Na Saleh Ally
USAJILI wa kiungo kinda Frank Domayo kutoka Yanga kwenda kujiunga na
mabingwa wapya wa Tanzania Bara, Azam FC, ndiyo gumzo katika soka la nyumbani.
Uamuzi wake wa kusajiliwa Azam FC, unaweza ukawa umewaudhi wengi kwa
maana ya mapenzi ya kibinadamu, lakini hakuna ubishi kuna mambo kadhaa ambayo
ni muhimu yanaweza kujadiliwa.
Mashabiki wa Yanga hawawezi kufurahia hata kidogo, huenda wanaweza kutupa
lawama kwa viongozi ambao hata hivyo nao wameelezea suala hilo kwa kusema
waliwasiliana na Domayo mara kadhaa ili kujadili mkataba wake lakini
akawazungusha.
Viongozi wa Yanga wameeleza walivyofanya juhudi kumpata Domayo ambaye
aliendelea kusisitiza kwamba wangejadili baadaye suala hilo hadi waliposikia
ametua Azam FC, juzi usiku.
Kwa fedha Sh milioni 70 na mshahara wa Sh milioni 3 kwa mwezi, Domayo ana
haki ya kuona kwake ulikuwa ni wakati mwafaka wa kuhama kwa maana ya maslahi.
Hakuna njia ya Yanga kumrudisha Domayo sasa, kikubwa ni kukubali kilichotokea.
Lakini kwa Domayo mwenyewe kuna mambo kadhaa ambayo tunaweza kuangalia kwa
lengo la kujifunza tu.
Fedha ni kitu muhimu lakini hesabu za maisha zinaweza kuwa ndiyo bora
zaidi kwa kuwa kuna wachezaji wengi wamewahi kuhama kwa mamilioni ya fedha kutoka
sehemu moja kwenda nyingine na hii si hapa nyumbani tu.
Angalia Marouane Fellaini ambaye ametua Manchester United akitokea
Everton anaonekana hana lolote katika kipindi hiki. Wapo ambao wamesahau kuwa
ni mchezaji mzuri na mwenye uwezo mkubwa.
Ukirudi kwa Samir Nasri aliyekuwa na Arsenal halafu angalia huyu wa sasa
ambaye anakipiga na Manchester City, lazima utaona kuna kitu ambacho ni tofauti
kabisa au unaweza ukafanya tathmini ya Juan Mata wa Chelsea na Man United au
ilivyokuwa sasa kwa Fernando Torres.
Kusema Fellaini si mchezaji mzuri itakuwa kichekesho, kocha aliyekuwa
naye ni yule aliyetoka naye Everton, jiulize tatizo ni nini? Tofauti ya Man
United na Everton inaweza kuwa na ile ya Yanga na Azam FC kwa kuwa ni timu
lakini zenye mfumo tofauti wa malezi na maisha ya ujumla.
Hawa wachache wanaweza kuwa ni mfano tu, lakini kuna wengine wale
waliohama kutoka timu moja kwenda nyingine wakiwa nyota lakini kule walipohamia
kwa kitita kikubwa wakakwama kabisa na mambo yakawa magumu.
Hakuna sababu ya kusema lengo la makala haya ni kumkatisha tamaa Domayo
kwamba uamuzi wa kujiunga na Azam FC haukuwa ni sahihi. Ni wake na
unaheshimika, lakini kujifunza ni jambo jema.
Kwamba je, Domayo ameiva vilivyo kwa sasa na Azam FC inaweza ikamuamini
kwa asilimia mia naye akafanya kama inavyotakiwa hadi kufikia kujitengenezea
nafasi au namba ya uhakika?
Kwa tathmini za msimu uliopita, Domayo ndiye alikuwa amepanda na huenda
Azam FC waliliangalia hilo kwamba kwa msimu ujao kuna nafasi kubwa kwake
kufanya vema zaidi.
Lakini katika soka mambo hubadilika, Domayo atakutana na ushindani mkubwa
zaidi wa namba kuliko ule wa awali kwa vile Azam ina viungo wengi zaidi kama
Jabir Aziz ‘Stima’, Himid Mao, Kipre Balou, Ibrahim Mwaipopo na wengine.
Hivyo kwake kutakuwa na mabadiliko makubwa na kinachotakiwa kwa Domayo ni
kujiandaa katika mambo mengi sana lakini muhimu ni makundi mawili.
Kwanza kisaikolojia kwamba hatakuwa Yanga na alipo sasa ni Azam FC ambayo
ushindani wake wa namba utakuwa ni mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa Jangwani.
Maana yake hata maandalizi atakayofanya lazima yaendane na suala la alipo na si
alipotoka.
Lakini suala la pili ni kuangalia suala la kujiamini na uwezo wa
atakachokifanya atakapokuwa Azam FC ambayo ushindani wake ni mkubwa zaidi,
aamini zaidi kwenye ushindani wa uwanjani. Hivyo lazima kuwe na maandalizi
maradufu kwake binafsi.
Vingine kwake vinabaki ni vitu vya kibinadamu ambavyo vitawagusa karibu
watu wote wakiwemo mashabiki kuwa, Domayo bado anapaswa kuiaga Yanga katika mtindo
mzuri na hasa viongozi ambao wanaweza kuwa kwa niaba ya wanachama na mashabiki.
Yanga ndiyo ilimuamini, ikaenda kumnunua katika kituo kilichomlea kisoka
na baada ya hapo ikampa nafasi ya kuonekana ndiyo maana Azam FC ikamuona na
kuwa tayari kutoa dau kubwa. Zaidi ya hapo, maisha yaendelee na kila la kheri
kwake.
FIN.
0 COMMENTS:
Post a Comment