Baba mzazi wa mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete amesema mwanaye sasa
amewanyamazisha waliokuwa wakiamini hana lolote.
John
Tegete ambaye ni Kocha Mkuu wa Toto African inashiriki daraja la kwanza amesema
mwanaye ana uwezo mkubwa wa kufunga na itakuwa vema akipewa nafasi.
Tegete
Jr aliifungia Yanga mabao mawili ilipoitandika Stand United mabao 3-0, Jumamosi
iliyopita mjini Shinyanga na kuifanya ipande juu katika msimamo wa ligi hiyo
kwa kufikisha pointi kumi.
Nyota
huyo ambaye alijiunga na Yanga akitokea Shule ya Sekondari Makongo, hivi sasa
ndiye anayeongoza kwa kuzifumania nyavu klabuni hapo pamoja na kwamba amecheza
dakika 20 tu.
Tegete
Sr alisema kuwa mwanaye huyo amewaziba midomo wale wote waliokuwa wakimchukia
na kumfanya akose nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga licha ya kuwa na
uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu kuliko mchezaji mwingine klabuni hapo kwa
hivi sasa.
Alisema
kitendo cha mwanaye huyo kuwa benchi muda mwingi bila ya kucheza kilikuwa
kikimuumiza sana na alikuwa akiwapigia kelele mara kwa mara viongozi wa Yanga
juu ya jambo hilo, lakini waliziba masikio kwa sababu tu ya chuki binafsi.
“Siku
zote nilikuwa nikimwombea mazuri mwanangu juu ya wale wanaomchukia kwa kila
nilipokuwa nikiwauliza kwa nini hachezi, waliniambia kuwa hachezi kwa sababu
anapokuwa uwanjani hufanya mzaha, jambo ambalo si kweli kabisa, Tegete hayupo
hivyo ila yeye ni mtu wa watu na hupenda kucheka na kutaniana na kila mtu.
“Hata
hivyo, pamoja na yote hayo, namshukuru Mungu, mwanangu ameonyesha kuwa yeye ni
bora zaidi katika kikosi cha Yanga hata kama wanamchukia lakini atabakia kuwa
bora,” alisema Mzee Tegete ambaye pia ni kocha mkuu wa timu ya Toto African ya
jijini Mwanza.







0 COMMENTS:
Post a Comment