MWENYEKIKTI wa Kamati ya uchaguzi ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Hamidu Mbwezeleni ametangaza uchaguzi mkuu
wa shirikisho hilo utafanyika Oktoba 20, mwaka huu.
Kauli hiyo ya Mbwezeleni ni sawa na
hatua moja upya kwa wapenda soka nchini, kwamba angalau siku ya uchaguzi
imejulikana na sasa mijadala inaanza kupaa.
Kwanza ni kuhakikisha haki inatendeka na
hakuna mambo yatakayosababisha msigano kama ilivyokuwa awali, lakini hata wagombe
lazima wakubali kwamba kuna kufuatwa kwa sheria.
Sitegemei mtu asiyekuwa na vigezo
akienguliwa eti ionekana ameonewa kwa kuwa kama pia atapata nafasi siku zijazo
tutahoji kwamba ilikuwaje akaruhusiwa akapita.
Kikubwa hasa ambacho nimelenga kujadili
leo ni kuhusiana na suala la kamati hiyo chini ya TFF kuamua kuiweka siku ya
uchaguzi mkuu siku ambayo Simba itaikaribisha yanga kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Kwangu naona ni kichekesho, pia naona
kumbe hakuna tofauti kati ya ujanjaujanja wa kubabaisha mambo kati ya TFF na
uongozi wa Simba ulivyofanya katika mikutano yake miwili.
Simba imekuwa ikitumia staili ile ya
kizamani, viongozi wa kizamani ambao huwapumbaza wanachama wao katika mikutano
muhimu ya mwaka kwa kuhakikisha siku hiyo kuna mechi.
Ntakukumbusha mkutano uliopita wa
wanachama wa Simba, pamoja na uongozi kuwa na mapungufu mengi, Mwenyekiti
Ismail Aden Rage aliuondesha mbiombio, ukiwa umepangiwa vitu kibao vya
kubabaisha.
Kama haitoshi, Simba siku hiyo ilikuwa
inacheza mechi ya kirafiki dhidi ya URA ya Uganda. Hivyo wanachama wake
walikuwa na hofu kupita kiasi, walitaka mkutano uishe ili wakaone mechi na
‘janja’ ya Rage akawaambia kila aliyekuwa na ‘beji’ ya kuingilia kwenye mkutano
huo, basi ndiyo kiingilio cha mechi.
Baada ya hapo, hakuna aliyekuwa amehoji
kuhusiana na mambo muhimu ya mapato na matumizi au mwenendo wa klabu kwa sababu
ya mechi ya kirafiki.
Kamati hiyo ya uchaguzi ya TFF pia
imeangukia huko, sasa imeweka uchaguzi mkuu, siku ambayo Simba na Yanga
zinapambana Uwanja wa Taifa.
Kila mmoja anajua namna kunavyokuwa na
presha kubwa siku ya mechi hiyo, kila mmoja anataka kuwahi uwanjani na hii ni
sehemu ya kufanya mambo yaende haraharaka bila ya kutafakari kwa kina.
Sioni kama kulikuwa na ulazima huo,
ingewezekana angalau siku moja kabla uchaguzi huo ungefanyika na baada ya hapo
mechi ikafuatia. Lakini watu kuchagua viongozi huku wakiwaza watakwenda
uwanjani saa ngapi, tena wakiwa wanatakiwa kuwahi si sahihi.
Ndiyo maana Napata hofu hapa kwamba kutakuwa
kuna kitu kinasukwa ambacho pia lazima hakitakuwa sahihi kwa kuwa kinalenga
kusaidia kitu au upande fulani.
Uchaguzi wa TFF ni kitu muhimu muhimu
katika soka ya Tanzania, uongozi unaoingia unakuwa madarakani kwa miaka minne,
si kitu kidogo. Sasa kuna sababu gani ya kuwalazimisha watu wakifanye kwa hofu
au kwa kulipua?
Kwani ingepangwa siku moja kabla au
baada, kungekuwa na tatizo gani? Nafikiri ni wakati wa wahusika kuangalia
kwamba tumepiga hatua na lazima tuwe na fikra sahihi zinazolenga kujenga.
Upuuzi ambao umekuwa ukifanywa na klabu
zetu kwa lengo la kuwapumbaza wanachama ambao wamekuwa wakikubali kilaini, leo
unaingia tena hadi kwenye shirikisho ambalo ni baba na linatakiwa kuonyesha
tofauti, hii si sahihi.
0 COMMENTS:
Post a Comment