Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya kufua umeme ya Pan African Power
Solution inayoimiliki kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),
imedhamini tuzo ya Mwanamichezo bora wa
chama cha Waandishi wa Habari nchini (Taswa).
Kampuni hiyo leo ilikabidhi
mfano wa hundi ya shilingi milioni 20, kwa uongozi wa chama hicho ikiwa ni njia
mojawapo ya kusaidia michezo hapa nchini.
Taswa ambayo imekuwa
ikiandaa tuzo ya mwanamichezo Bora, inahitaji kiasi cha shilingi milioni 120,
ili kufanikisha utoaji wa tuzo hiyo baadaye mwaka huu.
Akizungumza wakati wa
makabidhiano ya hundi hiyo, Mwenyekiti wa IPTL, Harbinder Sigh Sethi, alisema
wametoa msaada huo ili kuchangia tasnia ya michezo hapa nchini.
“ Siyo kwamba IPTL tuna
fedha nyingi sana, au ni matajiri sana, bali tunafanya hivi ili kuchangia
michezo hapa nchini.
“Tunayaomba na makampuni
mengine yajitokeze kwa ajili ya kuwasaidia Taswa, kwa kuwa jambo wanalofanya ni
zuri sana hapa nchini Tanzania. Huu kwetu ni mchango kidogo, lakini ni vizuri
na makampuni mengine yakajitokeza kusaidia,” alisema Sethi ambaye aliwahi
kushiriki mbio za magari za ubingwa wa Afrika.
Naye mwenyekiti wa Taswa,
Juma Pinto, ambaye alipokea hundi hiyo alisema wanaishukuru IPTL kwa msaada huo
kwani ni jambo jema kwa kampuni kama hiyo kujitokeza kusaidia michezo hapa
nchini.
“Bado tunahitaji kubwa
sana. Tunatakiwa kupata milioni 120 ili kufanikisha tuzo za mwaka huu. Ni
vizuri tukiwashukuru sana IPTL kwa msaada wao, tunajua kuwa utatufikisha sehemu
fulani.
“Tunaomba na makampuni
mengine yajitokeze ili kutusaidia kutoa tuzo ya mwaka huu kwa mafanikio
makubwa,” alisema Pinto.
0 COMMENTS:
Post a Comment