April 30, 2014


JINA ni Adam David Lallana, kiungo wa Southampton ambaye sasa ndiye gumzo kubwa la usajili wakati huu ambapo Ligi Kuu England inaendea ukingoni.


Lallana ni kati ya viungo gumzo kwa kipindi hiki na huenda ndiye anayetakiwa na timu nyingi zaidi ambazo zinataka kujiimarisha zaidi.

Manchester United ndiyo imekuwa ya kwanza kuonyesha nia yake ya kumkamata Lallana, lakini Liverpool ambayo inapambana kubeba ubingwa wake wa kwanza baada ya kuukosa kwa zaidi ya miaka 20, nayo imeingia vitani.

Kila mmoja anamtaka Lallana ambaye ni kati ya wachezaji walio katika kikosi cha England kitakachocheza Kombe la Dunia nchini Brazil, kuanzia Juni mwaka huu.

Lallana ni gumzo kutokana na aina yake ya uchezaji, uwezo wa kutengeneza nafasi, kumiliki mpira lakini ana ubunifu wa hali ya juu.
Si kazi kubwa kwake kuwatoka mabeki wawili, watatu au kupiga pasi za chini na juu zinazoweza kuwapita watu watatu au wanne na kumfikia aliyemkusudia.

Lallana ameweka rekodi kadhaa, lakini inayovutia zaidi kwa msimu huu ni kupangwa katika mechi 36 na kati ya hizo 35 zote alianza katika kikosi cha kwanza na moja tu ndiyo aliingia baadaye.

Maana yake ni tegemeo na anakubalika na takwimu zake za msimu zinazidi kumbeba kwani katika mechi 36 alizocheza amefunga mabao tisa na kutengeneza sita huku akiwa amepiga mashuti ya uhakika 66.

Waingereza hawachezi mpira wa kuremba, wao wanamfananisha Lallana na Xavi au Iniesta wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, lakini huyu ana nguvu zaidi ndiyo maana analiweza soka la Kiingereza.

Lallana hana sababu ya kubaki Southampton safari hii na Mkenya, Victor Wanyama anayekipiga naye timu moja amesema kuwa itakuwa vigumu kubaki na timu hiyo kwa kuwa ni lulu.
Zaidi wengi wamekuwa wakisema ataangukia Manchester United ambayo imekuwa ya kwanza kutia nguvu za kumnasa kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake.

Kuna ule msemo wa kisoka au mtaani, kitu nyingine. Sawa na kusema mtu mwingine ambaye uwezo wake ni wa hali ya juu. Sasa ndivyo ilivyo kwa Adam David Lallana ni kitu nyingine.

Takwimu Premier League 2013/14:
MECHI    MABAO   ASISTI   MASHUTI
  36                   9             6            66



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic