MCHEZO wa
soka hapa nchini umetawaliwa na vituko vingi zaidi kwa viongozi kuliko hata
vile vinavyotokea uwanjani.
Wataalamu
wa soka wanasema hivi, soka linapokuwa burudani zaidi uwanjani, ndiyo muonekano
sahihi kwamba limekua. Lakini kama migogoro baina ya viongozi na wanachama
ikitawala, basi ujue kuna walakini.
Coastal
Union ni moja ya klabu kongwe nchini, asili yake ni mkoa wa Tanga na imefanya
vizuri sana katika miaka ya 1980 na hata 1990 kabla ya kuanza kuyumba.
Mkoa wa
Tanga una watu wa mpira, ni kati ya mikoa ambayo watu wake wana mapenzi ya juu
na mchezo huo wa soka hata kama timu zao hazipo ligi kuu.
Safari hii
wana timu mbili, Coastal Union na Mgambo Shooting na timu zinazosafiri kwenda
kucheza kwenye Uwanja wa Mkwakwani zinajua namna timu hizo ambavyo zimekuwa na
ushindani wa hali ya juu.
Tokea
Coastal Union imerejea Ligi Kuu Bara, kwa kiasi kikubwa imeongeza changamoto kwenye
ushindani wa ligi hiyo ingawa msimu huu imeonekana kuyumba kwa kiasi kikubwa.
Inawezekana ni suala la kusubiri kujipanga.
Lakini kuna
jambo moja ambalo limekuwa ni la kushangaza zaidi baada ya wanachama kadhaa wa
Coastal Union kusumbuka kwa zaidi ya miezi mitatu wakisaka uanachama katika
klabu hiyo bila ya mafanikio.
Wanachama
hao, wameamua kuandika barua kuipeleka hadi kwa Shirikisho la Soka Tanzania
wakidai kwamba wamekuwa wakiomba kupewa uanachama wa Coastal Union lakini
juhudi zao zinagonga mwamba na wamemtuhumu Katibu Mkuu wa Coastal Union, Kassim
El Siagi, kuwa anawakwamisha.
Wanachama
hao wakiongozwa na kiongozi wao, Abdulatif Famau, wamelalamika kwamba kumekuwa
na hali ya kuzungushwa kupata uanachama, tena imefikia hatua katibu huyo wa
Coastal akiwaambia lazima wajaze fomu na majina yao yajadiliwe kwenye mkutano
wa wanachama ili kuwapa nafasi, kichekesho!
Kwa mujibu
wa Famau, amesema wamewahi hadi kufika nyumbani kwa katibu huyo na kumuachia
maagizo mkewe kwamba wanataka uanachama na wamekuwa wakifanya hivyo bila ya
mafanikio na waliamua kwenda nyumbani kwa katibu huyo kwa kuwa imekuwa ni
vigumu kumpata akiwa ofisini.
Kinachoshangaza,
timu kama Manchester United, Real Madrid, Barcelona, Arsenal, Chelsea na
nyingine zinaendelea kusaka wanachama duniani kote. Vipi Coastal Union inaweza
kuweka kauzibe kupokea wanachama wapya?
Uchunguzi
niliofanya nikagundua kuwa, wanakataa wanachama wapya kwa kuwa uongozi wa
Coastal Union una taarifa kwamba kuna watu wanataka kuwa wanachama eti ili
waufanyie vurugu uongozi. Hiki ni kichekesho kingine.
Coastal
Union inaendeshwa kwa mujibu wa katiba, kama kuna watu watakuwa wanaingia
wafanye vurugu ni rahisi kuwathibiti kwa kufuata kanuni, lakini si kuwazuia eti
watafanya vurugu, nani ana uhakika na hilo?
Binafsi
naona ni tabia ya viongozi waoga na wale wa kizamani ndiyo watakuwa wanahofia
changamoto kutoka kwa watu wengine na hasa vijana ndiyo maana Al Siagi na
wenzake wanajaribu kupiga chenga kuwapa uanachama vijana ambao wanaamini
watahoji mambo kadhaa.
Kuna kila
sababu ya kubadilika, kujifunza na kujiamini kwa viongozi hao wa Coastal Union
na wakiwa bora basi ni lazima wazikubali changamoto kwa kuwa kila wanachama
wanavyoongezeka, maana yake Coastal Union ina nafasi ya kupiga hatua zaidi.
Inapendeza
Coastal Union ikiwa na wanachama nchi nzima na baada ya hapo iendelee kujitanua
hadi nje ya nchi. Lakini kama leo uongozi utaanza kuhofia kuchukua wanachama
wapya tena wanaotokea mkoani Tanga, hiki ni kichekesho cha juu zaidi na lazima
kuwe na kipimo sahihi na msisitizo, lazima katiba ifuatwe na ndiyo itakuwa
muongozo na si kuipindisha kwa ajili ya kulinda nafasi zenu hata kama Coastal
inaporomoka eti kisa ni kukwepa changamoto!
FIN.
wewe kaseja tunajua simba damu, tena yanga wala hatukutaki
ReplyDelete