July 23, 2014




ASILIA yake ni Afrika katika nchi ya Senegal, lakini amekuwa akiichezea timu ya taifa ya Ufaransa ambayo ameicheza mechi 61 kwa miaka 10, sasa.


Ingawa amekuwa akitoka na kurejea, Evra ni kati ya wachezaji wachache ambao wameweza kudumu katika kikosi cha timu ya taifa kwa miaka 10.

Mara ya mwisho aliichezea Ufaransa kwenye Kombe la Dunia, wiki chache zilizopita nchini Brazil na kufanikiwa kuvuka hadi hatua ya robo fainali ambapo timu yake iling’olewa na Ujerumani ambao ndiyo walitwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Ukirudi upande wa klabu, Evra amekichezea kikosi cha Manchester United tokea mwaka 2006, kabla ya kuamua kufunga safari na kwenda Juventus akiamini wakati umefika hasa baada ya United kumsajili Luke Shaw.

Shaw lazima acheze, umri wa miaka 33, unatosha kwake, miaka nane ya kuichezea Man United inatosha, amehamia Juventus ambayo si timu lelemama pia, hii inaonyesha yuko fiti kuendeleza soka la ushindani.

Juventus ambayo rasmi imemtwaa Julai 21, mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili na ada ya pauni milioni 1.2 ambayo itafikia milioni 1.5 kama itafanikiwa kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, imepata mtu.

Pamoja na kwamba umri umekwenda, lakini rekodi zake Manchester United, zinaonyesha ni kati ya mabeki bora, kati ya wachezaji wa kiwango cha juu ambao United imewahi kuwa nao.

Ilikuwa ni nadra kwake kuumia, ndiye kati ya wachezaji watano wa juu ambao Kocha Alex Ferguson, hakuwahi kufikiria kuwabadilisha wakati kikosi chake kinacheza.

Pia ndiyo mmoja wa wachezaji wachache wa Manchester United, ambao walikuwa fiti kwa asilimia mia katika mechi zote 38 za ligi katika misimu hadi mitatu.

Ameacha rekodi nyingi ambazo zinaweza kuwasaidia wachezaji wengi, wakiwemo wale wanaocheza namba tatu kama yeye, lakini hata wale wanaocheza namba nyingine.

Moja ya sifa zake ni kutokuwa na ‘mambo mengi’ kama vile starehe za klabu, wanawake wengi, sigara na kutopumzika.

Akiwa Monaco, licha ya kuwa na miaka 24, lakini wachezaji wenzake walimbandika jina la ‘Babu’, maana hakuwa akiongozana nao klabu wala sehemu nyingine za starehe na alipumzika mwishoni mwa msimu.

Hicho ndiyo kilikuwa chanzo cha yeye kuanza kufanikiwa na kufikia kuwa mmoja wa mabeki bora zaidi wa kushoto duniani na ana uhakika wa kuendelea kutamba akiwa Juventus.

Anaweza kuwa na mambo mengi sana ambayo yatawasaidia wachezaji hapa nyumbani na duniani kote kama watataka kujifunza kupitia yeye.

Si rahisi kutaja kila kitu, lakini hizi tano zinaweza kudhihirisha ubora aliokuwa nao.


1. Akiwa na Man United
Alicheza mechi 273 za Premier.
Akashinda 186.
Sare 43.
Alipoteza 44.

 2. Msimu uliopita, Evra alicheza mechi 10 ambazo United walipoteza msimu uliopita na ndiyo nyingi zaidi kuitumikia klabu hiyo kwa msimu na ikapoteza.

Mfano kwa msimu wa 2011-12 na 2012-13, yote miwili, Man United, ilipoteza mechi 10.

3. Evra ndiye alikuwa mchezaji aliyelala na kuokoa mipira mingi kuliko mwingine msimu uliopita. Alifanikiwa kuokoa hatari 54 kwa njia ya ‘takolin’.

4. Hadi anaondoka England, ndiye alikuwa mchezaji aliyepiga mipira mingi ya vichwa akiwa katika nafasi ya pili kutokana na mipira 185. Anayeongoza ni Nemanja Vidic aliyepiga 199, ambaye amehamia Inter Milan.

5. Ametwaa makombe & ngao 14:
Makombe 5 ya Premier
Matajii 5 ya Ngao ya Hisani
Makombe 3, Kombe la Ligi
Kombe moja Ligi ya Mabingwa Ulaya.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic