Pointi tatu za mezani ambazo timu ya
soka ya Standa United ya mkoani Shinyanga ilipewa hivi karibuni na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kushinda rufaa yake dhidi ya JKT Kanembwa ya
Kigoma, zimezua balaa mkoani humo baada ya kuifanya Mwadui FC inayofundisha na
Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kukosa na nafasi ya kupanda ligi kuu.
Licha ya kushinda mchezo wake wa mwisho
dhidi ya Polisi Dodoma, Mwadui haijapanda daraja kwa kuwa pointi tatu za mezani
za Stand zinaifanya timu hiyo kufikisha pointi 32, mbele ya Mwadui kwa tofauti
ya pointi moja.
Julio amegeuka mbogo na kutamka wazi
kuwa atahakikisha anapambana mpaka tone la mwisho la damu yake ili Mwadui iweze
kupata haki yake. Julio amedai wameonewa na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) na Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Julio
alisema taratibu ambazo TFF ilizitumia kuipatia pointi tatu Stand United katika
rufaa yake waliyokuwa wamekata dhidi ya JKT Kanembwa si sahihi na zilijaa
ubabaishaji.
“Sikubaliani kabisa na maamuzi hayo
ambayo yamelenga kutunyima haki yetu, haiwezekani TFF wakatoa maamuzi hayo bila
ya kusikiliza pende zote mbili, lakini pia majibu ya rufaa hiyo wakayatangaza
saa chache kabla ya mechi zetu za mwisho kuanza.
“Hakika TFF hivi sasa kumejaa
ubabaishaji ambao unanifanya nimkumbuke Sunday Kayuni, kwani kuna siku Katibu Mkuu
wa Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga, alinipigia simu akiwa na Jamal Malinzi
(Rais wa TFF).
“Akaniambia kuwa nisijisumbue kwani timu
yangu haiwezi kupanda daraja kwa sababu yeye amekuja Dar es Salaam kuchukua
ponti tatu za Stand United ambazo waliwakatia rufaa JKT Kanembwa zitakazotunyima
ushindi,” alisema Julio.
Alisema kutoka na hali hiyo, kwa sasa
TFF kumejaa ubabaishaji tofauti na zamani ambapo alidai kuwa watu wengi walikuwa
wakimwona aliyekuwa Mkugenzi wa Ufundi wa shirikisho hilo, Sunday Kayuni kuwa
hafai kwa sababu tu ya kuwa mkali na kukataa mambo ya kibabaishaji lakini kwa
sasa hali ni mbaya.
Katika hatua nyingine, Julio aliongeza
kuwa mpaka sasa yeye anajua kuwa timu yake ya Mwadui ndiyo iliyopanda daraja na
siyo Stand United, hivyo atafanya usajili kwa ajili ya michuano ya ligi kuu
msimu ujao kama kawaida na TFF wakae wakilijua hilo.
Kabla ya mechi za juzi Jumamosi, Mwadui
ilikuwa na pointi 28 na Stand United 26 lakini baada ya timu hizo kushinda,
Mwadui ilifikisha ponti 31 na Stand United 29, lakini ushindi wa mezani
unaifanya Stand iwe na 32.
0 COMMENTS:
Post a Comment