MARA kadhaa
kumekuwa na matatizo makubwa sana kuhusiana na suala la waamuzi wa soka nchini
kuboronga katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara.
Waamuzi hao
wamekuwa wakifanya madudu kila kukicha na kusababisha vurugu kila mara na
baadhi yao wakionyesha waziwazi kwamba wamepania kuisaidia timu fulani.
Kwa kuwa
suala la rushwa ni siri kubwa, kila mmoja anaweza kukanusha na kusema kivyake,
lakini lazima tukubali kwamba kuna hilo tatizo.
Viongozi
wengi wa soka wamekuwa hawapambani na rushwa, sitaki kusema wanahusika pia au
la, lakini ukweli wako wanaoshiriki hata kudhoofisha nguvu ya kupambana na
rushwa.
Lakini
juzi, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, alikiri kwamba
wapo wanaofanya mchezo huo mchafu na kwamba baada ya muda itafikia siku
atamkamata mmoja wao na atakuwa mfano kwa wengine.
Malinzi
ameyasema hayo wakati anafanyiwa mahojiano na kipindi cha michezo cha Radio
One, huku akionyesha kwamba anakerwa na hali hiyo ambayo hakuna ubishi
inazorotesha michezo nchini.
Mara ngapi
kuna wale ambao wanataka hali hiyo kwisha wamekuwa wakipambana lakini badala
yake wanaonekana ni sawa na maadui wakubwa kwa kusema ukweli?
Kitendo cha
Malinzi kusema hadharani na kuonyesha anakerwa na jambo hilo, ndiyo wakati
mzuri na mwafaka wa kuanza kufunga safari ya kupambana nalo na ikiwezekana na
kulimaliza ili matokeo ya ligi kuu na ligi nyingine yawe ni yale yanayopatikana
kwa uwezo na si ujanjaujanja.
Kuna timu
hadi zimeunda vitengo vya fitna, kuna watu wanalipwa fedha ili kuhakikisha
wanawahonga waamuzi ili kufanya mambo yaende vizuri kwao licha ya kuwa wana
wachezaji na makocha wa kimataifa wanaolipwa fedha nyingi.
Waamuzi
wanajua kuwa wao ni tatizo ingawa si wote, wako wanaowajua wenzao kwa majina kwamba
wanashiriki mchezo huo mchafu ambao kadiri siku zinavyosonga, wanataka kuufanya
halali na hauna tatizo.
Lakini kama
Malinzi ambaye ndiye kiongozi wa juu zaidi katika soka ameona upuuzi huo,
uchafu huo, basi kiwe kipindi mwafaka cha kumaliza kila kitu na kukifanya
kiende vizuri, inawezekana na vizuri vita hii ianzie kwa waamuzi wenyewe na
chama chao.
Si waamuzi
wote wanaochukua rushwa, lakini wako wachache wanaoharibu sifa ya waamuzi
wenzao na wao wote kutokana na tabia ya tamaa inayowaongoza. Tunajua huo ni
ugonjwa wa dunia nzima kwa kuwa hata Ulaya, Marekani na kwingineko kuna waamuzi
wenye tabia hizo.
Lakini si
sahihi kuiga mfano mbaya na kuufanya ndiyo mwenendo wa maisha hata kama
tumekuwa tukikopi mengi kutoka kwa wenzetu kutokana na wao kupiga hatua. Badala
yake tuyatumie makosa yao kama sehemu ya kujifunza na kufanya kilicho bora,
maana ifikie siku nao waje waige kwetu, inawezekana.
Hakuna haja
ya woga, kweli kuna waamuzi mnachukua mlungula na mnajuana. Wenyewe pia mnajua
tamaa zenu zinavyoathiri mpira wa Tanzania ambao kila siku haukui.
Hata kama
kuna makosa ya viongozi au uzembe wa wachezaji, lakini waamuzi ni sehemu kubwa
ya kuzorotesha mchezo wa soka na mmegeuza rushwa ni haki yenu kwa kuwa tu ni
vigumu kuwa na ushahidi mnavyochukua kwa vile wanaotoa pia wanaficha siri.
Bosi wenu
sasa anajua, huenda tamaa inazidi kuwaongoza. Lakini kama imefikia hadi
anayewaongoza amekubali, basi kidogo anzeni kuona hata aibu ili muusaidie mpira
wa Tanzania.
0 COMMENTS:
Post a Comment