May 2, 2014





Na Saleh Ally
BAO la 15 la Cristiano Ronaldo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu alilolifunga wakati Real Madrid ikiivaa Bayern Munich, Jumanne lina mambo mengi sana ya kuelezea.
Ilikuwa ni katika mechi ya pili kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bayern Munich wakiwa nyumbani lakini Madrid wakawaadhibu kwa kuwachapa kwa mabao 4-0 na kusonga hatua ya fainali.
Bao hilo lilikuwa ni la 15 kwa Ronaldo ambalo limemfanya aweke rekodi mpya ya kufunga mabao zaidi ya 14 katika msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, rekodi mpya.
Wakali wa kupachika mabao ambao wamefunga mengi wamekuwa wakiishia mabao 14, mmoja wao akiwa ni Lionel Messi wa Barcelona lakini Ronaldo akaanzisha rekodi mpya katika kizazi cha sasa.

Wakati anafunga bao hilo na kuweka rekodi mpya ambayo aliishindilia na bao jingine la 16 alilofunga kwa mkwaju wa adhabu, bao la 15 ndiyo chanzo cha yote yaliyotokea.
Bao hilo pamoja na kuweka rekodi, lakini ndiyo bao ghali zaidi la soka kuwahi kutokea kutokana na pasi zake mbili za mwisho kabla ya mfungaji wa bao lenyewe.
Real Madrid walikuwa wanashambuliwa na baada ya mpira kuokolewa na kumfikia Karim Benzema, alikimbia nao kumpasia Gareth Bale ambaye alikimbia nao kwa kasi kubwa kabla ya kumpa Ronaldo aliyemaliza kazi hiyo.
Walioshirikiana kutengeneza hadi kufunga bao hilo ni kati ya wachezaji ghali duniani, Benzema ambaye alinunuliwa kwa pauni milioni 35 (zaidi ya Sh bilioni 87.5) akitokea Lyon ya Ufaransa kujiunga na Real Madrid, akampasia Bale.
Bale ambaye ndiye mchezaji ghali zaidi duniani kutokana na kununuliwa kwa pauni milioni 86 (zaidi ya Sh bilioni 215) akitokea Tottenham Hotspur ya England na kujiunga na Real Madrid, naye akakimbia nao na kumpasia Ronaldo aliyefunga kwa utulivu mkubwa.
Mfungaji, yaani Ronaldo, anashikilia nafasi ya pili kwa bei ya juu ya uhamisho, kwani Madrid ilimnunua kwa kitita cha pauni milioni 80 (Sh Sh bilioni 200) akitokea Manchester United.

Ukipiga hesabu za gharama za walioshirikiana katika pasi mbili za mwisho na mfungaji, utaona ni pauni milioni 199 (zaidi ya Sh bilioni 497.5), hivyo kulifanya bao hilo kuwa ghali zaidi kuliko jingine lolote lililowahi kufungwa hapo kabla, kwa maana ya wachezaji gani walishiriki katika pasi hizo mbili za mwisho.
Hivyo ni bao lililozaa rekodi mpya kwa wafungaji likiwa ni la 15 kwa Ronaldo lakini ni lile lililosukwa na wachezaji wenye thamani kubwa duniani, hivyo kulifanya kuwa ghali zaidi kuwahi kufungwa.

WACHEZAJI 10 GHALI ZAIDI DUNIANI:
Bale                              pauni 86m (kutoka Spurs - Madrid)
Ronaldo            pauni 80m (Kutoka Man Utd - Madrid)
Ibrahimovic     pauni 59m (kutoka Inter-Barcelona)
Kaka                             pauni 56m (kutoka AC Milan - Madrid)
Cavani               pauni 55m (kutoka Napoli - PSG)
Falcao                pauni 51m (kutoka A.Madrid - Monaco)
Torres                pauni 50m (kutoka Liverpool - Chelsea)
Neymar             pauni 48.6m (kutoka Santos - Barcelona)
Zidane               pauni 46m (kutoka Juve - Madrid)
Rodrigues         pauni 38.5m (kutoka FC Porto-Monaco)


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic