January 15, 2014



LISSU ALIPOTEMBELEA GLOBAL PUBLISHERS, JANA.

Na Saleh Ally
MMOJA wa wanasiasa machachari nchini ni Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).


Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), amekuwa akitajwa karibu kila sehemu yanapozungumziwa masuala mbalimbali yanayohusiana na siasa hapa nchini kutokana na umaarufu alionao.

Lakini Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amekuwa akizungumziwa au kuhusishwa karibu kila sehemu inayohusisha vurugu, mfano bungeni na amekuwa na sifa ya kutokuwa na woga hata kidogo.
 
LISSU AKIFAFANUA JAMBO.
Kwa sasa ni kati ya wanasiasa walio msitari wa mbele kupambana katika sakata linaloendelea dhidi ya mbunge mwingine kijana na machachari, Zitto Kabwe. Hayo yote, yanabaki kuwa yao lakini tukirudi kwenye michezo, Lissu ana mengi ya kusimulia.

Kuna watu ambao hawaamini kama wanasiasa wanaweza kuwa na muda wa kufanya mazoezi au kuvutiwa na michezo mbalimbali.
Pamoja na pilika za kisiasa na mapambano ya kila siku, Lissu anasema anavutiwa na michezo mbalimbali lakini soka ndiyo namba moja.

Bila ya kujali rangi za njano na kijani, anasema kwa hapa nyumbani yeye ni shabiki wa kikosi cha mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, ambao wameweka kambi nchini Uturuki kujiandaa na mzunguko wa lala salama wa ligi hiyo pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, Lissu ana zaidi ya miaka kumi hajawahi kugusa uwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara zikipigwa kwenye uwanja wowote ule na zaidi amekuwa akilazimika kuangalia kwenye runinga.

Si kwamba hana muda au hana uwezo wa kufika uwanjani, badala yake kinachosababisha asifike uwanjani ni mashabiki wa Simba. Unaweza kujiuliza wao wanamzuia vipi kufika uwanjani wakati anashangilia timu nyingine?

“Mimi napenda sana mpira, timu yangu ni Yanga. Ila siku hizi sipendi kabisa kwenda uwanjani kuangalia mechi, napenda kuangalia kwenye runinga tu,” anasema Lissu.

“Mara nyingi naangalia nyumbani kwenye runinga au hata baa, nakaa naangalia na si kwenda uwanjani,” anaongeza.  Alipoulizwa sababu ya kutokwenda uwanjani wakati ana uwezo wa kufanya hivyo, alisema:

“Nakumbuka mwaka 1993 nilikwenda uwanjani wakati Simba ilipocheza na Stella (ya Ivory Coast), siwezi kuisahau siku hiyo namna mashabiki wa Simba walivyonifanya, sijasahau hadi leo.”

Siku hiyo Simba ilicheza mechi ya fainali ya Kombe la Caf dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast. Wakati mashabiki wengi walijitokeza Uwanja wa Taifa, Temeke jijini Dar es Salaam wakiamini Wekundu wa Msimbazi wangebeba kombe hilo, mambo yalikuwa tofauti.

Wengi waliamini Simba ingeshinda kutokana na mambo mawili, kwanza sare ya bila kufungana waliyoipata ugenini mjini Abidjan.  Lakini pia ulikuwa ni ubora wa kikosi cha Simba kilichokuwa na wachezaji kama Mohammed Mwameja, George Masatu, Ramadhani Lenny, Hussein Marsha, Edward Chumila, Malota Soma na wengine kibao.

Mwisho wa yote Simba ililala kwa mabao 2-0, huku aliyefunga mabao yote, Boli Zozo, akijijengea jina hapa nchini. Hasira za mashabiki wa Simba zilikuwa juu, walikuwa wakorofi, walikuwa wakiwapiga watu walioamini walikuwa wana furaha wao kupoteza mchezo huo. Lakini vibaka nao wakatumia nafasi hiyo kuchukua riziki haramu.

Lissu anasema akiwa anatokea uwanjani, alikutana na tafrani kama hilo ambalo liliwakuta wengi siku hiyo na wamekuwa wakiendelea kusimulia.

“Nakumbuka nilikuwa nimefika eneo la Kidongo Chekundu, walitokea mashabiki tulioambiwa ni wa Simba, walinizunguka na kunibeba juujuu. Wakati wananishusha chini sikuwa na viatu wala pochi, wangeweza kunivua hata suruali.

“Wakati bado nashangaa, dereva taxi mmoja ndiye alinisaidia kunipeleka Chuo Kikuu, wakati huo nilikuwa bado mwanafunzi. Tangu siku hiyo sijawahi kurudi uwanjani,” anasema.

Kuhusiana na mazoezi, Lissu anasema amekuwa akishiriki ingawa si kwa kiasi kikubwa: “Mazoezi ni kitu kizuri sana, inabidi nishiriki kwa ajili ya kujiweka vizuri tu.”

Kuhusiana na Chadema kushiriki katika michezo, Lissu anasema: “Kweli michezo ni ajira, siwezi kusema tumefanya nini kama chama, lakini naweza kusema katika hili vizuri tukaondoka katika kauli za uhamasishaji, tumechoshwa.

“Usione tuko kimya, tumechoshwa na kauli hizo, sasa ni wakati wa vitendo na kama  tunataka tuwe taifa la michezo kama wenzetu Kenya wanavyofanya vizuri kwenye Olimpiki au mataifa ya Afrika Magharibi na soka, basi lazima tuwekeze kwa vijana na si manen.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic