Na Saleh Ally
MIAKA minne iliyopita, wachezaji kutoka
England, Brazil na Italia ndiyo walikuwa na soko kubwa katika soka.
Soka la kimataifa, ngazi ya ligi zenye nguvu
kama Premier League (England), Serie A (Italia), Bundesliga (Ujerumani), La
Liga (Hispania) na League 1 (Ufaransa).
Wachezaji kutoka mataifa hayo walipiga hatua
moja kutoka huku, kwenda upande mwingine na wakaendelea kufanya vizuri.
Pia kulikuwa na kundi la mwisho, hili
lilijumuisha wachezaji kutoka Ulaya Mashariki kama Serbia, Jamhuri ya Czech,
Croatia na kwingine, pia wale waliotokea barani Afrika, hawa walionekana
wachezaji wanaocheza soka kwa ajili ya kulainisha maisha.
Yaani wanatokea kwenye maeneo ambao maisha yako
chini, ilikuwa ni lazima wapambane kupata maisha bora kupitia soka.
Hispania ndiyo walishangaza wengi, bila ya
kujali watapata fedha nyingi au kidogo, waliendelea kubaki kwao Hispania.
Wachezaji wengi wa Hispania, ndoto zao za juu
zilikuwa ni kucheza ligi ya kwao, La Liga, Ligi ya Mabingwa Ulaya au michuano
iliyo chini ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) au lile la kimataifa (Fifa).
Hawakuwa na haja ya kwenda England au Italia,
wengi walibaki nyumbani licha ya kuwa na vipaji vya juu.
Wachache au asilimia ndogo sana ndiyo waliokuwa
tayari kutoka na kwenda kucheza soka kwenye nchi za Ulaya hasa England na
Ujerumani.
Wachezaji kutokea Hispania walionekana
wasingeweza lolote, tena hata kidogo kwa kuwa ni ligi inayojumuisha nguvu na
kasi, vitu ambavyo walionekana, hawana.
Leo mambo yamebadilika, Hispania ni kati ya
mataifa yanayotawala soka Ulaya na duniani kote.
Achana na timu yao kupokonywa Kombe la Dunia,
hiyo haizuii wao kuwa bora lakini wachezaji wao kibao wanang’ara katika ligi
mbalimbali kubwa.
Safari hii wako hadi ndani ya England na utaona
imefikia hadi mchezaji kutoka England kuaminiwa kucheza namba sita kwa mfano
Mikel Arteta aliyefanya vizuri akiwa na Everton na baadaye Arsenal.
Kabla ya hapo, Arsenal ilikuwa na Cesc Fabregas
ambaye sasa anaendelea kufanya vizuri Chelsea. Manchester United imemtwaa
kiungo Ander Herrera na Juan Mata kwa kazi kama hiyo.
Cheki na Santi Cazorla anavyofanya vizuri na
Arsenal, lakini Manchester City wamechukua ubingwa wakiwa na wapishi wawili wa
Kihispania, David Silva na Jesus Navas.
Muangalie kijana aitwaye Suso aliye Liverpool,
ni matata na ana uwezo mkubwa sana.
Hao ni viungo, ukipanda kwa washambuliaji,
Fernando Torres ambaye aliwashangaza wengi akiwa na Liverpool kabla ya kwenda
Chelsea ambako mambo yalikataa, sasa yuko Italia.
Chelsea wamemchukua Diego Costa, anaonekana ni
mtambo, anatishia amani za mabeki, makipa na hata ajira za makocha.
Ukirudi kwa walinzi, wako kama Cesar
Azpilicueta aliye Chelsea, lakini Liverpool nayo imewajaza akina Jose Enrique,
Alberto Moreno na Manquillo.
Kuna wachezaji zaidi ya 33 kutoka Hispania
ambao wanacheza ligi za juu kwenye nchi 13 za Ulaya.
Wengi wao ni tegemeo katika timu wanazozichezea
na wanaanza na nchi karibu zote hodari kwenye mchezo huo kama England, Italia,
Ujerumani, Ufaransa, Ureno, Ugiriki, Urusi, Uturuki na kwingineko.
Dalili zinaonyesha kuwa ndani ya miaka miwili
kumekuwa na kasi kubwa ya wachezaji wa Kihispania kusambaa kwenye nchi za
Ulaya. Dalili kuwa wanaweza kuwa watawala wa mchezo huo.
0 COMMENTS:
Post a Comment