Kana utaamua kuzungumza kuhusu matatizo yanayoendelea katika timu mbalimbali
zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, basi huenda usipate nafasi ya kuzungumza mambo
mengi ya msingi.
Matatizo ni
mengi sana lakini viongozi wamekuwa wakifanya kila namna kuhakikisha wanayaziba
ili kuonekana walipo, kila kitu kimetulia.
Walipo binadamu, matatizo
hayakosi kwa kuwa ‘wana undugu’, lakini yako yale ambayo yanaweza yakatatuliwa
na kufanya mambo yakaenda vizuri.
Timu nyingi
zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, zikiwemo kongwe za Yanga na Simba, zina madeni kwa
kuwa wachezaji wake wanadai fedha za usajili.
Fedha za
usajili mara nyingi hutolewa kwa mafungu na nyingine huwa ni ahadi tu, lakini
limekuwa ni tatizo kubwa kuwachezaji kupata haki zao baada ya usajili
kukamilika.
Mambo mengi
hasa katika timu hizo kongwe hayako katika mpangilio sahihi, wanaofanya kazi
hata wao wanajua lakini wanalazimika kuonyesha mambo yanakwenda vizuri kwa kuwa
wao ni viongozi.
Kuficha
upuuzi hakuwezi kusaidia ujenzi mzuri wa ukuta bora uliolenga kufanikisha
busara. Hakuna ubishi busara ina sehemu husika, inawezekana wakati mwingine
haihitajiki na utekelezaji unatakiwa kuchukua nafasi.
Hakuna
busara inayohitajika kwa viongozi wanaodaiwa na wachezaji zaidi ya kuwalipa tu,
wanatakiwa kufanya utekelezaji au kutimiza ahadi walizowaahidi wachezaji wao.
Wachezaji
wengi wamekuwa wakilalama, wanasema malalamiko yao chinichini kwa hofu ya
kutoonekana wasaliti au kuingia katika migogoro na viongozi wao.
Wengi wao
wamekuwa wakikata tamaa na kuona kama wanadanganywa, lakini wakweli wamekuwa
wakionekana wasaliti bila ya kujali wanayodai ni haki yao.
Hivyo ni
vema viongozi wa timu zote zinazoshiriki ligi kuu wakaliangalia hilo, walipeni
wachezaji fedha zao kama mlivyoahidi ili kujenga morali sahihi ya timu. Lakini
hakuna sababu ya kulazimisha uadui miongoni mwa wale wanaodai haki zao.
Lazima mjue
hata kama nyie ni viongozi, basi wachezaji nao wana haki zao na ndiyo
wanaouunda kundi linawapa nyie vyeo vya kuitwa viongozi.
Kawaida
jamii imekuwa ikichukua wasema kweli, isipokuwa watu wachache tu wanaojua
kwamba ukweli ni kitu kizuri na watu wanapaswa kuwa huru kuzungumza kitu chenye
chembe za ukweli.
Ukitaka
kuona kama ukweli unaonekana si kitu kizuri, angalia pale klabu zinapoguswa,
mfano wasikie mchezaji analalamika hajalipwa, au kuelezwa kwamba wamechelewesha
fedha za malipo fulani wanazodaiwa na wachezaji wao.
Nguvu ya
kukanusha au kujibu inakuwa kubwa sana, vizuri nguvu hiyo ingetumika
kuhakikisha wanaodai wanalipwa ili kuwajenga vizuri kisaikolojia katika hali ya
ushindani.
Mchezaji
anayedai, mwenye hofu ya kulipwa na hofu ya kuonekana adui kama ataulizia zaidi
ya mara mbili kuhusu haki haki yake, atacheza vipi mpira akiwa na ari ya
ushindi? Mwisho mnajisahau na kuwaangushia lawama tu. Kukubali ni sehemu ya
kujifunza hasa kama ukiona kuna upungufu, hivyo ili wasawadai, basi walipeni
haki hao ili muwe katika mstari mzuri wa kujaza nia na akili zenu katika kazi
yenye mafanikio.
0 COMMENTS:
Post a Comment