June 4, 2014


MANJI (KATIKATI) AKITETA JAMBO NA WAJUMBE WA BARAZA LA WADHAMINI LA YANGA, MZEE  KATUNDU NA MAMA KARUME.

Wanachama wachache wanaopinga Yusuf Manji kuongezewa muda wa kuendelea na kazi kwa mwaka mmoja, wameambiwa wajitokeze klabu.


Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto amezungumza na SALEHJEMBE na kusema kuna kundi dogo la wanachama wasiopungua kumi wamekuwa wakipinga uamuzi wa wanachama walioamua kuungezea muda uongozi wa Yanga.
“Yalikuwa na maamuzi ya wanachama zaidi ya 4,000 lakini kama wako wanapinga, wajitokeze na kuorodhesha majina, halafu demokrasia itachukua mkondo wake.
“Hivyo wafike pale klabuni, wajiandikishe majina yao kwa katibu,” alisema Kizuguto.

Wanachama zaidi ya 4,000 wakiwemo wajumbe wa bodi ya wadhamini ndiyo waliomuomba Manji aongezewe miaka minne, lakini yeye akaomba angalau mmoja.

Soma wakala:


KUNA rekodi nyingi sana zinawekwa katika mchezo wa soka duniani kote, lakini safari hii kumekuwa na rekodi mpya kwenye mchezo wa soka nchini.
Wanachama wa Yanga kwa pamoja, bila ya kusita wala kulazimishwa kwa umoja wao wameamua kumuongezea muda mwenyekiti wao pamoja na timu yake, aongoze kwa miaka zaidi.
Wanachama hao waliokutana Jumapili iliyopita kwa ajili ya marekebisho ya katiba kama ambavyo walivyokuwa wameagizwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wao wakaingia kwenye ajenda nyingine kabisa.

Ajenda hiyo ya kumuongeza Manji miaka, wakasema kwa umoja kuwa wanamuongezea miaka nane, yaani akae madarakani kwa kipindi chote hicho na baada ya hapo, uchaguzi mkuu ungefanyika.

Maombi ya wanachama wa Yanga, yalipitia kwa Mama Karume ambaye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyoi. Kwa mujibu wa katiba ya Yanga, Mama Karume ni mmiliki wa klabu hiyo.
Kama Mama Karume ndiye mmoja wa wamiliki wa klabu, kwa kushirikiana na wanachama ambao ndiyo wenye klabu kwa pamoja bila ya pingamizi wakaamua kumuongezea miaka hiyo minane.

Manji mwisho alitoka nje na kushauriana na makamu wake, Clement Sanga kabla ya kurejea na kuomba aongezwe mwaka mmoja tu badala yam inane kama walivyotaka wamiliki kama Mzee Katundu, Mama Karume na wanachama wote wa Yanga.
Namna gani ni kitu cha kuvutia kwenye soka, wanachama wa klabu wanafikia kumuamini kiongozi wao kwa kiasi kikubwa namna hiyo. Wanaona wako tayari hata kumpa dhamana ya kuongoza miaka nanen baadaye.

Imani gani ya juu kiasi ya hiyo iliyowahi kutokea kwa Manji imewahi kutokea kwa mwanamichezo mwingine hapa nchini na hasa viongozi? Lakini nani kawahi kusikia kiongozi wa soka kwa Afrika Mashariki na Kati amewahi kuaminiwa kiasi hicho?
Manji si mchawi, wanachama na wamiliki wa Yanga si watu wasiojua wanalolifanya lakini wanaona na wanatambua kuwa Manji ni kiongozi sahihi, mchapakazi, anayefanya kazi kwa maslahi ya klabu na si maslahi yake binafsi.

Kama imani ya wanachama wa Yanga kwa kiongozi mmoja, basi imekuwa juu kupita iliyowahi kutokea kwa kiongozi mwingine yoyote aliyewahi kutokea katika klabu hiyo tokea kuanzishwa kwake.

Wako watakaokerwa na rekodi au sifa aliyopata Manji, wako watakaopandikiza na kusema imetengenezwa au vinginevyo lakini vizuri kuamini wanachama wa Yanga na wamiliki wao ni watu wanaojitambua.

Wana hamu ya maendeleo, wanataka mabadiliko na ndiyo maana wanakuwa tayari kumkabidhi kila kitu mtu ambaye wanaamini ana uwezo wa kufanya hivyo na sasa hawana mwingine zaidi ya Manji.
Manji anaweza kuwa mfano si Yanga tu, Simba na klabu nyingine zinazomilikiwa na wanachama kwamba viongozi na hasa wale wa juu, wanapaswa kuaminiwa na wanachama kutokana na utendaji wao bora.

Historia inaonyesha Manji alianza kuingoza kampuni kubwa ya Quality Group akiwa na umri wa miaka 20 tu. Leo ana miaka 48, amefanya kazi ya kuwa bosi wa juu kwenye kampuni kubwa kama hiyo yenye utajili wa zaidi ya dola milioni 700, sasa ni miaka 28.

Inamjengea hali ya kujiamini, utamaduni wa kutaka mafanikio kwa ajili ya anachokiongoza na watu wake na si mafanikio, tumbo lake au maendeleo yake binafsi, ndiyo maana ameweka rekodi hiyo kubwa ya uaminifu katika michezo nchini kuliko aliyowahi kuipata yoyote yule.
Viongozi wa Yanga waliopita, hali kadhalika Simba na kwingine ambako kunayumba kama Coastal Union, wakipenda wanaweza kujifunza. Kama watakuwa hawataki, waachane naye na kuendelea kuboronga.
Yanga ina nafasi kubwa ya kupiga hatua kwa kuwa sasa kuna muungano wa karibu na mapenzi ya pamoja kati ya wamiliki, mwenyekiti na wanachama ambao ndiyo wanaounda klabu ya Yanga.
Sasa Yanga itafeli vipi kama watu wote wanaaminiana kiasi hicho na kupendana kwa dhati. Kinachofuatia hata kama watateleza ni lahisi kuambiana na kurekebisha mambo halafu wakasonga mbele.
Uaminifu walioonyesha wanachama kwa Manji, ni fundisho lakini dawa mpya kwenye soka nchini. Viongozi kama yeye wanahitaji, watu wasihofie kusema kwa kuwa wataonekana wanajipendekeza.
Kama Manji angekosea, wanachama wangeonyesha kutokuwa na imani naye, haraka hili lingejadiliwa. Lakini kwa kuwa ameaminika, basi iendelee kuelezwa na viongozi wakongwe zaidi yake warudi nyuma kujifunza na wale chipukizi waamini wanaweza kufanya kazi zao kwa ubora kama wake na kuleta maendeleo.
Hakuna taasisi au klabu imewahi kuendelea wakati kiongozi wake ni mroho wa madaraka na aliyepania kujiendeleza yeye. Tuna mifano kwenye taasisi za michezo na klabu mbalimbali zikiwemo kubwa kama Simba na Yanga. Sasa rudini shule kwa somo la Manji, soka la Tanzania, linahitaji watu kama yeye.

.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic