NGASSA, MMOJA WA VIUNGO WENYE KASI ZAIDI AFRIKA MASHARIKI NA KATI. |
Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazil, Marcio
Maximo, amewaandaa viungo washambuliaji Mrisho Ngassa na Simon Msuva kuwa ndiyo
chachu kubwa ya ushindi wake dhidi ya watani wao wa jadi Simba, katika mchezo
wao wa Oktoba 18, kwenye Uwanja wa Taifa.
Simba na Yanga watakutana katika mchezo wa
raundi ya nne wa Ligi Kuu Bara, huku zikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1,
katika mchezo wao wa mwisho wa ligi hiyo walipokutana katika uwanja huo msimu
uliopita.
Katika mazoezi ya Yanga ambayo yanafanyika
kwenye Uwanja wa Boko Veterani uliopo Boko nje kidogo ya Jiji la Dar, Maximo
ameonyesha kuwatumia zaidi viungo wake hao wenye kasi kupiga mipira ya
krosi kwenda kwa washambuliaji wake wanaoongozwa na Mbrazili, Geilson Santos ‘Jaja’
na kuwapa kazi rahisi ya kupachika mipira wavuni.
Katika mazoezi hayo, Maximo alitumia muda
mwingi kuwapa viungo hao mazoezi maalum ya kupiga krosi zitakazoleta madhara
katika lango la wapinzani wao huku akiwataka washambuliaji kuzitumia vizuri
krosi hizo.
Mbali na Msuva na Ngassa waliolifanya zoezi
hilo kwa muda mrefu na kwa ufasaha mkubwa, Maximo aliwatumia pia wachezaji
wengine katika zoezi hilo ili nao pia wapatapo nafasi ya kupiga krosi wapige
zenye madhara. Wachezaji waliofanya zoezi hilo ni pamoja na Andrey Coutinho,
Nizar Khalfan, Hussein Javu na beki Edward Charles.
0 COMMENTS:
Post a Comment