| ANDY COLE AKIZUNGUMZA NA SALEH ALLY KATIKA MAHOJIANO MAALUM. YUKO HAPA NCHINI KWA AJILI YA KAMPENI YA MIMI NI BINGWA INAYOENDESHWA NA KAMPUNI YA AIRTEL TANZANIA |
Na Saleh
Ally
IMEKUWA si rahisi
kwa wapenda soka wengi kukumbuka kwamba maisha ya soka ya mshambuliaji Andrew
Alexander Cole, maarufu kama Andy Cole, yalianzia Arsenal.
Labda
inatokana na kwamba mafanikio makubwa aliyapata akiwa na Manchester United,
Cole hajawahi kusahau hata kidogo kuhusiana na Arsenal kwa maana ya maisha yanavyotakiwa
kuwa, unapoanzia unapajua, lakini hujui mwisho wake.
Baada ya
mambo kutokwenda vizuri na Arsenal, Cole alipelekwa Fulham iliyokuwa daraja la
kwanza kwa mkopo na baada ya mechi 13 akiwa amefunga mabao matatu tu, akauzwa
katika klabu ya daraja la kwanza ya Bristol aliyoifungia mabao 20 katika mechi
41, hii ni katika msimu wa 1992-93.
| AKIKABIDHIWA KIFAA CHA MIMI BINGWA |
Uwezo wake
uliwavutia Newcastle, maana yake akarejea tena Ligi Daraja la Kwanza England,
ikiwa ni baada ya msoto wa zaidi ya miaka mitatu. Akaisaidia kubeba ubingwa na
kupanda ligi kuu.
Utaona
baadaye akipita Newcastle, Manchester City, Blackburn Rovers, Fulham na
Manchester United, Cole anaingia kwenye rekodi baada ya kuweka rekodi ya kuwa
mfungaji bora wa pili mwenye mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu England, kinara
ni Allan Shearer.
Cole yuko
hapa nchini katika kuiongezea nguvu promosheni ya Mimi ni Bingwa inayoendeshwa na
Kampuni ya Simu ya Airtel na hii ni mara yake ya pili kuja nchini. Mara ya
kwanza ilikuwa ni 2011 na alikuja kwa ajili ya Airtel Rising Stars.
Katika
mahojiano maalum kati ya Cole na Championi Jumatatu, mshambuliaji huyo nyota
enzi hizo, anasema hakuna kitu kinachopatikana kwa urahisi huku akisisitiza,
programu ya Airtel Rising Stars ina nafasi ya kuleta mabadiliko katika soka
Tanzania lakini bado kuna mambo ya kufanya.
Championi:
Unafikiri kuna kitu cha kuiongezea Airtel Rising Star?
Cole: Hiyo
ni programu na ina kila nafasi ya kufanya vizuri, lakini watu ndiyo wanatakiwa
kuongoza kila kitu kupitia makundi yao.
Championi:
Unaweza kufafanua zaidi?
Cole: Mfano
wanaokuzwa ni vijana, wanaofanya kazi ya kuwaendeleza ni makocha na wahusika
wengine. Wote wanatakiwa kujituma, kuwa na nia ya kuzifikia ndoto zao kwa kuwa
Airtel itawapa vifaa vyote kama mipira, jezi na vitu vingine, lakini wao
watatakiwa kufanya kitu.
Championi:
Wewe unaweza kuwa mfano, uliuzwa hadi timu ya daraja la pili ukitokea ligi kuu
ukiwa na Arsenal, ilikuwaje uliweza kuamka na kufikia hapa ulipo?
Cole:
Haikuwa kazi rahisi hata kidogo, sikulala kwa kuwa lengo langu lilikuwa ni
kufikia ndoto yangu ya kuwa mshambuliaji bora.
Championi:
Unafikiri Tanzania ina nafasi siku moja ya kupata mchezaji atakayecheza Ligi
Kuu England?
Cole:
Inawezekana kabisa, lakini kama nilivyosema kuwa na ndoto, halafu juhudi na
maarifa kutaka kuzifikia.
Championi:
Labda kama Tanzania tunahitaji muda wa miaka mingapi kufanikiwa katika hilo?
Cole: Nani
anajua? Inawezekana ni siku chache zijazo, inategemea na wahusika wanavyoitumia
nafasi hiyo bora wanayopewa na Airtel, kwanza waamini si kitu kidogo na
wakifanyie kazi.
Championi:
Kuja Tanzania kwa Andy Cole si kila kitu, labda nini kingine cha kufanya?
Cole:
Kikubwa ni vijana, angalieni sana hilo. Bila kuwakuza na kuwaendeleza hakuna
mafanikio, ndiyo maana nasema Airtel wamefanya kitu bora, muwaunge mkono.
Championi:
Tukirudi England, umekuwa na mafanikio makubwa, mmoja wa wafungaji bora katika
historia, umecheza timu kubwa kama Arsenal, Man United, Man City. Vipi
Liverpool, hukuvutiwa nayo?
Cole:
(Tabasamu), inawezekana lakini ukweli ni kwamba nimecheza Manchester United kwa
mafanikio makubwa. Sidhani kama nilihitaji tena kwenda Liverpool, ila sina
chuki nayo.
Championi:
Vipi pamoja na kuwa bora, uliamua kumaliza soka lako England, hukupenda
changamoto nje ya nchi yako na hasa Hispania au Italia kama ilivyokuwa kwa
Beckham, Owen na wengine?
Cole: Kwangu
kucheza Premiership ni kitu cha kujivunia, napata kila kitu na ukisema ubora
pale ni zaidi. Bado utaona tunacheza na wachezaji wa kila nchi, Ligi ya
Mabingwa unakutakana pia na timu za Hispania, Italia.
Championi:
Umekuwa bora katika ufungaji mabao, lakini huna umbo kubwa sana, hilo liko vipi?
Cole: Hisia
hizo zimekuwa potofu, wengi wanaamini hivyo kwamba watu wenye miili mikubwa
ndiyo wanaweza kufunga. Kikubwa kipaji, mazoezi na kujituma, ndiyo maana
nimefanikiwa.
Championi:
Vipi kufanya kazi na Alex Ferguson, kuna ugumu?
Cole:
Ferguson si mtu lelemama, hapendi watu wazembe na siku zote ukiwa unajituma na
unafanya kazi vizuri, basi unakuwa rafiki yake mkubwa.
Championi:
Kabla ya kuja hapa mwaka 2011, uliwahi kusikia lolote kuhusu mpira wa Tanzania?
Cole: Kweli
hapana, nchi hii si maarufu kisoka kama Ghana, Afrika Kusini, Cameroon.
Mnahitaji kukua ingawa wakati juhudi zinafanyika, lazima mkubali muda
unahitajika, kidogokidogo tu.
Championi:
Timu yako ya zamani Manchester United inayumba sasa, unafikiri itakaa vizuri?
Cole: Hiki
ni kipindi cha mpito tu, Manchester United itasimama na kufanya vizuri. Kwa mabadiliko
ya kocha ilikuwa ni lazima iwe hivyo.
Championi:
Vipi wanaweza kuwa mabingwa au angalau kupata nafasi nne za juu?
Cole:
Lolote linawezekana, ingawa naweza kusema wakikosa ubingwa, sidhani kama
watakosa hata nafasi ya nne. Tusubiri.
MAKOMBE
ALIYOWAHI KUTWAA:
Arsenal
Ngao ya
Jamii ya FA (1991)
Newcastle
United
Ubingwa
Ligi Daraja la Kwanza (1992-93)
Manchester
United
Ligi Kuu
England (mara 5)
Kombe la FA
(mara 2)
Ngao ya
Jamii (mara 2)
Ligi ya
Mabingwa Ulaya (mara moja).
FIN.







0 COMMENTS:
Post a Comment