Wakati bado akiwa na kibarua Yanga,
Kocha Mkuu, Ernie Brandts amepata timu ambayo inataka akafanye kazi nchini
Chile.
Taarifa zinaeleza kuwa timu hiyo kutoka
Chile imepiga simu katika klabu ya APR ya Rwanda ikitaka mawasiliano na Brandts.
Mmoja wa viongozi wa APR ameliambia
gazeti hili kuwa klabu hiyo ya Chile imekuwa ikiwasumbua kutaka mawasiliano na
Brandts nao walichofanya ni kumuunganisha nao.
“KIla siku wanasema wanataka kuzungumza
naye, tuliwaambia wapige Yanga. Lakini wao wameendelea kupiga hapa, tumewapa
namba wamtafute, wakasema haipatikani. Tumetafuta na kuwapatia nyingine sasa
hatujui kama wamezungumza naye,” alisema ofisa huyo aliyekataa kutajwa
kuhusiana na hilo kwa madai haliihusu klabu yake.
Alipoulizwa Brandts kuhusiana na hilo,
akasema hivi karibuni hajawahi kupata simu kutoka Amerika Kusini. Lakini kabla
aliwahi kuwasiliana na wakala aliyemuambia jambo hilo.
“Hakuna aliyenipigia wakati huu, lakini
kabla sijakwenda Ujerumani kuna wakala aliwasiliana na mimi na kunieleza kuna
timu ya Amerika Kusini inanihitaji,” alisema na alipoulizwa uamuzi wake ukoje.
“Niliwaeleza bado nina mkataba na Yanga,
hivyo tungeweza kuzungumza wakati mwingine na kujua nini cha kufanya.”
Brandts ameipa Yanga ubingwa wa Tanzania
Bara, lakini kabla alikuwa kocha wa APR ambayo aliibebesha ubingwa wa Rwanda na
makombe mengine mawili.
0 COMMENTS:
Post a Comment