Ushindi wa
Mtanzania, Francis Cheka kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Dunia unaotambuliwa na
WBF si kitu kidogo, hivyo ni furaha karibu kwa kila Mtanzania anayeipenda nchi
yake.
Natambua Cheka
hawezi kukosa wapinzani, wako Watanzania waliotamani achapwe na Mmarekani,
Phills Williams kwa kuwa huenda wao hawamuungi mkono.
Lakini kwa
Wazalendo wa nchi yetu, hakuna hata mmoja ambaye angetamani kuona mambo hayo
yanatokea, badala yake kila mmoja alitamani bondia huyo kutoka Morogoro
anaiwakilisha Tanzania vema kama alivyofanya, hongera Cheka.
Pamoja na
ushindi wa Cheka, kuna mambo mengi sana ya kujifunza ambayo tunalazimika
kuyafanyia kazi mapema ili kuondoa hatari mbele yetu. Kwamba wakati mabondia au
wanamichezow anajiandaa, hakuna watu wengi wanaojitokeza kwa ajili ya kusaidia.
Kusaidia
inawezekana ikawa ni mapenzi ya mtu mmoja mmoja, lakini bado nina imani kuwa
kwa pambano la kimataifa kama alilopigana Cheka, basi lazima Watanzania
walitakiwa kuonyesha ushirikiano tokea mwanzo.
Cheka
alikuwa anapigana kwa ajili ya nafsi yake, lakini anategemea msaada na nguvu ya
Watanzania kwa kuwa anapigana kama mwakilishi wa taifa, ndiyo maana Watanzania
kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, tuliimba wimbo wetu wa taifa, tena hata bila
ya mlio wa ala yoyote ya muziki.
Furaha ya
Cheka leo ni juhudi ya watu wachache sana, ukianzia yeye, kocha wake, familia
yake na Watanzania wachache waliojitokeza kumsaidia kuhakikisha anafanya vizuri
katika pambano hilo.
Ukiachana
na mtu mmoja, narudi upande wa serikali na hili nimekuwa nikilia nalo kwa
kipindi kirefu sana. Inawezekana linaonekana la kawaida kwa kuwa
anayelizungumza anaitwa Saleh Ally na hana mamlaka yoyote serikalini na wala si
mbunge wala mwanasiasa.
Mengi
nimefanikiwa kuyabadilisha kwa kuwa nimekuwa nikiandika bila kuchoka, hata hili
najua siku itafika na mambo yatabadili.
Nasisitiza hivi, serikali lazima
iingize nguvu zake katika mapambano ya michezo mbalimbali inayolihusisha taifa.
Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenalla Mukangara alikuwa mgeni rasmi,
sina nia ya kumsema vibaya lakini namfikishia ujumbe wangu.
Kwamba
kufika kwake usiku wa pambano hilo ni kuonyesha uzalendo na anastahili pongezi,
lakini bado yuko katika kundi la wale wahusika ambao hawakutaka kujua Cheka
amejiandaa vipi na atapambana vipi.
Cheka ni
mwakilishi wa wananchi na serikali yao, hivyo ilikuwa ni lazima wizara iliyo
chini ya Mukangara ifanye jambo ikiwa ni pamoja na kufuatilia maandalizi ya
Cheka kama yalikuwa yanakwenda vizuri na kama kuna upungufu, basi mambo yawekwe
sawa.
Lazima
tukubali, wanamichezo wengi nchini wana maisha duni na wanahitaji msaada kila
wanapokuwa wanajiandaa na mapambano yao. Kama itakuwa wanapambana wenyewe,
yaani Watanzania kwa Watanzania, serikali inaweza isihusike, lakini ikifikia
kuwania ubingwa ambao unamhusisha bondia wa nje, basi wasaidiwe.
Tabia ya
kusubiri mabondia washinde, halafu wengine wajitokeze na kujipatia sifa ya
kutaka kama walifanya kitu si sahihi. Najua baada ya muda utaanza kusikia Cheka
amekaribishwa sehemu mbalimbali zinazohusisha viongozi wa serikali ambao
walikaa kimya kabisa wakati akijiandaa.
Najua,
kuelezwa ukweli kwa wengine kunachukuliwa kama kudharauliwa kwa kuwa utamaduni
wa mkubwa kukosolewa na mdogo unaonekana ni kama dharau, mimi sijali hilo.
Ila
ninawasisitiza, wanaohusika na michezo wana kila sababu ya kubadilika na
kuwasaidia wanamichezo wa Kitanzania kama nilivyoeleza, hali yao ni duni
kimaisha na fedha wanazopata kwa ajili ya kujiandaa ni ndogo sana.
Cheka ana
maisha duni, kazi yake ni kuuza chupa za plastiki na wakati fulani aliishi kwa
kukota chupa za soda na kwenda kuziuza, mnalijua hili. Hivyo wakati mmesikia
anajiandaa, basi mlitakiwa na kumsaidia kwa kuwa anafanya hivyo kwa ajili ya
taifa.
Ameshinda,
acha tufurahi wote kwa kuwa tuna haki ya kufanya hivyo. Lakini shujaa huyo
mlimtenga na kusubiri mafanikio yake, kitu ambacho si sahihi na mabadiliko
yanatakiwa. Ninaamini mmenielewa, ila nawakumbusha zaidi, mkijikausha,
nitawakumbusha tena bila ya woga.
SOURCE:
CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment