Na Saleh Ally
UKIINGIA kwenye Jumba la Makumbusho la Real
Madrid ambalo liko kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jijini Madrid, moja ya
vitu vinavyovutia ni glavu za kipa Iker Casillas.
Hii inaonyesha wanamjali, si unfair kwa
Kingereza au injusta kwa Kihispania. Na ndiyo jambo bora kwa maana ya kuonyesha
thamani.
Kumjali ni sehemu ya kuonyesha mambo makubwa
ambayo ameyafanya Casillas akiwa na klabu hiyo kwa miaka 15.
Miaka hiyo 15 ni ile ambayo ameichezea timu
kubwa na kufanikiwa kuibebesha makombe 17 yanayotambulika au kuheshimika.
Mfano Ligi ya mabingwa mara tatu, La Liga
makombe matano, Copa de Rey, mawili na mengineyo.
Kipa huyo anaaminika amewashawishi makipa
nyota katika nchi mbalimbali duniani wapatao 1,000 kuamua kuwa makipa.
Kwamba hata kama walikata tamaa, lakini
waliamua kuwa makipa kwa kuwa waliona yeye anafanya vizuri na wao wangeweza
kufanya hivyo au walitamani kuwa kama yeye.
Tena kinachovutia zaidi kwa Casillas kuwa ni
kipa ambaye ni nahodha, nahodha mwenye mikono ya bahati.
Asilimia 70 ya makombe yaliyotua Real Madrid
tokea mwaka 1999, yamepitia mikononi mwake kwa kuwa alikuwa nahodha.
Katika mechi ya juzi wakati Real Madrid
ilipoivaa Lodogoret ya Bulgaria
katika mechi ya Ligi ya Mabingwa
Ulaya na kushinda kwa tabu kwa mabao 2-1, Casillas alikuwa nyota wa mchezo
kutokana na kuokoa hatari nyingi.
Kinachoumiza kwake, au inaweza hata
ikawaogopesha wanasoka wachanga wanaochipukia ni vitendo vya baadhi ya
mashabiki wa Real Madrid kumzomea kwenye mechi kadhaa.
Walimzomea kwa kuwa alifanya makosa kadhaa, wakiamini yalisababisha
timu hiyo kupoteza ushindi katika mechi moja au kukaribia kupoteza.
Mashabiki wanaweza kweli kumzomea Casillas!
Kweli mpira haujali au hauna haki, Waingereza wanasema unfair na Wahispania
wanatamka injusta.
Kweli injusta, si haki kumzomea shujaa wa
miaka 15 kwa makosa mawili. Kwa nini binadamu wanasahau sana?
Shukurani ya binadamu ni kwa wakati husika
tu? Au huu ndiyo mfumo wa binadamu wanaopenda mpira? Jiulize kuzomewa
kunamsaidia au kumshusha zaidi?
Kikubwa ni kutenda haki, kuamini watu
wanakosea na wanaokosea wapewe muda kidogo wa kujirekebisha.
Linalotokea kwa Casillas linaweza kuwatokea
wachezaji hapa nyumbani lakini kuna mambo mawili ya kujifunza kila upande.
Kwanza kwa wachezaji, Casillas amekuwa
akizomewa, lakini hajaacha kujituma na kuendelea kufanya vizuri kwa kuwa
anataka kuwaziba midomo wanaozomea, hili ni funzo kwa wachezaji wa hapa
nyumbani.
Pili ni kwa mashabiki, kumzomea Casillas
ambaye anakuwa anpambana kwa ajili yao, ni kijishambulia wao wenyewe kwa kuwa
wakimchanganya, inayoathirika ni Madrid na ukweli ni kwamba, hastahili dhaharu
na manyanyaso hasa kutoka wa wale anaoamini anawapenda, pia wanampenda na
kumuunga mkono, kwani asipokuwa makini, watammaliza kabisa.
0 COMMENTS:
Post a Comment