ‘majembe’ na msimu huu utakuwa wa kwao kuthibitisha kuwa
wanaweza.
Yanga:
Mnyarwanda Haruna
Niyonzima na mwenzake, Mbuyu Twite mwenye asili ya DR Congo, hawa wamekata
tiketi kwamba ni ‘shoka’ na kazi wanaiweza, lakini bado watu wanategemea zaidi
na inawezekana.
Lakini kazi bado kwa
Didier Kavumbagu (Mrundi), pamoja na kwamba alionyesha ni mzuri wa kupachika
mabao, lakini msimu uliopita hakukaa sawa sana.
Alianza mzunguko wa
kwanza kwa kasi ya kimondo, halafu mzunguko wa pili ‘gari likakata mafuta’ sawa
na Mganda, Hamis Kiiza.
Kiiza amekuwa ‘majikupwa
majikujaa’, maana haeleweki yuko katika kasi ipi, leo 60, kesho 10. Lazima
afanye mabadiliko ingawa kama atafuzu majaribio Lebanon, basi atakuwa
amejiondoa katika ushindani.
Wakati wa kipindi cha
maandalizi ‘pre-season’, wageni hao walipewa asali na samli, lakini sasa ni
wakati mwafaka wa kupewa jembe wakalime na kazi inaanza kesho.
FIN.
0 COMMENTS:
Post a Comment