September 9, 2013



KAMANDA WA KIKOSI CHA KUZUIA NA KUPAMBANA NA MADAWA YA KULEVYA TANZANIA, GODFREY NZOWA YALIYOWAHI KUKAMATWA.
*Alitumia umafia kukwepa mitego ya Mwakyembe
Na Mwandishi Wetu
Sura ya Tanzania inazidi kuchafuka katika suala la usafirishaji wa madawa haramu ya kulevya baada ya mshambuliaji wa zamani wa Simba, kumatwa na madawa ya kulevya kwenye uwanja wa ndege.


Mshambuliaji huyo aliyewahi kuichezea Simba mwanzoni mwa miaka ya 2000 amekamatwa na madawa ya kulevya siku tatu zilizopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Vyombo vya habari vya Ethiopia vimetangazwa kukamatwa kwa wanamichezo wawili, mmoja akijitambulisha ni mchezaji wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars.

Taarifa hizo zimeeleza kwamba walikamatwa baada ya kutoa Bole wakitokea Burundi na wote wawili walikuwa na pasi za kusafiria za Tanzania.

Inaonyesha wazi, uamuzi wa kupitia Bujumbura ili kukwepa ukali wa ulinzi ulioboreshwa kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe kutaka mambo yawe hivyo na kulivalia njuga suala la madawa ya kulevya.

Mwanamichezo mwingine alielezwa kuwa aliwahi kuwa bondia, taarifa hizo zimeeleza kuwa alikamatwa wakati akipanda ndege kutaka kutoka Addis Ababa kwenda Zurich, Uswiss ambako angepanda treni kwenda Stockholm, Sweden anakoishi.

Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa alisema yuko nje ya nchi kikazi lakini akaahidi kulishughulikia suala hilo.

“Niko nje ya nchi kikazi, sina taarifa na suala hilo zaidi ya ile meli iliyokamatwa Italia na madawa na imesajiliwa Tanzania. Lakini nitalifanyia kazi, nipe muda nilikabidhi kwa Interpol na watalifanyia kazi,” alisema.

Lakini Mtanzania mwingine anayeishi nchini Sweden alisema kuna taarifa za kukamatwa kwa mwanasoka Mtanzania ambaye anaishi nchini humo.

“Tumeambiwa ni (anamtaja), unajua sasa alikuwa hachezi soka na taarifa zimezagaa eneo kubwa la Stockholm. Lakini bado hatujawa na uhakika.

“Huyo mwanamichezo mwingine (anamtaja), alikuwa na mke mzungu hapa na amepigiwa simu kwamba mumewe amekamatwa. Sasa tunaendelea kusubiri uthibitisho kuhusiana na hilo,” alisema Mtanzania huyo ambaye ameishi Sweden kwa zaidi ya miaka sita sasa.

Juzi na jana, taarifa za kukamatwa mwanamichezo mwingine, bondia Mbwana Matumla katika mpaka wa Ujerumani na Uswiss akiwa na madawa zilizagaa.

Kamanda Nzowa pia alisema analifuatilia hilo lakini kaka yake mkubwa, Rashid Matumla alisema suala hilo halina uhakika.
“Nimekuwa nikimtafuta Mbwana kwenye simu kwa zaidi ya siku kumi bila ya mafanikio, ukweli hatuna uhakika na suala hilo na tunaendelea kulifuatilia.

“Napenda tupate uhakika kwanza, ninawashauri watu kuacha kusema moja kwa moja kama ni kweli hadi tutakapopata uhakika kwa kuwa sijampata kwenye simu hadi sasa,” alisema Matumla.

Taarifa nyingine zimeeleza kuwa, mwanasoka huyo aliyenaswa alikuwa jijini Dar siku chache zilizopita na kuonyesha kufuru ya fedha baada ya kutumia zaidi ya shilingi milioni mbili kuwatuza wanamuziki wa bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ katika onyesho lake moja jijini Dar.

Tatizo la Watanzania kukamatwa na madawa ya kulevya ndani na nje ya nchi linazidi kukua na kuichafulia sifa nchi hii.
Katika nchi mbalimbali kama utaonyesha pasi ya kusafiria ya Tanzania, wengi wamekuwa na hofu kutokana na sifa hiyo.
SOURCE: CHAMPIONI.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic