Na Saleh Ally
BENCHI la ufundi na wachezaji wa Simba wamekuwa kwenye presha kubwa
sana, mashabiki na wanachama walikuwa wakilalamikia sana matokeo ya timu yao.
Simba ilicheza mechi sita na kutoka sare zote, mwisho ikapata
ushindi katika mechi ya saba na kupunguza presha kupita kiasi.
Ukiangalia matokeo hayo ya mechi saba kupitia msimamo wa Ligi Kuu
Bara, hadi ligi inasimama baada ya kila timu kucheza mechi saba, utaona ni kama
maajabu.
Matokeo yanaonyesha mashabiki na wanachama walikuwa na presha
kupindukia ingawa takwimu zinaonyesha Simba haikufanya vibaya na haina tofauti
kubwa na Mtibwa Sugar, Yanga na Azam FC.
Tena kama utakwenda kwa mahesabu, kuna sehemu inaonekana Yanga na
Azam FC ziliboronga na Simba ikafanya vizuri zaidi yao.
Imeshinda moja:
Katika mechi saba ilizocheza, Simba imeshinda mechi moja tu na iko
katika nafasi ya saba kati ya timu 14 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
Pamoja na kwamba Simba ilishinda mechi moja na kuwa kati ya timu
zilizoshinda mechi chache zaidi katika mechi saba, ajabu inazipita hata timu
zilizoshinda zaidi ya mechi moja.
Timu zilizoshinda zaidi ya mechi moja lakini ziko chini ya Simba
kimsimamo, yaani kuanzia nafasi ya nane ni Polisi Moro iliyoshinda mechi mbili
na nafasi ya tisa ipo Mgambo iliyoshinda mechi tatu.
Stand United iko nafasi ya kumi ikiwa imeshinda mechi mbili hali
kadhalika Ruvu, iliyo katika nafasi ya kumi na moja.
Ndanda FC iko nafasi moja kabla ya mkiani na imeshinda mechi mbili.
Zimeshinda moja:
Timu nyingine ambazo zilishinda mechi moja kama Simba ni Prisons na
Mbeya City zote kutoka jijini Mbeya.
Maana yake Simba kwa ushindi, iliringana na timu hizo mbili lakini
Prisons ipo katika nafasi ya 12 na Mbeya City nafasi ya 14 na inaburuza mkia.
Hii inaonyesha bado Simba haikuwa na matokeo mabaya ya kutisha
tofauti na mashabiki wake walivyokuwa wakifikiria.
Karibu na Mtibwa:
Mtibwa Sugar ndiyo inayoongoza ligi kwa kuwa na pointi 15 kileleni.
Wakati Simba iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi tisa.
Tofauti ya Simba na Mtibwa Sugar ni pointi sita tu ambazo ni ushindi
wa mechi mbili. Katika soka lolote linatokea, iwapo Mtibwa itateleza mara moja,
Simba ikashinda, basi tofauti itakuwa ni pointi tatu tu. Utaona bado nafasi ya
kikosi hicho cha Phiri haikuwa mbaya kama mashabiki walivyoona.
Yanga & Azam:
Timu hizi mbili ndizo mashabiki wa Simba walikuwa wakizitazama ziko
wapi na zinakwenda vipi.
Yanga iko katika nafasi ya pili na Azam FC ya tatu. Kila moja ina
pointi 13, tofauti yao na Simba ni pointi nne tu!
Angalia pengo hilo, utagundua Simba haikufanya vibaya katika mechi
zake. Kwani inatakiwa ushindi mmoja na sare kuwafikia Azam na Yanga na hasa
kama watateleza na katika soka, kila kitu kinawezekana.
Utaona licha ya Simba kulalama sana lakini hawana tofauti kubwa kati
yao na Azam hali kadhalika Yanga.
Kila mechi pointi:
Simba na Mtibwa pekee ndiyo timu zilizovuna pointi katika kila mechi
kati ya saba walizocheza.
Maana yake, Simba na Mtibwa Sugar pekee ndiyo timu ambazo
hazikupoteza hata mechi moja hadi sasa katika msimu huu.
Unapozungumzia ubora wa safu ya ulinzi, bado unaweza kuiita safu ya
ulinzi ya Simba ni kati ya zile bora, kwa kuwa haijapoteza hata mechi moja.
Sare sita na ushindi mmoja, unataka nini!
Beki ngumu:
Ingawa Simba imekuwa ikilalamikiwa kwamba ina safu nyanya ya ulinzi,
ukweli ni kwamba haikuwa kama ambavyo watu walikuwa wakipiga hesabu za
harakaharaka.
Katika mechi saba, safu ya ulinzi ya Simba iliruhusu mabao sita.
Utaona iko katika nafasi ya saba lakini JKT Ruvu iliyo katika nafasi ya sita,
imeruhusu saba.
Coastal Union iliyo katika nafasi ya nne imeruhusu saba pia.
Ukiangalia tofauti kati ya safu ya ulinzi ya Yanga pia Azam, kamwe
hauwezi kuthubutu kuiita safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa nyanya.
Katika mechi saba, Yanga imeruhusu mabao matano, Azam imeruhusu
manne. Tofauti na Yanga ni bao moja, Azam ni mabao mawili tu!
Ukisema difensi ngumu zaidi imekuwa ni ya Mtibwa Sugar iliyopitisha
mabao matatu tu, wakati difensi nyanya ni ya Ndanda FC iliyoruhusu mabao 13!
Azam & Yanga:
Bado unaweza kusema safu za ulinzi za Yanga na Azam si makini kama
ile ya Simba.
Simba haijapoteza hata mechi moja kupitia mechi hizo saba. Azam FC
imepoteza mechi mbili katika saba! Hali kadhalika Yanga imepoteza mbili katika
saba.
Katika soka matokeo ya juu ni ushindi, saizi ya kati ni sare na ya
chini ni kupoteza.
Katika mechi saba, Simba haijagusa matokeo ya chini, bado iko kwenye
daraja la kati na la juu. Wakati Azam na Yanga, zimepita kote.
0 COMMENTS:
Post a Comment