April 21, 2014




Na Saleh Ally
KAULI ya Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho kumpongeza mwamuzi Mike Dean haikuwa na maana hiyo, badala yake ilionyesha uchungu ulioshindwa kujificha kwenye macho yake na kujitokeza machoni.

Mourinho alikuwa ana hasira kutokana na kupoteza mchezo ambao ulikuwa ni muhimu kwake kupata pointi tatu muhimu katika kupambana kupata ubingwa wa England.
Lakini bado Mourinho alikuwa anataka kuendeleza rekodi yake ya kutofungwa hata mara moja kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, nyumbani kwa Chelsea.
Mourinho katika vipindi viwili ambavyo amekuwa Chelsea, amefanikiwa kuiongoza Chelsea mechi 77 bila ya kupoteza hata moja kwenye uwanja huo. Mechi yake ya kwanza ndani ya Stamford Bridge ikiwa ni Agosti 15, 2004 dhidi ya Manchester United ya Alex Ferguson na kuilamba kwa bao 1-0.
Rekodi hiyo haikuwa ndogo, pia haikuwa rahisi kwa kuwa inahitaji kila aina ya umakini na upambanaji kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri kama yalivyokuwa.
Hivyo, Mourinho aliona kama ameonewa hasa baada ya Dean kutoa mkwaju wa penalti ambayo imevunja rekodi hiyo ya Mourinho kwa kuifunga Chelsea mabao 2-1, licha ya kwamba ndiyo timu inayoburuza mkia wa Premiership na ikiwa na asilimia 94 za kuporomoka hadi daraja la kwanza.
Dean alitoa penalti kwa madai kuwa beki Cesar Azpilicueta wa Chelsea alimuangusha Jozy Altidore wa Sunderland na Fabio Borini akapewa kazi ya kufunga penalti hiyo, kweli akafanya hivyo na mwisho Chelsea ikapoteza.
Marudio kwenye runinga yanaonyesha, Altidore ndiye alikuwa ameukanyaga mguu wa Azpilicueta wakati wakianguka. Hivyo kama ni faulo, beki huyo wa Chelsea ndiye alikuwa ametendewa madhambi.
Chelsea ilionyesha kiwango cha juu, mara mbili ya Sunderland katika mechi hiyo, lakini ikashindwa kufunga. Mwisho penalti ambayo si sahihi imewarudisha nyuma na kuharibu rekodi ya Mourinho kitu ambacho ni sawa na kuibiwa.
Ajabu vyombo vya habari vya Ureno, vimeonyesha kuchukizwa na suala hilo na kuandika waziwazi kuwa “rekodi ya Mourinho imetaifishwa na mwamuzi Mwingereza.”
Mjadala wa Dean umekuwa gumzo kwa kuwa amekuwa akifanya makosa mengi kila anapoichezesha Chelsea na timu nyingine, lakini ukweli unabaki kuwa Chelsea imepoteza na Mourinho amepoteza pia.
Kutokana na Chelsea kupoteza kwa mara ya kwanza Stamford Bridge ikiwa chini ya Mourinho, sasa rekodi inasomeka hivi. Wameshinda mechi 61, wametoka sare 16 na kupoteza moja.
Pamoja na rekodi hiyo ya kutofungwa ya Mourinho kuvunjwa kwa makosa ya mwamuzi huyo, lakini kocha huyo Mreno anazo rekodi lukuki ndani ya Stamford Bridge. Nenda kwa namba.
1 – Sam Allardyce amepoteza mechi moja tu kati ya nne alizowahi kucheza kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, Chelsea ikiwa chini ya Mourinho. (Mechi 3 akiwa kocha wa Bolton Wanderers na moja akiwa na West Ham).
2 – Arsenal na Bolton Wanderers ndiyo timu ambazo zimekuwa zikimsumbua Mourinho kwa kulazimisha sare na kufanya wagawane pointi kwenye uwanja wa nyumbani.
3 –Sare tatu mfululizo alizowahi kuzipata Stamford Bridge licha ya kwamba hakupoteza, lakini aliachia pointi sita, zilikuwa ni dhidi ya Bolton Wanderers, Manchester United na Everton , hiyo ilikuwa ni msimu wa 2006-07.
4 – Liverpool, Newcastle na Portsmouth ndiyo timu pekee ambazo zimepoteza mechi nyingi zaidi ndani ya Stamford Bridge. Kila moja imepigwa mechi nne na Newcastle maarufu kama Magpies, hawajafunga hata bao moja katika mechi hizo.
5 – Bolton Wanderers ndiyo timu iliyokuwa inaisumbua zaidi ngome ya Mourinho ndani ya Stamford Bridge. Kwani imefunga mabao matano katika mechi tatu ilizocheza, maana yake ndiyo iliyofunga mengi zaidi kwenye uwanja huo dhidi ya Chelsea.
13 – Mechi 13 ndiyo rekodi ya Mourinho kushinda mfululizo kwenye Dimba la Stamford Bridge.
39 – Kabla ya kupoteza kwa Sunderland juzi, Chelsea ilikuwa imefungwa mabao 37 ndani ya Stamford Bridge, ukiwa ni wastani wa 0.49. Sasa imefungwa mabao 39.
61 –Kwa asilimia 61, Chelsea imecheza bila ya kufungwa katika mechi zake za Stamford Bridge.
79% – Kwa asilimia 79, Mourinho amefanikiwa kushinda mechi 59 kati ya 76  za Premier League ndani ya Stamford Bridge.
157 – Chini ya Mourinho ndani ya Stamford Bridge, Chelsea imefunga mabao 157 katika Premier League ukiwa ni moja ya wastani bora kabisa wa mabao 2.09 kwa kila mechi.
FIN.
REKODI MSIMU WA 2013-14
CHEZA   SHINDA   SARE    POTEZA 
35            23              6               6 
REKODI YA UKOCHA YA MOURINHO
                                                      M         W     D       L       
Benfica                      (2000- 2000)       11     6       3       2      
UniĆ£o de Leiria            (2001- 2002) 20     9       7       4      
Porto                            (2002-2004)      127 91     21     15    
Chelsea          (2004-2007)         185 124 40     21    
Inter                              (2008-2010)     108 67     26     15    
Real Madrid           (2010-2013)         178 128 28     22    
Chelsea          (2013-Sasa)     52          33     8       11    
                                            JUMLA          681 458 133 90    
*Ufunguo M-Mechi, W-Alizoshinda, D-Sare, L-Alizopoteza
FIN.










0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic