GUMZO kubwa katika kipindi hiki ni
kuhusiana na suala la tiketi za elektroniki.
Mashabiki wa soka wanaona ni jambo geni,
tumeona katika mikoa ambayo mechi za Ligi Kuu Bara zimechezwa na mfumo wa
malipo ya elektroniki umetumika.
Mashabiki wengi wamelalamika kwamba
mfumo huo hawauelewi na unawapa wakati mgumu sana kuutumia.
Kuna malalamiko kadhaa kama namna ya
upatikanaji kwa tiketi hizo, wengi wanalazimika kwenda kununua sehemu ambazo
wanaona ni mbali.
Imezoeleka kuwa, tiketi za mechi
zinapatikana uwanjani, mtu anapokwenda ananunua palepale na kuingia zake
uwanjani kushuhudia mechi.
Lakini kuna waliolalamika kuwa, wauzaji
wanaonyesha dharau kwa wanunuzi, mfano mzuri yule ambaye alikuwa akifanya kazi
ya kuuza tiketi kwenye moja ya matawi ya Benki ya CRDB wakati Yanga
ilipokaribishwa na Coastal Union mjini Tanga.
Muuza tiketi aliyekuwa na miwani, anaonekana
kutumia muda mwingi kuzungumza na simu wakati mashabiki wa soka wakiwa kwa
wingi wakisubiri kununua tiketi hizo.
Sitaki kuingia kwenye kundi la
wanaoamini kwamba mikataba ya uuzwaji tiketi za elektroniki ni ufisadi au
kashfa kwa uongozi wa TFF ya Leodegar Tenga.
Lakini naliangalia suala hilo kwa njia
hii, kwamba TFF hii ya Jamal Malinzi, inafanya nini kuhakikisha mfumo huo wa
tiketi za elektroniki unakwenda kama inavyotakiwa? Kwa kuwa hata tukiukataa
leo, bado utatumika miaka ijayo kwani dunia ndiko inapokwenda.
Sasa TFF ya sasa inauacha kwa kuwa
haikubaliani nao au kwa kuwa TFF ya Tenga ndiyo iliingia mkataba huo? Maana
kuna mambo mengi ya msingi hayafanyiki.
Zaidi ya kuuzungumzia kizembe, yaani
hakuna nguvu inayotumika kuonyesha kuna mabadiliko, hata namna ya ununuzi wa
tiketi hizo, TFF inategemea kutoa tu taarifa kwenye vyombo vya habari.
Kama TFF haifanyi lolote, mfano
matangazo kwenye runinga, redio au magazeti ili kutoa elimu kuhusiana na mfumo
huo mpya, nani atafanya kazi hiyo?
Kinachofanyika ni Bodi ya Ligi au TFF
kufanya biashara lakini hawataki kufanya matangazo. Wakati mwingine najiuliza,
hata hao CRDB pamoja na uzoefu wao katika biashara, vipi hawatangazi na
kufafanua ili kumaliza maswali mengi ya wapenda soka?
Kinachoonekana ni kwamba, wahusika
wanataka kufanya biashara, lakini wanahofia gharama ya kuitangaza, kitu ambacho
si sahihi hata kidogo.
Tunajua, nchi hii kama ni biashara kwa
kuvizia mikutano au taarifa kwa vyombo vya habari si sahihi. Vipi kuhusu kile
kitengo cha masoko cha TFF?
Lakini Bodi ya Ligi Kuu, kama ilivyo TFF
kwa kuwa wanaingiza fedha, basi lazima wakubali kwamba wana kitu cha kufanya
hasa kufafanua, kuutangaza mfumo huo mpya pamoja na faida zake na si kwenda kwa
kubahatisha tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment