Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema alifanya kila juhudi za kumuokoa Frank Domayo asijiunge na Azam FC.
Cannavaro amesema alifikia kujaribu kuzungumza naye katika dakika 15 za mwisho kabla ya kusaini lakini ikashindikana.
“Mwanzo nilizungumza naye na kumuambia viongozi Yanga wamekuwa wakimpigia simu na hapokei, akasema atapokea, hakufanya hivyo.
“Lakini hakufanya na nilipojua anakaribia kusaini kama dakika 15 za mwisho nilimfuata na kumshauri asisaini kabla ya kuzungumza na viongozi, lakini akakataa na kusema anataka kucheza Azam, niwaambie hivyo viongozi.
“Sikuwa na ujanja, lakini nikuambie, viongozi wamejitahidi sana kumueleza Domayo kuwa wanataka kumpa mkataba, nafikiri miezi mitatu minne iliyopita.
“Lakini alikuwa anakataa na hata kuna wachezaji walisaini mkataba lakini Domayo aliendelea kukataa na wao walimsubiri. Sasa sidhani kama viongozi wanaweza kulaumiwa.
“Domayo ameenda kutafuta maisha, nafikiri Wanayanga wakubali na baada ya hapo wawaunge mkono viongozi kwa ajili ya kutafuta wachezaji wengine wazuri.
“kama Yanga tutaanza kulumbana kwa mchezaji aliyeondoka, itakuwa matatizo kwetu na wenzetu wanajipanga,” alisema Cannavaro.
Domayo ametua Azam FC na mkataba wake amesaini wakati akiwa kambini kwenye timu ya taifa mjini Tukuyu Mbeya.
0 COMMENTS:
Post a Comment