MAMBO bado siyo mazuri kwa Kocha
wa Manchester United, Louis van Gaal, baada ya timu yake hadi sasa kushindwa
kwenda na kasi ile aliyokuwa anaitaka.
Kocha huyo awali alisema
kuwa timu yake inaweza kuzoea kasi anayoitaka yeye baada ya kupita miezi
mitatu, lakini hadi sasa linaloonekana kuwa tatizo kubwa kwake ni majeruhi na
siyo hali ya wachezaji kuzoea tena.
Wachezaji wa Manchester
United wamekuwa wakisumbuliwa na majeraha mara kwa mara msimu huu jambo ambalo
linazidi kumweka kwenye wakati mgumu kocha huyo raia wa Uholanzi.
Kwenye safu ya ulinzi ya
timu hiyo wachezaji wake Jonny Evans, Marcos Rojo, Tyler Blackett na Phil Jones
kwa sasa wapo nje kutokana na majeraha huku Chris Smalling akiwa fiti lakini
atashindwa kucheza kutokana na kuwa na kadi nyekundu.
Kocha huyo amekuwa
akilazimika kuwatumia wachezaji makinda Paddy McNair pamoja na kiungo Daley
Blind kama mabeki kwenye timu hiyo.
Lakini wakati mashabiki na
wachambuzi wengi wa soka wakitazama tatizo hilo, wamesahau kuwa tatizo kubwa
zaidi kwa United kwa sasa lipo kwenye safu ya ushambuliaji.
Kukaa nje kwa mshambuliaji Radamel
Falcao kutokana na kusumbuliwa na majeraha ni tatizo lingine kubwa sana.
Staa huyo raia wa Colombia,
aliichezea timu hiyo mchezo wa mwisho wakati walipopata sare ya mabao 2-2 dhidi
ya West Brom, kwenye mchezo huu alifanikiwa kucheza kwa dakika 18 tu akitokea
kwenye benchi.
Taarifa zimekuwa zikisema
kuwa, mchezaji huyo amekuwa akisumbuliwa na tatizo la goti siyo leo tu bali kwa
muda mrefu.
Inaelezwa kuwa staa huyo aliyesajiliwa
kwa mkopo akitokea Monaco ya Ufaransa, amekuwa akiwekewa barafu kwenye goti
hilo kila anapomaliza mazoezi ya timu hiyo hata anapoonekana kuwa fiti, jambo
linalozidi kutoa ishara mbaya zaidi.
Hali inaonekana kuwa bado
siyo nzuri kwa mchezaji huyu na suala la Manchester kumsajili kwa mkopo
walifanikiwa kucheza kamari yao vizuri lakini isiyo na faida.
Huko nyuma, Falcao amewahi
kusumbuliwa na tatizo la goti mara tatu tofauti, kwa mara ya mwisho ulikuwa
msimu uliopita ambapo alikaa nje ya uwanja kwa miezi nane na kushindwa kwenda
kwenye Kombe la Dunia.
Ni sahihi kusema kuwa United walicheza kamari yao vizuri
kumsajili kwa mkopo mchezaji huyo kwenye siku ya mwisho kabisa ya usajili
kuliko wangetoa kitita kikubwa na kumchukua moja kwa moja.
Lakini kwa kuwa walilipa
kitita cha pauni milioni 16, unaweza kusema kuwa ni mkopo usio na faida kama
atakaa nje kwa muda mrefu kama inavyotarajiwa.
Tatizo linalokuja sasa ni
kwamba inaonekana kuwa Falcao hana shida sana kwenye goti lake kama wengi
wanavyofahamu, bali kwa sasa anasumbuliwa na misuli ya nyuma ya mguu.
Kocha wa United, ameongeza
hofu baada ya kunukuliwa na Taasisi ya Habari ya la Reuters, akisema kuwa hana
uhakika kama mchezaji huyo ataweza kuichezea timu hiyo tena msimu huu, kutokana
na kusumbuliwa na nyama hizo.
“Siwezi kusema kuwa Falcao
atarudi lini uwanjani, inategemea na hali yake ya majeraha itakavyokuwa, kwa
sasa anasumbuliwa na nyama za nyuma za mguu, goti siyo sana.
“Lakini hata alivyokuwa fiti wakati mwingine tulikuwa
tunashindwa kumtumia kwa kuwa alikuwa amekaa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na
majeraha, hivyo tatizo kubwa lilikuwa kwenye balansi yake uwanjani,” alisema
van Gaal.
Hali halisi inaonyesha kuwa,
majeraha ya mchezaji huyo kwa sasa ni hatari, hawezi kuwa faida kwenye kikosi
cha United ambayo inamhitaji mtu kama huyo kwa nguvu kubwa kwa sasa.
Ukweli ni kwamba kwa sasa
safu ya ushambuliaji ya United siyo bora kwani kufahamu kuwa wanaweza kumpata
Falcao ndiyo maana United waliamua kumuachia Danny Welbeck na Javier Hernandez
wakaondoka.
Tatizo limekuwa kubwa kwao
kwa kuwa mshambuliaji wao waliyekuwa wanamtegemea msimu huu Robin van Persie
anaonekana kuwa chini sana kwa kiwango chake, lakini pia Wayne Rooney
anaonekana kupanda na kushuka.
Kinda anayepewa nafasi mara
kwa mara James Wilson yeye bado anatakiwa kuendelea kujifunza mambo mengi sana
kwa sasa na wakati mwingine akikosa kabisa uzoefu.
Kwa usajili wa mchezaji
ambaye alikaa nje kwa miezi sita kutokana na majeraha ili aje akakusaidie ni
lazima ukubali mambo mawili, kufanikiwa au kufeli, mpaka sasa United wamefeli,
labda baadaye sana.
0 COMMENTS:
Post a Comment