YANGA WAKIJIFUA KWENYE UWANJA WA MAZOEZI WA AL AHLY |
Na Saleh Ally, Cairo
KLABU za Zamalek na Al Ahly ndiyo
unazoweza kuzilinganisha na Yanga na Simba nchini, kama utakuwa unazungumzia
suala la ukongwe na maendeleo.
Unaweza kufanya hivyo kwa maana ya historia
na kuangalia timu zipi ni kongwe na historia ndefu katika nchi husika, lakini
kama ni suala la maendeleo, basi hizo mbili za Misri ndiyo mwili na zile za
nyumbani ni vivuli.
UWANJA WA AL AHLY, TAYARI WAMEANZA KUJENGA MWINGINE AMBAO WATAUTUMIA KWA AJILI YA MECHI. |
Simba na Yanga ndiyo klabu zinazopaswa kuwa
na maendeleo zaidi kuliko nyingine yoyote Tanzania, lakini si hivyo kwa sasa
kwa kuwa zimekuwa na mipango duni, isiyo endelevu kwa kipindi kirefu sana.
Yanga iko hapa Cairo baada ya kucheza
mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya al Ahly, imejifunza mengi
kupitia klabu hiyo kongwe ingawa hakuna litakalofanyiwa kazi kwa kuwa kila mara
timu hizo, iwe Simba au Yanga, zimekuwa zikisafiri na kukutana na mengi ya
kujifunza, wakirejea nyumbani, kila kitu wanakiacha walipokiona, maana yake
hawajifunzi zaidi ya kushangaa.
ENEO LA MADUKA KATIKA ENEO LINALOMILIKIWA NA KLABU YA ZAMALEK, NYUMA UNAONEKANA UWANJA WAKE WA MAZOEZI. |
Jana asubuhi, Yanga walifanya mazoezi
yao wa mwisho kwenye Uwanja wa Al Ahly, hapo ndiyo makao makuu ya klabu hiyo,
katikati mwa jiji hili.
Wachezaji walionyesha kufurahishwa na
kushangazwa, namna ambavyo wenzao wana mazingira mazuri kupitiliza ya kazi. Ndani
ya uwanja kuna vyumba vya kupumzikia ambavyo kuna vitanda 20 kwa mchezaji iwapo
atataka kupumzika.
Kuna chumba maalum kwa ajili ya mafunzo
au wachezaji kujipumzisha na runinga kubwa imeweka huku makochi yakiwa
yamepangwa kwa mpangilio mzuri sana.
Achana na suala kuwa na gym bora, bado
wana uwanja wa kisasa kabisa wa kufanyia mazoezi ambao Yanga na Simba, tokea
miaka ya 1930 zilipoazishwa, imekuwa ni hadithi tu, huku Watanzania wakiendelea
kuonyeshwa ramani za viwanja.
Ndani ya klabu hiyo, kuna mgahawa mkubwa
wenye uwezo wa kubeba zaidi ya watu 300 kwa wakati mmoja na biashara yakiwemo
maduka mbalimbali yakiendelea.
Kabla ya hapo, Championi Jumatano
lilifanya ziara kwenye Uwanja wa Zamalek ambao hauna tofauti kubwa na ule wa Al
Ahly, pia wana mgahawa mkubwa ambao unaingiza watu zaidi 200 wakiwa wamekaa
safi kabisa.
Lakini Zamalek inamiliki eneo kubwa na
limepangishwa maduka, mmoja wa viongozi ameliambia gazeti hili, asilimia 28 ya
mapato yao yanatokana na hayo maduka kwa kuwa wafanyabiashara zaidi ya 36
wamekodisha na wanalipa pango.
Yanga ina eneo Mtaa wa Mafia, Kariakoo,
hakuna cha maana kinachoendelea. Simba wana maduka makao makuu ya klabu yao,
fedha zinaingia matumboni mwa wajanja, ni majanga tu.
Ahly ni kati ya klabu zinazomiliki kituo
kikubwa cha runinga barani Afrika. Yanga na Simba hawawezi? Lakini wamewahi
hata kufikiri na kufanya mipango ya kuanza taratibu?
Ahly na Zamalek sasa hawana kipato cha
mashabiki tena, wanategemea wadhamini na miradi hiyo ndiyo inachukua nafasi ya
mapato yao ya milangoni ili kuendelea kulipa mishahara mikubwa ya wachezaji
wao.
Jiulize Yanga na Simba, zingeishi vipi
kama kungekuwa na adhabu ya mashabiki kutoingia viwanjani? Wakati ni huu,
lazima kuwe na mabadiliko na mwendo wa fikra endelevu badala ya kuamini
mafanikio ya klabu ni timu kushinda pekee.
Jitanueni kiakili na mnapojifunza,
lifanyieni kazi. Simba na Yanga, kuendelea kubaki mlipo ni sawa na mtu mzima au
mzee anayelazimisha kupaka rangi nyeusi kwenye ndevu zake nyeupe ili aendelee
kuonekana kijana, kumbe umri umeenda.
0 COMMENTS:
Post a Comment