Kiungo wa zamani wa Simba, Mwinyi Kazimoto, ameanza ‘kula bata’ au
maisha na klabu yake mpya ya Al Markhiya SC ambayo imekwenda kuweka kambi
nchini Tunisia.
Kazimoto
alijiunga na klabu hiyo hivi karibuni kwa mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea
Al-Markhiya ya Qatar kwa dau la dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 80) na tayari
amepata Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Al Markhiya SC imeenda kuweka kambi katika nchi hiyo ya Afrika
Kaskazini kujiandaa na Ligi Daraja la Pili nchini Qatar ambayo inatarajia
kuanza Septemba, mwaka huu.
Mmoja wa Watanzania waliompeleka Kazimoto nchini humo, ameliambia
Championi Ijumaa kwamba kiungo huyo ameshaanza kuzoea mazingira na atakuwa
nchini Tunisia kwa wiki mbili au tatu.
“Hadi sasa wana wiki moja wakiwa Tunisia, sasa sijajua vizuri ratiba
ya timu yao kama ni wiki mbili au tatu ambazo wamepanga kukaa huko,” alisema.
“Baada ya hapo, watarejea hapa Doha kwa ajili ya kumalizia maandalizi
kabla ya kuanza kwa Ligi Daraja la Pili. Timu kadhaa za hapa hupendelea
kusafiri nje ya Qatar, hasa wakati wa kipindi cha maandalizi.”
Kazimoto amejiunga na timu hiyo akitokea Simba ambayo ameitumikia kwa
misimu miwili, kabla ya hapo alikuwa akiichezea Ruvu JKT ya Pwani.
0 COMMENTS:
Post a Comment