Na Saleh Ally
BEKI na kocha wa zamani
wa Simba, Talib Hilal amesema huu ndiyo wakati mwafaka kwa wanachama kufanya mabadiliko
katika klabu yao kwa kuwa makini kupita kiasi.
Uchaguzi wa Simba
utakaohitimisha uongozi wa miaka minne wa Ismail Aden Rage, umepangwa kufanyika
Juni 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Hilal ambaye aliichezea
Simba kwa mafanikio kabla ya kuhamia nchini Oman, ameliambia Championi Ijumaa
kuwa, wanachama wa Simba ndiyo wenye uamuzi wa kuipa timu hiyo ahueni au mateso
ya miaka minne mingine kama ilivyokuwa katika uongozi uliopita.
Katika mahojiano na
gazeti hili kutoka Sharm El Sheikh nchini Misri, Hilal amesema, mateso yaliyotokana
na Simba kutokuwa na viongozi imara yalikuwa ni funzo tosha kwa kipindi hicho
cha miaka minne.
Kwa sasa Hilal ni
kocha wa timu ya soka ya taifa ya Oman ya ufukweni na yupo nchini Misri ambako kuna
michuano ya kimataifa kwa nchi za Kiarabu.
Hilal amesema atashangazwa
kama Wanasimba kwa mara nyingine watachagua viongozi wasio bora, hasa wale
ambao wana maneno mengi wakati wa kampeni, hasa maneno yanayoashiria kuwa hawana
nia njema na klabu hiyo.
Championi: Unafikiri
Simba wanatakiwa kuchagua kiongozi wa aina gani?
Hilal: Lazima awe
mkweli, asiye na siasa na maneno mengi. Simba imeathirika kwa kipindi cha miaka
minne kutokana na watu wenye maneno badala ya vitendo.
Championi: Unaweza
kufafanua maneno bila ya vitendo?
Hilal: Ndiyo,
viongozi waliokuwepo walikuwa wanasema maneno mengi sana bila ya utekelezaji. Hakuna
mafanikio kwenye maneno mengi, lazima vitendo vitangulie ndiyo maana naonya kuwa
wawe makini.
Championi: Unasema
hivyo, labda umeishaona viongozi wenye maneno mengi kati ya wagombea?
Hilal: Kwenye uchaguzi
karibu wa kila sehemu, watu wa namna hiyo hawakosekani na wanachama wanalijua hilo
kwa kuwa ni wazuri kutoa maneno matamu wakati utekelezaji wao unakuwa chini sana.
Championi: Lakini
ni vigumu kujua kama kweli maneno hayo ni ya kampeni tu, wanaweza kuwa na maneno
matamu ndiyo maana wanachama wanashawishika.
Hilal: Kwa wanachama
wa Simba hakuna wasiyemjua, hasa kuhusiana na uongozi. Ukiangalia asilimia 90
ya wale wanaogombea nafasi ya rais na makamu wake, wameishaongoza Simba hata iwe
ni kamati ya usajili, hivyo wanachama wanajua nani ana maneno, nani mtendaji na
yupi ni kiongozi sahihi kumchagua ili awasaidie.
Championi: Kwa maana
hiyo, unaamini uhai wa Simba uko mikononi mwao (wanachama)?
Hilal: Hakika ni hivyo,
wakiwa makini hawatajuta kwa miaka yote minne na watakuwa tayari kusaidiana na uongozi
wao kuhakikisha Simba inarudi kwenye heshima yake.
Lakini wakivuruga
wakati wa uchaguzi kwa papara zao, basi ndiyo mwisho wanaanza kuulaumu uongozi kuwa
hauko makini na vurugu zinaanza, kumbe chanzo ni wanachama.
Championi: Huenda
hilo linachangiwa na wanachama ambao ni bendera fuata upepo, ili mradi tu wakiambiwa
ndiyo wanafuata bila ya kutafakari?
Hilal: Sidhani kama
ni fuata upepo, lakini wanaweza kuwa hawatafakari vizuri wanachokifanya, wanatakiwa
kuwa makini na kuamini Simba inaumia kutokana na wao kutokuwa makini au
kuchagua kwa kumridhisha fulani halafu wao wanaumia kwa miaka minne baadaye.
Hilal aliiongoza Simba
kutwaa ubingwa wa Ligi Ndogo Bara iliyopigwa kwa mtoano mwaka 2008 na katika fainali,
alikiongoza kikosi chake kukifunga cha Yanga chini ya Sredojevic Milutin
‘Micho’ mjini Morogoro na kutwaa ubingwa.
Siku ya mechi hiyo,
akiwa njiani kwenda Morogoro, Hilal alipata ajali mbaya ya gari na huku gari likiwa
nyang’anyang’a, Mungu akamsaidia akatoka salama na kwenda uwanjani kuiongoza Simba
kubeba ubingwa huo.
Lakini kabla ya hapo,
Hilal, aliiongoza kambi ya Simba jijini Muscat, Oman kabla ya kushirikiana na
James Aggrey Siang’a na benchi lake la ufundi kuivua ubingwa wa Afrika timu bora
barani humu wakati huo, Zamalek, tena kwao jijini Cairo.
0 COMMENTS:
Post a Comment